Pages

Pages

Wednesday, July 10, 2013

Tamko lote la Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, juu ya kuandaa vijana wa kukilinda chama chama chao

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Freeman Mbowe.

MUHTASARI
Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu imeagiza kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima wanapewa mafunzo maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi maalum katika mikoa yote.
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAAMUZI YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA KILICHOFANYIKA TAREHE 06-07/07/2013 KATIKA HOTEL YA BLUE PEARL, DAR ES SALAAM.

Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ilikutana katika Kikao cha dharura kuanzia tarehe 06-07/07/2013 katika Hotel ya Blue Pearl Dar es salaam kujadili pamoja na mambo mengine Rasimu ya Katiba mpya na hali ya Siasa nchini.
Kamati kuu imejadili na kuyatolea maamuzi mambo mbalimbali kama ifuatavyo:

1:0. Hali ya Siasa Nchini.

Kamati kuu imepokea taarifa ya hali ya siasa nchini na kuzingatia mambo yafuatayo:

a) Shambulio la Bomu Arusha.

ü Kamati Kuu imesikitishwa na kulaani kwa nguvu zote tukio la Bomu Arusha lililosababisha watu wanne kuuwawa na zaidi ya watu 70 wengine kujeruhiwa vibaya.

ü Kamati Kuu imeridhika kwamba shambulio hilo lililenga kuwaua viongozi wakuu wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Freeman A. Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mheshimiwa Godbless J. Lema na viongozi na wanachama wengine wa CHADEMA waliohudhuria Mkutano wa kufunga kampeni za udiwani katika Jiji la Arusha pamoja na kuvuruga Uchaguzi huo na kuinyima CHADEMA ushindi mkubwa;

ü Kamati Kuu imeridhika kwamba ushahidi uliopo wa vielelezo na wa mashuhuda wa shambulio unaonyesha ushiriki wa moja kwa moja wa Jeshi la Polisi katika shambulio hilo;

ü Kamati Kuu imefadhaishwa na kauli ya Serikali bungeni iliyolenga kulikosha Jeshi la Polisi kwa kuhusika kwake na shambulio hilo dhidi ya CHADEMA na wananchi wa Jiji la Arusha na kuilaumu CHADEMA wakati CHADEMA ndio mhanga wa shambulio hilo;

ü Kamati Kuu imeshangazwa na kitendo cha Serikali kupuuza maafa yaliyowafika wananchi wa Arusha kwa kushindwa kushiriki katika mazishi ya wahanga wa mauaji ya Soweto na kuwashambulia kwa mabomu ya machozi, vipigo na maji ya sumu waombolezaji waliokusanyika kuwaaga marehemu waliouawa kwenye shambulio;

ü Kamati Kuu imesikitishwa na Rais Kikwete kuendelea kukaa kimya juu ya shambulio la Arusha na kushindwa kwake kuunda Tume huru ya Kimahakama kuchunguza kwa uwazi shambulio hilo. Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba ukimya huu wa Rais Kikwete na kushindwa kwake hata kuwatembelea wafiwa na wahanga wengine wa shambulio hilo ni ushahidi mwingine wa kuhusika kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali katika kupanga na kutekeleza shambulio la Arusha;

ü Kamati Kuu imefadhaishwa na kitendo cha Bunge la Jamhuri ya Muungano kuendelea na vikao vya Bunge kama kawaida; kukataa kutoa mchango wowote kwa wahanga na kushindwa kupeleka ujumbe wa Bunge kuwatembelea na kuwafariji wahanga na waathirika wa shambulio kinyume na utaratibu uliozoeleka wa Bunge kutambua na kushiriki katika majanga na misiba ya aina hii.

Kamati Kuu inautaka uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano uwaeleze Watanzania kama maafa ya shambulio la Arusha yalikuwa na tofauti yoyote na maafa ya shambulio la bomu la Olasiti, au na maafa ya mabomu ya Gongo la Mboto, ajali ya MV Skargit au maafa mengine yaliyosababisha Bunge la Jamhuri kuahirisha shughuli zake, kutoa michango kwa waathirika pamoja na kupeleka ujumbe wa Bunge kuwafariji wafiwa na wahanga wa matukio hayo;
Kutokana na maelezo hayo hapo juu Kamati kuu imeazimia kuwa:

• Iwapo Rais ataendeleza msimamo wa kutokuunda tume huru ya kimahakama, Ushahidi uliopo juu ya tukio la kurushwa Bomu Arusha utawekwa wazi muda utakapofika kwa wananchi wa Tanzania; vyama na mashirika ya kiraia ya haki za binadamu hapa nchini na ya nje ya nchi; ofisi za kibalozi za mataifa rafiki na Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa ili yaishinikize Serikali kuunda Tume huru ya Kimahakama kuchunguza shambulio hilo na matukio mengine ya mauaji yenye sura ya kisiasa ambayo yamehusishwa na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vya Serikali au vya Chama cha Mapinduzi;


2:0. Hali ya Wananchi wa Mtwara.

Kamati kuu imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa juu ya unyanyasaji, utesaji, ubakaji na uonevu wanaofanyiwa wananchi wa Mtwara hivi sasa na vyombo vya dola huku serikali ikikaa kimya juu ya jambo hili bila kukemea. Kamati kuu imejadili kwa kina namna wananchi wa Mtwara wanavyofanyiwa na vyombo vya dola na kufikia maazimio yafuatayo;

ü Vyombo vya dola vitimize wajibu wake wa kulinda amani na mali ya raia na siyo kuwatesa na kuwapiga wananchi kwa kuwasababishia vifo kinyume na Haki za Binadamu.

ü Serikali iwasikilize wananchi wa Mtwara na siyo kutumia ubabe, unyanyasaji, uonevu na mateso kama mbinu za kuhalalisha kukubalika kwake kwa wananchi.

ü Rais Kikwete alitangazie taifa “hali ya hatari” kwa mkoa wa Mtwara kama anaona kuwa Mtwara ni hatari kwa kiasi hicho cha kulitumia JWTZ kuzunguka mitaani na silaha za kijeshi ili taifa liweze kujua,Aidha kama jeshi la polisi limeshindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria atangaze kulivunja jeshi hilo mara moja.

ü Serikali iunde tume huru ya kuchunguza matukio ya mauaji,ubakaji,utesaji na ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyofanywa na vyombo vya dola na waathirika wote waweze kufidiwa kwa mujibu wa sheria.

3:0. Kauli ya Waziri Mkuu.

Kamati Kuu imejadili kwa kina kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba ni sahihi kwa Jeshi la Polisi nchini kuwapiga Wananchi wote wanaotumia haki zao za Kikatiba kupinga sera au maamuzi ya Serikali. Kamati Kuu imeazimia kuwa:

ü Kauli ya Waziri Mkuu imekiuka Katiba na sheria za nchi yetu zinazokataza Jeshi la Polisi kutumia nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na silaha na ambao wanatumia haki zao za kikatiba kufanya maandamano;

ü Kamati Kuu inaamini kwamba kauli ya Waziri Mkuu inatoa Baraka kwa Jeshi la Polisi kuendeleza vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya wananchi ambayo yamelifanya Jeshi la Polisi la Tanzania kutangazwa kuwa moja ya majeshi katili ya polisi katika Afrika Mashariki;

ü Kamati Kuu inaungana na wananchi, taasisi na mashirika ya kitaifa na kimataifa ambayo yamelaani vikali kauli hiyo ya Waziri Mkuu na inawataka wananchi, taasisi na mashirika hayo kuendelea kumlaani vikali Waziri Mkuu kwa kauli hiyo;

ü Kamati Kuu inaamini kwamba Waziri Mkuu amepoteza sifa za kuendelea kuwa Waziri Mkuu na inaungana na wananchi na taasisi ambazo zimedai Waziri Mkuu awajibike au awajibishwe kutokana na kauli yake hiyo. Aidha, Kamati Kuu inawaelekeza Wabunge wote wa CHADEMA washirikiane na Wabunge wengine wote wenye mapenzi mema na nchi hii na ambao wanaamini katika utawala wa sheria waanzishe mchakato wa kumpigia kura ya kutokuwa na Imani Waziri Mkuu kupitia Bunge;

ü Kamati Kuu imewataka Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii ya watanzania kupuuza kauli ya Waziri Mkuu katika utekelezaji wa kazi zao kwa kuwa kauli hiyo ni ya uvunjifu wa Katiba na Sheria na inachochea uvunjifu wa amani.

4:0. Uchaguzi wa Madiwani.

Kamati Kuu imepokea taarifa kuhusu ushiriki wa CHADEMA katika Uchaguzi wa Madiwani uliofanyika tarehe 16/06/2013 katika kata 22.

ü Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti na uongozi wa Kanda mbalimbali za CHADEMA kwa maandalizi mazuri katika Uchagzuzi huo uliosababisha CHADEMA kuwapokonya CCM ushindi katika kata 4 ilizokuwa imeshinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kamati Kuu imewapongeza wananchi kwa kuipatia CHADEMA kura asilimia (47.7%) dhidi ya CCM (49%) na (3.3%) za CUF.

ü Kamati kuu imesikitishwa na vitendo vya fujo walivyofanyiwa viongozi, wagombea pamoja na Wanachama mbalimbali katika sehemu mbalimbali palipo fanyika Uchaguzi. Kamati Kuu imesikitshwa na kulaani vitendo hivyo vikiwemo vya watu kukatwa mapanga , kuchomwa visu na kubakwa kwa akina Mama na vijana wahuni walioandaliwa na Chama cha Mapinduzi.

ü Kamati Kuu imelaani vitendo hivyo vya kinyama vilivyofanywa mbele ya jeshi la polisi na Wakuu wa Wilaya.

ü Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi ya wagombea, Wanachama na viongozi wa CHADEMA, Kamati Kuu imeagiza kwamba kitengo cha ulinzi cha Chama “Red Brigade” kiimarishwe zaidi kwa kuhakikisha kuwa vijana wote wa Red Brigade Nchi nzima wanapewa mafunzo maalum ya UKAKAMAVU yatakayoandaliwa katika Makambi maalum katika mikoa yote.

ü Kamati Kuu imejadili maandalizi ya Uchaguzi wa madiwani katika kata nne (4) katika Jiji la Arusha. Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa juu mipango inayofanywa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo na viongozi wengine wa CCM mkoani Arusha katika kuhujumu zoezi la Uchaguzi kwa kuwatisha wapiga kura kwa kutumia polisi na vijana wa Green Guard siku ya uchaguzi.

ü Kamati Kuu inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuchukua hatua stahiki kuzuia harakati za polisi na CCM za kuvuruga Uchaguzi na kutaka kujipatia ushindi kwa njia za hila. Aidha Kamati kuu imelitaka jeshi la polisi kuheshimu maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na Serikali, Tume ya uchaguzi na vyama vya siasa.

ü Kamati Kuu imesikitishwa na Tume ya Uchaguzi kushindwa kuwazuia CCM kuendelea na kampeni za Uchaguzi huku wakiwa wamezuia kampeni hizo kwa vyama vingine.

ü Kamati Kuu imeendelea kuwapa pole wananchi wa Arusha kwa matukio mabaya wanaofanyiwa na serikali ya CCM mkoani humo, na imewapongeza kwa kusimama kidete katika kulinda haki na ukweli.

ü Kamati Kuu imewaomba wananchi wa Arusha wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura tarehe 14 Julai 2013, na imewataka wabunge wote washiriki katika kusimamia zoezi la upigaji kura na uhesabuji kura siku ya Uchaguzi na wananchi wajitokeze kwa wingi kulinda kura bila hofu.

5:0. Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kamati Kuu imejadili kwa kina sana maudhui yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba;

• Kamati Kuu imetambua kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya;

• Hata hivyo, Kamati Kuu imetambua na kuainisha mapendekezo mengine ya msingi ambayo yanastahili kuboreshwa zaidi katika Rasimu hiyo;

• Msimamo na maazimio ya Kamati Kuu juu ya Rasimu ya Katiba Mpya yameainishwa na kuchapishwa katika kijitabu maalumu ambacho kitazinduliwa katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika siku, tarehe na mahali patakapo tangazwa hapo baadaye.


Imetolewa na:

……………………….

Freeman A. Mbowe, (MP)

Mwenyekiti Taifa



No comments:

Post a Comment