Pages

Pages

Wednesday, July 10, 2013

MGODI UNAOTEMBEA:REA waiangalie upya sera yao ya umeme vijijini



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAJUZI wa mambo na wanaharakati wanaendelea kuumiza vichwa vyao katika baadhi ya mambo yanayochelewesha maendeleo ya Tanzania, licha ya kuwa na mbiu nyingi, ikiwamo hii ya Maisha bora kwa kila Mtanzania.
Umeme unavyoweza kuleta maisha bora kwa Watanzania.
Kauli mbiu hii ilianzishwa na kusimamiwa kwa ukaribu kabisa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, wakati huo anawania nafasi hiyo kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo
Kikwete alibanwa kwa karibu na wagombea kutoka vyama mbalimbali, akiwamo Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kutoka Chama Cha Wananchi (CUF), Dk Willbroad Slaa kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema na wengineo.

Sio lengo langu kuelezea mbiu hizo au mchakato wa urais, ila jinsi sera ya umeme vijiji inaposhindwa kufanyiwa kazi kwa ufanisi na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Hali hii inasababisha wananchi wengi wa vijijini waendelee kuishi maisha magumu. Wapo wapo tu. Leo hii Mtanzania anayeishi vijijini anashindwa kumiliki hata simu ya mkononi maana ni gharama kwake.

Kama kijiji kina umeme, walau maisha yanaweza kuwa rahisi kidogo, maana wajasiriamali wengi wanaweza kujikwamua, hata kwa kugandisha ice cream, kuuza juisi, soda na maji baridi.

Kama hivyo haitoshi, bado huduma mbalimbali zinazohitaji umeme zinaweza kuanzishwa na kuwanufaisha watu wote, ndio maana kila Mtanzania ana haki ya kupata nishati ya umeme.

Mwishoni mwa mwaka jana, Wakala wa Umeme Vijijini REA, walitoa matangazo katika baadhi ya magazeti ya Mwananchi na Rai Mwema, kati ya Jumanne ya Desemba 18 na 19 kwa kurasa mbili ya umeme vijijini.

REA walielezea mikakati ya mwaka 2013 ambapo vijiji kadhaa vilitajwa kupelekewa umeme kwa ajili ya kuwasogezea huduma hiyo, ikiwa ni tamko lililotolewa na REA, wakisisitiza kuwa mpango huo utakuwa tunu kwa 
Watanzania wote, hususan wale wanaoishi maeneo ya vijijini.

Ikumbukwe kuwa, huduma ya umeme katika Taifa hili bado si ya uhakika na ndio maana mara kwa mara kunatangazwa mbinu na kuwataka wananchi watowe maoni juu ya nishati ya umeme.

Inashangaza. Mtu anaombwa atowe maoni anataka TANESCO iweje, wakati tangu azaliwe hajawahi kutumia nishati ya umeme nyumbani kwake.

Huyu atowe maoni yanayohusu nini? Au aitusi serikali, REA na TANESCO yao? Haya ni matamko ya kisiasa yanayoleta wasiwasi mkubwa na suala la maendeleo ya Watanzania wote, kwa kupitia nishati ya umeme ambayo ndio inayoweza kuukwamua uchumi wetu unaojikongoja siku baada ya siku.

Angalia, Waziri wa Nishati na Madini Tanzania, Sospeter Muhongo anakutana na wadau wa umeme Mlimani City.

Kikubwa kinachojadiliwa hapo ni siasa, maana baada ya majibu yake mara nyingi huishia kwenye karatasi, maana wananchi wengi wa vijijini wanaishi maisha ya dhiki kwasababu ya kukosa nishati hii muhimu.

Nasema haya baada ya hata vile vijiji ambavyo vinasifa ya kupewa umeme, lakini wanaendelea kuwekwa visogoni na serikali kwa kupitia REA wenyewe ambao ndio kila kitu katika kuwasambazia wananchi hao.

Kwa mfano, ukitoka katika wilaya ya Korogwe kwenda Handeni, kijiji cha kwanza kinachoitwa Komsala, hiki hakina umeme tangu nchi ipate uhuru, licha ya kupitwa na njia mbili za umeme.

Ipo njia inayopeleka umeme wilayani Handeni, ambapo vijiji mbalimbali vya mbele kama vile Kwamatuku, Sindeni, Misima na Makao Makuu ya wilaya hiyo, hivyo inashangaza kwanini vijiji vya nyumba yake havina umeme?

Pia ipo ile njia kubwa ya umeme iliyopita pia katika kijiji cha Komsala, hivyo hakika ni aibu kama REA wanashindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi sambamba na kuwasogea maisha bora wananchi wao.

Ukiangalia yale matangazo yaliyotolewa na REA mwaka jana mwishoni, utagundua kuwa yalikuja baada ya wadau wa umeme sambamba na wananchi wa vijiji vya Komsala na Kwakiliga kulalamika kutengwa licha ya kuwa kwenye (Underline Transformers ).

Sera ya umeme vijijini inasema vile vinavyopitwa na njia ya umeme, yani Underline Transformers vinastahili kupewa huduma hiyo, badala ya kuwa watazamaji wa nguzo za umeme zinazopita kando ya nyumba zao na kuelekea kwingine.

Kama hivyo ndivyo, kulikuwa na haja gani REA kuwadanganya wananchi wa vijijini, hasa hivi vya Komsala na Kwakiliga, ukizingatia kuwa wao wenyewe walitangaza mkakati wao wa kuwaunganisha mwaka huu ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Ukiacha Komsala, vijiji vingine vilivyotajwa kupewa umeme ni Msasa, Kwedisemi, Kwamkole, Mkuyuni, Kwinji, Teleguru na Kisangasa.

Katika wilaya ya Korogwe, REA ilitangaza kuunganisha umeme kwa vijiji vya Kilole Mzee, Kwasunga, Kwamaraha, Batini, Mswaha, Kwamtawazi, Mgobe, Lusanga, Kieti, Vugiri na Bagamoyo Ambanguru.

Ni aibu kama vijiji vinavyopitwa na njia ya umeme vikashindwa kupatiwa huduma hiyo tangu Tanzania ipate Uhuru wake, ingawa kunakuwa na sera za kila zinazotangazwa na kuzua maswali na taharuki za aina yake katika Taifa letu, ukizingatia kuwa Bajeti ya 2013/2014 haijavilenga vijiji vingi, vikiwamo vile vilivyotajwa kutekelezewa mwaka huu.

Tangazo lenye kurasa mbili linapotoka katika gazeti hapa nchini ni zaidi ya Shilingi Milioni nne, hivyo linapotoka katika magazeti mawili, kama vile Mwananchi na Rai Mwema, REA walitumia kiasi kisichopungua Milioni nane, kama majibu yaliyoandikwa na wadau wa umeme katika gazeti la Mtanzania.

Gharama hizo zingetumika vizuri, walau zingeweza kununulia transformer moja kwa ajili ya kijiji kimoja kilichokuwa kwenye Underline Transformers, kama hiki cha Komsala, ambapo kina sifa zote na kipo karibu na wilaya ya Korogwe, licha ya kuwa chini ya wilaya ya Handeni.

Lakini si kwa REA. Fedha hizi zimetumika bure tu, ukizingatia kuwa hata yale yaliyochapishwa katika matangazo waliyotoa yameshindwa kutekelezwa kwa namna moja ama nyingine.

Hatuwezi kukubaliana na suala la matamko kama walivyotangaza kuwa jumla ya shilingi bilioni 826.1 zilitengwa kwa ajili ya upatikanaji wa umeme na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati.

Baadhi ya miradi iliyotekelezwa ni pamoja na: kuanza ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ikijumuisha ujenzi wa kituo cha kupokelea gesi Kinyerezi; kukamilisha ujenzi na kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito katika vituo vya Ubungo - Dar es Salaam (MW 105) na Nyakato - Mwanza (MW 60); kuendeleza miradi ya umeme vijijini katika mikoa 16; na kuendeleza upembuzi yakinifu katika miradi ya Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Liganga.

Aidha, hadi kufikia mwezi Desemba 2012, kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Grid ya Taifa kilikuwa MWh 5,759,756 ikilinganishwa na MWh 5,153,400 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 11.8.

Mara nyingi maneno kama haya yanakuwa ni porojo tu ili siku ziende. Hakuna mipango kabambe na ile inayotekelezeka.

Na ndio maana malalamiko yamekuwa mengi kutoka kwa wananchi na kuwa chuki dhidi ya serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Umeme ndio kila kitu, ndio maana katika mjadala wa Bajeti ya mwaka 2013/2014, wabunge walipigia kelele juu ya nishati ya umeme, hasa katika maeneo ya vijiji ambapo huko kumekuwa na kero sugu.

Wananchi ambao simu zao za mkononi zinahitaji gharama za kupelekwa mjini ili zichajiwe na kuwafanya waishi kwa tabu na maisha ya kubahatisha.
Kwa mfano, wananchi wengi wa kijiji cha Komsala, wanalazimika kwenda Korogwe Mjini ili wachaji simu zao, kusaga nafaka na huduma nyingine.

Kwa mtindo huu, utajiuliza ile kauli mbiu ya Maisha bora imetokea wapi? Itaishaje? Je, serikali ya CCM inafahamu haya yanayoendelea?

Hivi kweli wanakosa umeme wakati kijiji chao kinajitosheleza, huku juu ya nyumba zao ukipitishwa umeme unaokwenda mjini, yani Handeni Mjini.
Wananchi hawa wana tofauti gani na wengine wanaoishi kwa raha hasa maeneo ya mjini? Je, tunasahau kuwa wananchi wa mjini kwa asilimia kubwa wanahitaji uwapo wa vijijini?

Nini matarajio ya wananchi hawa kama Bajeti ya mwaka huu vijiji vya aina hii havijaguswa, wakati mwaka jana mwishoni REA walitolea ufafanuzi na kugusia mkakati huu wa underline transformers kwa kijiji hiki cha Komsala, ambacho licha ya kuwa wilayani Handeni, lakini huduma nyingi, ikiwamo TANESCO wanahuumiwa na wilaya ya Korogwe?

Je, waendelee kusubiria kama watoto wadogo wa ndege? Wananchi hawa wamekosa nini kwa serikali yao chini ya Kikwete, maana yeye mwenyewe aliahidi na mawaziri wake wanasisitiza juu ya umuhimu wa umeme vijijini?

Kama vyenye vigezo vyote vinanyimwa umeme kwa makusudi, itakuwaje majirani zao kwa Kweingoma, ambao hawa njia ya kawaida ya umeme haijapita kijijini kwao?

Waziri Muhongo anayajua haya? Wataalamu wake wanampa picha gani kabla ya kuandaa ‘project’ ya umeme vijijini?

Mtindo huu sio mzuri, maana tunazalisha wananchi wenye chuki na serikali yao. Ni vyema Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na wadau wake, kama vile REA na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania TANESCO kuliangalia suala hili kwa kina.

Umeme ndio kila kitu, ndio maana ziara ya Rais wa Marekani, Barack Hussein Obama Tanzania, ilizingatia zaidi nishati ya umeme, akisisitiza ndio inayoweza kulikwamua Taifa.

Maneno ya Obama yanakuja ikiwa ni ishara mbaya kwa serikali ya Tanzania, maana hakuna mipango ya wazi zaidi ya siasa kuchukua nafasi kila wasaa, ndio maana licha ya baadhi ya vijiji kutimiza masharti na vigezo vya kupatiwa umeme, ila wananyimwa.

Huu sio mpango mzuri unaoweza kuwapatia maisha bora Watanzania na wale wanaoishi maeneo ya vijijini, hivyo REA lawama hizi ni zao.
+255 712053949

No comments:

Post a Comment