Pages

Pages

Monday, June 24, 2013

Wadau wa soka, TFF wamlilia nyota wa zamani wa Taifa Stars

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Cosmopolitan na Taifa Stars, Mathias Kissa (84) kilichotokea leo alfajiri (Juni 24 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
                        Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani enzi zake, Kissa akiwa na timu ya Tabora alitamba katika michuano ya Kombe la Taifa wakati huo ikiitwa Sunlight Cup. Alikuwa akicheza katika nafasi ya ulinzi.
Baadaye alijiunga na Cosmoplitan ya Dar es Salaam, na pia kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ambapo enzi zake akiwa na wachezaji kama Yunge Mwanansali wakiiwakilisha Tanganyika na baadaye Tanzania Bara walitamba katika michuano ya Kombe la Chalenji wakati huo ikiitwa Gossage, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

Kissa ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa upande wa Tanzania, tuzo inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) alikuwa ndiye mchezaji msomi kupita wote wakati akichezea timu ya Taifa akiwa amehitimu elimu ya Darasa la Kumi.

Kwa mujibu wa binti yake, Erica, marehemu ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi (stroke) alioupata miaka mitano iliyopita, na kisukari. Baadaye alipata kidonda ambacho ndicho kilichosababisha kifo chake.

Msiba uko nyumbani kwa marahemu, Masaki, Mtaa wa Ruvu karibu na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST). Maziko yatafanyika keshokutwa, Jumatano (Juni 26 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kisa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Cosmopolitan na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Kisa mahali pema peponi.

No comments:

Post a Comment