Pages

Pages

Monday, June 24, 2013

Bunge lapitisha Bajeti ya 2013/2014


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BUNGE leo limepitisha Bajeti ya Shilingi Trilioni 18.2, kwa ajili ya kutumika mwaka wa fedha wa 2013 na 2014, huku Wabunge 35 wakisema hapana katika mchakato wa kuipigia kura bajeti hiyo.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa.
 Aidha, Bunge zima lilikuwa na wabunge 270, huku 35 wakiikataa na wabunge 235 kusema ndiyo.

Kwa sababu hiyo basi, serikali sasa itakuwa imepitisha bajeti yake, huku Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, akitumia dakika kadhaa jioni ya leo kujibu hoja za wabunge, yakiwamo malalamiko ya msamaha wa kodi kwa bajaj na kusema kuwa wamesikiliza maoni ya wabunge.


Mara baada ya mchakato huo wa upigaji wa kura kumalizika, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitumia fursa hiyo kuikumbusha Wizara ya Fedha juu ya kusimamia vyema fedha hizo kwa ajili ya kutumika kama zilivyopangwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo, kulikuwa na burudani ya aina yake katika upigaji wa kura wa kuipitisha bajeti hiyo, hasa pale sauti za baadhi ya wabunge kusikika zikisema ‘maandamano’ na kushangaza kwa kiasi fulani.

Wa kwanza kuulizwa juu ya kuikubali ama kuikataa bajeti hiyo alikuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda, ambaye bila ajizi aliipitisha moja kwa moja na kufuatiwa na mawaziri na manaibu waziri, ambapo baadaye walifuata wabunge waliokuwa bungeni.

Hata hivyo, ukiacha Mbunge machachali, Tundu Lissu kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyeipitisha bajeti hiyo, wabunge wengi wa chama chake hawakuwapo bungeni.

Ndio hao waliokuwa wakiitwa na kusikika wabunge waliokuwapo wakisema maandamano na kuleta kicheko kwa wabunge wengine bungeni na wale waliokuwa wakifuatilia kikao hicho kwa televisheni.

No comments:

Post a Comment