Pages

Pages

Monday, June 24, 2013

Serikali yasema shule za kata zinapunguza mimba na ongezeko la watu


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI kwa kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, imetangaza kuwa uwapo wa shule za Sekondari za Kata, zinapunguza uingiaji wa mimba kwa watoto wa kike.
Stephen Wasira, akiwa Bungeni Dodoma, picha na Maktaba yetu.
Akizungumza Bungeni mjini Dodoma, Wasira alisema kwa sababu hiyo ipo haja ya jamii kuzitumia zaidi kwa kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanasoma kwa ajili ya maisha yao.

Alisema mtoto wa kike akiishia darasa la saba, uwezekano wa kupata mimba ni mkubwa, huku utaratibu huo ukichangia ongezeko la watu duniani, hasa nchini Tanzania.

“Wengine wanazisema shule za kata, lakini zimechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya watoto wetu wasome na kuacha kupata mimba wakiwa katika umri mdogo.

“Mara nyingi binti akikomea darasa la saba tu, kupata mimba kwake ni rahisi, hivyo jamii iendelee kuwasimamia zaidi watoto wetu ili wasome zaidi kwa ajili ya maisha yao, huku katika suala la uongezeko la watu likipungua kwa kiasi Fulani,” alisema Wasira.

Bunge la Bajeti linaendelea mjini Dodoma, huku wiki hii kuanzia leo Jumatatu, Bajeti hiyo ya mwaka 2013/2014 ikitarajiwa kupitishwa kama ratiba inavyojulikana.

No comments:

Post a Comment