Pages

Pages

Monday, June 24, 2013

SIWEZI KUVUMILIA: Mpira ni pesa, Tanga Cement waidhamini timu ya Coastal Union


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU kama Coastal Union yenye maskani yake Tanga, ni wazi utaamini kuwa inanufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa kiwanda cha saruji kinachojulikana kama Tanga Cement.
Kikosi cha timu ya vijana, Coastal Union
Hii ni kwasababu wote wanategemeana. Tanga Cement kama kiwanda, kinaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Coastal Union.

Timu hii tishio katika soka nchini na yenye historia kubwa tangu kuanzishwa kwake, inatembelea basi dogo aina coaster lenye maandishi ya aina mbalimbali, yanayoelezea bidhaa za kampuni hiyo.

Hii ni kwasababu kiwanda hicho ndicho kilichonunua basi hilo na kuwapa timu hiyo ya Coastal Union, maarufu kama ‘Wagosi wa Kaya’.

Hata hivyo, tangu kukabidhi kwa basi hilo, hakuna msaada mwingine 
wanaotoa kwa timu hiyo. Awali nilifikiri kuwa wao ndio wadhamini wakuu kwa timu hiyo kongwe mkoani Tanga.

Hakika siwezi kuvumilia, maana licha ya Coastal Union kujitolea kwa kiasi kikubwa kwa kampuni hii ya saruji ya Tanga Cement, kuwatangaza kila mahali, ila si wadhamini wao.

Ndio hapo ninapoanza kushikwa na wasiwasi juu ya wadau wetu wa michezo Tanzania. Kwa Tanga Cement, kama inashindwa kuwadhamini Coastal Union, inataka kudhamini nani?

Wao ndio wanaofanya kazi kwa pamoja jijini Tanga. Wanategemeana kwa kila kitu. Nilifikiria watu wa masoko wangeangalia mtaji wa mashabiki na nafasi ya Coastal kuwatangaza kirahisi.

Coastal wanatoka Tanga na kuelekea mikoa mbalimbali ya Tanzania, wakitangaza bidhaa za Kampuni hiyo yenye mafanikio makubwa sokoni.

Sina lengo la kuwalaumu Tanga Cement wala kulazimisha, ila ni ushauri tu, maana najua nao wanaweza kunufaishwa zaidi na timu hiyo ya Wagosi wa Kaya katika soka Tanzania.

Huu ndio ukweli. Japo kuwa wamejitolea wenyewe juu ya basi hilo waliloipa timu hiyo, ila isiwe mwisho kuwasaidia ama kuwadhamini moja kwa moja.
Nasema hivi maana timu za mikoani zinakabiriwa na changamoto nyingi mno, hasa ukosefu wa fedha za kujiendesha.

Ndio maana licha ya baadhi yao kuwa na wachezaji wenye uwezo wa juu, ila nguvu zao zinaishia ukingoni, maana hakuna nyota wa soka anayeweza kucheza soka akiwa na njaa, ama mawazo familia yake.

Timu kama vile Toto African ya Mwanza, Villa Squad ya Kinondoni, zina njaa ya pesa, ukiacha zile za jeshi, Azam FC, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zinazomilikiwa na wenye nazo.

Kama hivi ndivyo, ni wakati wao basi wadau wa mikoani, matajiri kwa kupitia Kampuni zao, hasa Tanga Cement kuingia makubaliano ya wazi juu ya kuwadhamini Coastal Union ya jijini humo.

Hii itasaidia mno kuwafanya wachezaji waonyeshe kiwango cha juu zaidi. Hii itazidi kuwaletea heshima ukiacha basi waliloipa timu hiyo.

Tangu walikabidhi gari hilo kwa Coastal Union, wamekuwa wakipata matangazo mengi, hasa kwa kuona vijana hao wanajulikana na kuheshimika kwa kiasi kikubwa katika soka Tanzania.

Nikiwa kama mdau wa michezo, ni wakati huu sasa kuwakumbusha juu ya kuwekeza katika michezo, ukiwapo mpira wa miguu, hasa katika timu ya Coastal Union ya Tanga.

Ni wakati wao sasa kuingia katika udhamini, badala ya kusaidia, kama walivyojitolea katika kunununua basi hilo lisilozidi Milioni 50.

Milioni 50 kwa matangazo haichukui hata mwezi mmoja, kwa kuangalia na gharama zinazohitajika juu ya biashara hiyo, ila kwa Tanga Cement wao wameweza kujitangaza kwa miaka miwili sasa kutokana na nembo za bidhaa zao kutembea kila kona kwasababu yaa mgongo wa klabu ya Coastal Union.

Huu ndio ukweli wa mambo, maana hakika nimeshindwa kuvumilia, ukizingatia kuwa Tanga Cement wana kila sababu ya kuidhamini Coastal Union.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment