Pages

Pages

Saturday, June 29, 2013

Ni ujinga wasanii kutumia vifo kuuza sura



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA msemo unaosema kuwa siku zote uungwana ni vitendo. Kama msemo huu ni uongo, basi pia upo karibu na ukweli. Katika jamii yetu, wapo baadhi ya wasanii ambao wana tabia ya kupenda kuuza sura msibani, yaani kujionyesha.

 
Msanii Aunt Ezekiel. Note, matumizi ya picha hizi katika makala haya sio kwamba hawa ndio walengwa, ila zimetumika kama kufikisha kilio hiki kwa wasanii wote Tanzania.

Ukitaka kuwajua hawa, wala huwezi kupata tabu, maana siku zote huhudhuria kwenye misiba ya watu wanaojulikana. Kama si wao kufariki, basi ndugu zao.
                                  Rose Ndauka
Wakifika hapo, hawana kingine wanachofanya zaidi ya kupita katika makundi ya watu ili waonekane na kunyooshewa vidole. Mbaya zaidi, hata aina ya mavazi wanayovaa pia ni tatizo.
                                               Wema Sepetu
Jambo hili limekuwa likiwakera watu wengi kupita kiasi. Na baadhi yao hufikia kuanza kuwadharau wasanii hao wanaona hakuna mahala pengine kwa kuuza sura zaidi ya msibani.

Wasanii wa aina hiyo ni vigumu kuhudhuria msiba wa msanii mwenye jina la kati au asiyekuwa na jina kabisa. Ngoja niwe muwazi ili nieleweke katika makala haya.


Binafsi siamini kama msanii ni yule mwenye umaarufu, bali hata wale ambao si wengi wanawafahamu. Japo si lazima mtu kuhudhuria msiba, hasa kama sio hulka yake, lakini akiamua kwenda sharti kwanza ajiheshimu mbele ya hadhira.


Katika misiba wanakwenda watu wa kila aina. Wengine hupenda nidhamu kwa kila wanayemuona. Hili limetokea mara kadhaa hapa nchini. Kwa mfano, wakati marehemu Steven Kanumba anafariki, tuliona jinsi wasanii wetu, hasa wasichana walivyoshindana kuvaa vinguo vya ajabu na kujikalisha bila kuangalia mbele.


Tuliona matiti yalivyonyanyuliwa kwa vigauni visivyokuwa na staha wala soni mbele ya jamii inayoheshimika. Awali tulijua labda ni Jiji la Dar es Salaam, ila nikashangaa kuona hayo yakifanyika pia katika msiba wa Hussein Mkiety, maarufu kama Sharomilionea.


Kijana huyu alikufa kijijini kwao na kuzikwa huko huko siku mbili baadaye, wilayani Muheza. Muheza ilijaza wahuni. Wale walioguswa na kuamua kuhudhuria, walishindana pia kuuza sura.


Hata hivyo haitoshi, bado hayo yaliendelea katika msiba wa msanii Juma Kilowoko, maarufu kama Sajuki, bila kusahau Albert Mangwea ‘Ngwair’, aliyezikwa mkoani Morogoro.


Ukiangalia kwa haraka utagundua hawa ni wasanii maarufu, ndio maana wenzao wapenda kuuza sura wakaona ni vyema nao wakahudhuria kwa ajili ya kuuza sura.


Ndio maana msiba wa msanii Jaji Khamis ‘Kash’, Hassan Kihiyo waliyotangulia kuzikwa siku tatu kabla ya Langa Kileo, tulishangazwa na idadi ndogo ya wasanii waliokwenda kuwazika.

Ni ishara gani? Je, ndio kusema hawa wasanii hawana mvuto kiasi cha kugusa watu wengi? Hili ni jambo la kushangaza mno katika jamii iliyostaarabika.


Wasanii wa aina hii, wale wanaoangalia idadi ya watu ndio wahudhurie kazi za kijamii hakika hawana nafasi. Ni wakati wao sasa wajue kuwa kuuza sura kwenye msiba si uungwana.


Wao kama kioo cha jamii, lazima waishi kwa heshima ili kila mmoja ajaribu kuiga kutoka kwao.
Lakini ni wavivu kuhudhuria misiba ya watu wa kawaida na wakihudhuria basi utaona wakishindana kuonyesha sehemu za miili yao.


Nani kasema wadau na mashabiki wanakwenda kwenye msiba kwa ajili ya kutaka kuwaona miili yenu? Sehemu pekee za kutinga mavazi yasiyokuwa na nidhamu ni baa.


Sehemu za starehe vaeni mnavyotaka lakini si kwenye misiba. Kitendo hicho si cha kiungwana, hivyo ni wakati wao sasa kukaa na kuona jamii inawahitaji.


Tumechoka vituko kutoka kwa wasanii wa Tanzania. Kwanini kila siku malalamiko ni kwa wasanii? Huu ni wakati wa mabadiliko kwao. Wale wanaopenda kuuza sura kwa kupitia msiba washindwe.


Wamrudie Mungu, maana kufa kupo na kila mmoja lazima awe chakula cha udongo.
Sasa ole wenu wale msiokuwa na heshima mbele ya vifo.
kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment