Pages

Pages

Saturday, June 29, 2013

MAMBO FULANI MUHIMU:Ukijirahisi, inaweza kuwa balaa kwako



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI Jumamosi nyingine msomaji wangu tunakutana tena katika safu hii, kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano na maisha yetu ya kila siku.

Hatua ya muonekano wa picha hii inakuja kama kila mmoja ameamua kwa ridhaa yake pamoja na kujiridhisha kuwa hapo ndipo mahali sahihi.

Hiyo ni kwa sababu jambo hili linawagusa watu wengi katika jamii, hivyo kwa kulijadili tunaweza kupeana hili na lile kwa ajili ya kuishi maisha ya furaha.



Wapo wanaojichanganya na kuishi kwa presha katika mitaa yao, hasa pale wanaposhindwa kuwa makini katika uamuzi unaohusu mambo ya mapenzi.



Kwenye mapenzi ya kweli, kila kitu kinasema.
Msomaji wangu mpendwa, katika jamii wapo baadhi ya kina dada wanaojirahisi wanapowaona wanaume ambao ni machaguo yao halisi.

Wale ambao kwa kawaida wanawapenda na kuwahitaji, ingawa wanashindwa kuwapa ukweli katika kipindi cha mwanzo cha uhusiano wao huo.

Wanaanza kujichekesha kwao. Hujilainisha kwa kila aina, huku wakishindwa kubaini hisia zao na za wale wanaowapenda. Ndugu yangu, kumtamkia mwanaume au kuonyesha upendo wake kwake, ni jambo moja na kujirahisisha pia ni jambo jingine.

Wewe kama mwanamke, elewa unatakiwa uheshimu hisia zako kwa kujua vipi unaweza kufikisha ujumbe au kumweleza mwanaume, lakini tu, asifikirie vingine.

Nasema hivyo kwa sababu, kujichekesha ovyo ukiamini utafikisha ujumbe wako huko ni kujidanganya. Wapo ambao watakuona kituko.

Watakuona kicheche usiyejiheshimu kwa watu, hivyo sidhani kama utapendwa na kuthaminiwa. Huo ndio ukweli na tunapaswa kuwa makini katika hili.

Wakati ukijirahisi au kujilainisha kwa mwanaume, wenzako wanaweza kuchukua nafasi yako kwa kuwa na msimamo wao, kuwa na maadili mema kwenye jamii.

Lazima hilo tulijue kama tunahitaji kuwa na watu tunaowahitaji kuwa nao, ila si kwa kuona kujipitisha kwake, kujichanganya naye hata pasipohitaji ni njia ya kutamkiwa unapendwa na wanaume, maana huenda ukaonekana muhuni.

Hilo tuliseme hadharani ili kila mtu ajue makosa yake yanayoweza kumgharimu katika kipindi cha maisha yake, ukizingatia wapo mabinti ambao ni wasumbufu.

Kwa bahati mbaya, usumbufu huo hauna faida kwao hasa pale wanapojikuta wanamsumbukia mtu ambaye huenda hana muda wa kusikiliza kilio chake na kuambulia matusi.

Wanajikuta wakinyanyasika kwa namna moja ama nyingine, hasa kwa kutoonyeshwa mapenzi ya dhati, maana walifanya yale yasiyoruhusiwa.

Si wote ambao wanapenda wanawake waliojipitisha kwao na kuweza kuishi nao vizuri. Hata kama wakiwa pamoja, lakini kuna siku itatokea kashfa wanapoingia kwenye migogoro.

Mtu anaweza kuona msichana huyo ni mrahisi, akamtaka mwenyewe, hivyo hawezi kuweka akili yake kupoteza muda wa kumuwaza au kumlaki.

Kama mwanzo hajaonyesha udhaifu wakati wa kuanzana na mpenzi wake, matusi, kejeli hayawezi kuchukua nafasi, maana atakumbuka alivyopata tabu kwa ajili yako.

Sikatai hata mwanamke anaweza kufikisha ujumbe wa mapenzi kwa mwanaume, lakini si kama hivyo kwa kujipitisha pitisha ovyo, kutotumia nafasi nzuri kufikisha ujumbe wa mapenzi.

Wakati mwingine msimamo nao unahitajika na lazima uonyeshe kuwa wewe ni msichana makini. Nayasema haya kwa sababu moja tu, wengi wanaumia kwa kuwapenda wanaume.

Wanawapenda na kuwahitaji sana. Tatizo watafikisha vipi ujumbe wao kwa watu hao? Katika kuumia huko, wameamua wajitoe mhanga, ila si kwa njia nzuri.

Kuna mengi ya kufanya katika kufikisha ujumbe kwa mwanaume, hasa kwa wasichana wanaoumia kwa namna moja ama nyingine, ila tutayajadili kadiri tutakavyopata nafasi hiyo.

Nakutakia Jumamosi njema na tuendelee kuwa pamoja wiki ijayo katika ukurasa huu.

Tukutane wiki ijayo.


0712 053949
0753 806087

Mwisho
Ongeza umakini
SWALI: Habari za leo Aunt Jeni? Mimi ni mvulana mwenye umri wa miaka 25, tumekuwa tukikorofishana na mpenzi wangu mara nyingi, jambo la kushangaza kila tunapogombana huniambia hanipendi, tena husema kuwa ananitafutia sababu kubwa tuachane, kweli hapo kuna mapenzi ya kweli?
JIBU: Pole kwa yanayokukuta, kugombana ni mambo ya kawaida katika maisha ya mahusiano, lakini kama anaendelea kusema atakutafutia sababu ya kukuacha, inaonyesha wazi amedhamiria katika suala hilo, fungua macho na ongeza umakini wa hali ya juu na umchunguze, lazima utapata sababu inayosababisha yeye kusema hivyo.
SWALI: Habari yako Aunt? Matumaini yangu hujambo, kuna umuhimu gani wa kuwa na mpenzi ambaye hakupendi wala kukujali, ila anahitaji umtimizie kila kitu?
JIBU: Nashukuru mimi ni mzima, hapo hakuna mapenzi ya dhati, anachokihitaji kutoka kwako ni kukutumia na kuondoka, mapenzi ya kweli huonekana mapema. 
Imeandaliwa na Jennifer Ullembo
Maoni 0655 747403

No comments:

Post a Comment