Pages

Pages

Wednesday, June 26, 2013

Kiwanja cha wazi chaleta utata Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga



Na Mwandishi Wetu, Handeni
HALMASHAURI ya Wilaya ya Handeni imekumbwa na kashfa nzito kufuatia kugawa kiwanja cha wazi kilichopo maeneo ya mtaa wa Zizini kwa mfanyabiashara Said Khalfan  bila kuzingatia sheria na kanuni za ugawaji wa ardhi.
Eneo la wazi lililopo mtaa wa Zizini Handeni Tanga ambalo limejengwa nyumba ndogo ya biashara kama inavyoonekana kwa mbele lipo katikati ya hifadhi ya barabara na msongo mkubwa wa umeme. Picha na Mwandishi wetu.


Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa wilayani Handeni, umebaini kuwa kiwanja hicho kipo kwenye ndani ya hifadhi ya barabara pamoja na msongo mkubwa wa umeme. 

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Mtaa huo Musa Rajabu Kasidi au ‘Jaba’ alisema kiwanja hicho cha wazi kilikuwa ni kati ya viwanja sita ambavyo halmashauri ya wilaya hiyo ilibainisha kuwa ni viwanja vya wazi kwa kuwa tayari vilikuwa kwenye hifadhi ya barabara lakini alishangaa kuona mfanyabishara huyo akiendeleza ujenzi.

Alisema eneo hilo maalum lilitengwa kwa ajili ya kuendeleza mji huo na uongozi wa wilaya hiyo tangu mwaka 2000 lakini ilipofika mwaka 2003 ilibainika kuwa kuna watu wamegawiwa viwanja hivyo lakini walipobanwa walivirudisha lakini mfanyabishara huyo aligoma kurudisha hadi alipowekea alama ya x na Wakala wa barabara (Tanroad).

“Mhandisi wa wilaya wakati huo aliyefahamika kwa jina la Mbaga alipiga x kwamba abomoe jengo lake lakini cha kushangaza uongozi uliokuja wote wakaona panafaa kujengwa, ingawa tayari alikuwa amepewa notice ya kubomoa nilishangaa kuona anaendelea huku akifuta kabisa alama hiyo.

“Yule bwana ni mbishi kwa sababu hiyo sijui serikali wana mtazamo gani, kwa sababu inaonesha uongozi wa wilaya umejikanganya wenyewe ndio maana wanashindwa kumtoa.

“Kwa kuwa mimi ni mtu mdogo siwezi kuonekana kwamba nina uroho wa madaraka, mwisho wangu wa kufutilia ndio huo lakini nashindwa kuelewa serikali inatekeleza nini wakati hata Waziri Mgufuli jambo kama hili halitaki kabisa,” alisema.

Akizungumzia sakata hilo kiongozi mmoja wa Tanroad wilaya humo aliyejitambulisha kwa jina la Mkwiti alidai kuwa suala hilo ni kweli lipo lakini hataki kulizungumzia kwa sababu lipo kwenye halmashauri.

Kwa upande wake mfanyabiashara huyo, Said Khalfan alikiri kuwa eneo hilo ni lake ana alipewa kihalali na halmashauri hiyo tangu mwaka 2003.

“Lakini cha ajabu walikuja tena kunifungulia kesi zenye makosa manne na yote nilishinda miezi mitatu iliyopita na ikaamuliwa halmashauri inilipe fidia ya Sh milioni 56 kwa kunidhalilisha ila nikaamua kuwasamehe.

“Hili ni jambo lenye fitina ndani yake kwa sababu hati halali walinipatia wenyewe sasa wakadai nipo kwenye hifadhi lakini mwisho wa siku mahakama ya ardhi Korogwe iliidhinisha ni langu kihalali.

“Hili ni tatizo ambalo linaendeshwa kikabila na kidini wanatumia ubinafsi wakati eneo nimepewa kihalali kama wanataka waende mahakama ya mkoa, kwanza inashangaza kesi moja ya ardhi iwe na makosa manne,” alisema.

Wakati Mkurugenzi wa Wilaya ya Handeni Thomas Mzinga, alikiri kufahamu sakata hilo na kudai kuwa sasa linashughulikiwa na kamati ya ulinzi na usalama.

“Ni kweli hili suala lipo na tunalifahamu lakini pamoja na hatua zote zilizofikiwa sasa tumeiachia kamati ya ulinzi na usalama ilifanyie kazi kwanza,” alisema.

No comments:

Post a Comment