Pages

Pages

Thursday, June 13, 2013

Kituo cha Polisi Magomeni chadaiwa kumuachia kinyemela anayedaiwa kubaka binti wa miaka 12


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KITUO Cha Polisi Magomeni, jijini Dar es Salaam, kimeingia kwenye kashfa nzito, baada ya kudaiwa kumuachia anayedaiwa kuhusika na ubakaji wa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 12 jina tunalo bila sababu za kueleweka.
 Moja ya vyeti vilivyotoa majibu ya sakata hilo la ubakaji
Msamaria Mwema, Halima Athumani.
Msamaria mwema aliyekuwa anafuatilia suala hilo la ubakaji, aliyejitambulisha kwa jina la Halima Athuman, alidokeza juu ya suala hilo na kusema lilitokea Aprili 21, maeneo ya Magomeni Makuti, jijini Dar es Salaam.

Katika hali ya kushangaza, mmoja wa askari kutoka katika kituo hicho alitajwa kuwa alimpigia simu msamaria mwema huyo na kumwambia aachane na kesi hiyo kwakuwa inaweza kumletea matatizo.

Mwanamama huyo alisema kuwa mtoto aliyebakwa alikuwa anaishi na shangazi yake, Magomeni Makuti, lakini usiku wa kumkia Aprili 21, alipanda kwenye daladala kwa nia ya kwenda Kigamboni kwa mama yake mzazi Khadija Juma, baada ya kufanyiwa unyama huo.

“Nikiwa kama binadamu ambaye nipo sehemu ya jamii, niliamua kumsaidia mtoto yule, hata hivyo baada ya kumbana kwa maswali aliamua kuniambia ukweli juu ya kufanyiwa unyama huo na mume wa shangazi yake.

“Kwa bahati mbaya, baada ya taarifa kufika polisi na baadaye madai ya ubakaji huo kuthibitishwa na mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Mwananyamala,” alisema.

Siku ya Aprili 21, yalifanyika mazungumzo na Mkuu wa Kituo cha Polisi Magomeni, Mwanne Salum, hata hivyo kwa mujibu wa sheria za jeshi la Polisi, hakuwa msemaji mkuu wa sakata hilo, ingawa alikiri kulifuatilia kwa karibu kuangalia ukweli wake kwa ajili ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya dola.

Hata hivyo, Mkuu huyo alimtaka mwandishi wetu kuacha kuandika habari hizo, kwakuwa angehakikisha sheria zinafuata mkondo wake ikiwa ni kufungua jalada lenye kumbukumbu namba MAG/RB/5280/2013.

Tangu Aprili 21, tuhuma hizo hazikupewa kipaumbele, hadi mtuhumiwa kuachiwa kabla ya kufikishwa mahakamani, huku habari zake zikifanywa siri.

Taarifa hizi zilifika katika meza ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, kabla hajahamia Makao Makuu na kusema kuwa bado hakuwa na taarifa hizo.

“Ndio kwanza nasikia kutoka kwako, ila ningeomba huyo anayelalamika kwenye tuhuma hizo, aje ofisni kwangu nizungumze naye kwa ajili ya kujua kinachoendelea.

“Naomba umwambie huyo msamalia mwema aje ofisini kwangu siku ya Jumatatu ya Mei 27 ili nijuwe sakata lenyewe lilivyo na kutafuta suluhu kabla ya kuliandika kwenye vyombo vya habari, maana si kila jambo linalotokea nalijua, ukizingatia kuwa nina watu ambao nafanya nazo kazi,” alisema Kenyela.

Taarifa za kuachiwa kwa mtuhumiwa huyo kinyemela ni mwendelezo wa kashfa mbalimbali zinazoliandama jeshi la Polisi kila siku na kuzua hofu kwa wananchi wake, ambao wanategemea uwapo wa jeshi hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao.


No comments:

Post a Comment