Pages

Pages

Thursday, June 27, 2013

Coastal union kutua Arusha Julai 4 tayari kwa mashindano ya Rolling Stone


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU ya vijana ya Coastal Union inatarajia kuelekea jijini Arusha, Julai nne mwaka huu tayari kuanza kwa michuano ya Kombe la Rolling Stone, iliyopangwa kuanza kutimua vumbi Julai sita.
Kikosi cha vijana wa Coastal Union kikijifua uwanjani.
Coastal wanakwenda Arusha huku wakiwa na kumbukumbu ya kushika nafasi ya pili katika mashindano yaliyofanyika mwaka jana nchini Burundi na kuitangaza vyema Tanzania.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tanga, Meneja wa timu hiyo ya vijana, Abdulrahaman Ubinde, alisema kuwa wapo tayari kwa mapambano katika mashindano hayo.

Alisema watafika jijini Arusha siku mbili kabla ya kuanza kwa mashindano ya Rolling Stone, huku wakiwa na shauku ya kufanya vyema na kuonyesha cheche zao katika mpira wa miguu.

“Tumepanga kuelekea Arusha Julai nne kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo ambayo mwaka jana tulishika nafasi ya pili na kushangaza wadau wengi wa soka.

“Tupo imara na hakika vijana watafanya kazi nzuri katika mashindano hayo yanayoleta mwamko wa aina yake, ukizingatia kuwa Coastal Union imejiweka katika soka la ushindani,” alisema.

Katika patashika ya Ligi ya Tanzania Bara iliyomalizika mwezi uliopita, Coastal Union ambao imepandisha wachezaji sita wa vijana, ilimaliza ikiwa katika nafasi ya sita, huku ubingwa ukinyakuliwa na Yanga.

No comments:

Post a Comment