Pages

Pages

Saturday, May 25, 2013

Utundu, ubunifu, kujituma ni dawa zaidi ya limbwata



Wasanii wa Bongo Fleva, Dayna Nyange na Kala Jele 100 wakiwa kwenye picha ya malavidavi...

MAMBO FULANI MUHIMU
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HII sio Dunia ya kuendelea kupakwa masinzi kwa waganga wa kienyeji kwa sababu ya kuhangaika kumtuliza mume au mpenzi wako. Ni kweli kabisa, maana kama kukua kwa sayansi na teknolojia bado watu watajazana huko, tena kwa ajili ya mapenzi, hakika linashangaza.

Dunia ya leo dawa kubwa ni kujitambua. Ni kuelewa namna gani unapaswa kuishi na mwenzako katika hali ya kumfanya atamani kuendelea kuwa na wewe kwa moyo wake mwenyewe, bila kuchanganya ushirikina.

Ndio dawa za kienyeji zipo na zilikuwapo tangu enzi na enzi, lakini sio kichocheo cha mtu kupendwa au kuganda sehemu ambayo si sahihi. Kwa kulijua hilo, tunaweza kuutumia msemo huu.  ‘Hata chura anapenda maji lakini si ya moto’. Ni kweli, hivyo kama wewe hujui namna gani ya kuishi na huyo umpendae, hata kama mwili wote uchanjwe chale bado si ishara ya kufurahia uhusiano na mtu wako zaidi ya kujiumiza tu.

Inashangaza sana, maana licha ya mtoto wa kike kubarikiwa uzuri na urembo wa aina yake bila kusahau mwili wenye mnyumbuliko kiasi cha kumvutia kila mtu, lakini silaha yako kubwa kwa mpenzi wako ni kwenda kwa mtaalamu, yani dawa za kienyeji.

Hapa ni kujipotezea muda. Hakuna tiba hapo. Zaidi unajipumbaza mwenyewe, kujipotezea muda, maana silaha kubwa ni kufahamu mbinu nzuri zinazoweza kumfanya mume au mchumba wako atulie.

Unaweza kulambishwa hata mkia wa chatu au vitu vingine kulingana na mahitaji ya waganga hao, lakini bado ukashindwa kupendwa na kuhitajiwa na mtu unayeona ana nafasi moyoni mwako.

Nimekuwa nikiulizwa maswali ya aina hii mara kwa mara. Jibu langu ni kuwataka watu wenye mtazamo huo wabadilike kabla mambo hayajaharibika. Najua kuwa kila jamii ina utaratibu wake.

Siingilii imani hizo kama ni sehemu ya maisha yao, ila bado tunapaswa kufahamu kuwa limbwata nzuri, ambayo inaweza isiishe muda wake milele ni kujitambua na kuamua kupigania penzi lako.

Si kupigania kwa kuona dawa ni kukesha au kulala kwa waganga wa kienyeji, bali kutumia nafasi yako pale unapokuwa eneo la faragha na mtu unayejua ni sehemu ya maisha yako.

Badala ya kukimbilia kwa waganga kutafuta limbwata ya kumpumbaza mtu, ni bora ukahangaika kung’amua mtindo, njia zinazomfurahisha zaidi mume au mke wako, maana ndio silaha ya aina yake.

Ndio maana limbwata ni wewe mwenyewe. Tumia nafasi yako, maana kuhangaika kwa njia hiyo ni kujipotezea muda. Kwanza mapenzi ya dawa siku hizi yamepitwa na wakati.

Kila mtu anatumia uwezo wake mwenyewe. Tumia nafasi yako, maana bila kujitambua, bado huwezi kumfanya huyo ulimuwekea limbwata aone wewe ni zaidi kuliko wengine.

Muda wa kuhangaika na limbwata kwa wana ndoa wangeutumia kuwaza mbinu za kuwakwamua kimaisha, ukizingatia kuwa pendo lao limeimarika bila kutumia njia za panya, hasa mbinu za kwa waganga.

Waganga ambao si wote ni waaminifu. Wengine wanapofuatwa kwa shughuli hizo za kimapenzi, hutoa masharti magumu yakiwapo ya kulala pamoja, mbinu ambazo huleta kudhalilisha watu kwa tamaa zao za kimwili.

Na wanafanya hivyo kwasababu nao ni watu na wana matamanio yao kama walivyokuwa wengine. Tena kwa hao wanaojipeleka wenyewe, wanaona kuwaacha ni kujicheka ujinga.

Kwanini? Hayo yamesababishwa na ujinga wetu wana jamii, kuona kuwa kila kitu lazima twende kwa waganga. Hakuna kitu kama hicho. Hebu leo simama wewe kama wewe  na sio kutegemea waganga.

Hao waganga tuwaone kwa mambo mengine, lakini si kumtuliza mke au mume, maana wewe mwenyewe ukivuja jasho, kujituma saa 24, kufanya vitu vinavyomfurahisha, hawezi kukuacha ng’o.
Tubadilike wana jamii.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment