Pages

Pages

Saturday, May 25, 2013

Fadhili Athuman, Soldier, kipaji kipya kinachopakua filamu ya More Fire


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SANAA ni moja ya vitu vinavyohitaji uvumilivu na kujitoa kwa nguvu bila kuchoka, hasa kama lengo ni kuhakikisha kuwa mafanikio yanapatikana kwa namna moja ama nyingine.
                            Fadhili Athuman Soldier, pichani
Wasanii ambao hawana uvumilivu, hushindwa kuhimili changamoto zinazojitokeza katika tasnia ya sanaa Tanzania, ukizingatia kuwa mtu anayejiingiza kwa mara ya kwanza huhitaji muda hadi kuweza kutangaza na kuonyesha kipaji chake kwa hadhira.

                     Soldier, mkali wa filamu Tanzania
Kwa wale waliofanikiwa kuwa na uvumilivu, ndio hao wanaoishi maisha mazuri leo majina yao yakitajwa au kuandikwa kila mahali jambo linaalowapatia heshima kubwa kwenye jamii.

Miongoni mwa wasanii ambao licha ya kukabiriwa na changamoto za aina yake, lakini bado wanavumilia na kuzidisha uchu wa mafanikio katika tasnia ya soko la filamu hapa nchini, ni Fadhili Athuman, maarufu kama Soldier.

Kijana huyu kwa yupo kwenye hatua za mwisho kuingiza sokoni filamu yake ya More Fire, aliyoiandaa kwa umakini mkubwa akiwa na lengo la kuonyesha cheche zake katika ulingo huo nchini.

Kabla ya kufanikiwa kukamilisha filamu hiyo, Soldier alishiriki katika tamthilia mbalimbali, ikiwamo ile ya Cinderela, iliyokuwa inarushwa na kituo cha televisheni cha Star Tv ya jijini Mwanza.

Katika mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni, Soldier anasema kuwa katika tamthilia hiyo na nyingine alizowahi kucheza, msanii huyo ameweza kuonyesha umakini wa aina yake katika kuigiza, hivyo baadhi ya watu kumtabiria mafanikio siku za usoni.

“Sanaa ya Tanzania inahitaji uvumilivu na hakika naendelea kupigania mafanikio kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa nimechagua sanaa kuwa sehemu ya maisha yangu.

“Hakuna kitu ninachowaza zaidi ya sanaa, hivyo naamini mambo yataendeleaa kuwa mazuri, hasa kwa kuandaa filamu zenye kiwango cha juu na kuwaonyesha watu namna gani kazi inatakiwa ifanywe,” alisema.

Katika filamu yake hiyo ya kwanza kuandaa, amewashirikisha wasanii mbalimbali, akiwamo mnenguaji wa FM Academia, Queen Suzy, Kaila, Bi Fetty, Zuma, Sacy, Ngamakisi, Ize, Shelii, Todi.

Anasema kuwa filamu hiyo ya aina yake, ameandaa chini ya Kampuni yake Tanzania One Production yenye maskani yake jijini Dar es Salaam na iliyopania kufanya vyema katika sanaa nchini.

Msanii huyo anaendelea kusema kuwa kabla ya kuamua kutengeneza filamu hiyo, alianza zamani kujiingiza kwenye sanaa na kufanikiwa kucheza tamthilia na filamu za watu wengine.

Anaitaja filamu ya Wema iliyoandaliwa na msanii wa vichekesho nchini, Senga, huku akishiriki na wasanii wengine nyota na kuiweka juu filamu hiyo miaka kadhaa iliyopita.

Tamthilia alizowahi kucheza Soldier ni pamoja na Cinderela mwaka 2011, Ua Jekundu iliyokuwa ikirushwa mwaka 2004, Doa mwaka 2005 katika televisheni ya Chanel Ten, Zeze TBC 1 mwaka 2007.

Makundi aliyowahi kupitia msanii huyo na kujifunza sanaa ni pamoja na Fukuto Arts Group mwaka 2002 ambao lilifanikiwa kutengeneza tamthilia yao ya Ua Jekundu, wakati mwaka 2004 alijiunga na kundi la Dar Talent, huku miaka miwili baadaye akijiunga na kundi la Sea Breeze.

Hata hivyo, msanii huyo hajaweza kudumu na makundi hayo kutokana na mpangaranyiko wa kiutawala kwa baadhi ya viongozi wao, hivyo kuamua kukimbilia Watoto wa Tembo na baadaye Bongo Hood.

“Huko kote nilikuwa napigania maisha yangu kwa kupitia sanaa ya maigizo na filamu hapa nchini, jambo ambalo lilifanikiwa kuniweka katika mazingira mazuri na kuuweza ushindani uliopo.

“Ingawa bado sina jina kubwa, lakini wote wanaonijua mimi wanajua uwezo wangu, huku nikipania malengo ya juu zaidi kuhakikisha kuwa naweza kupambana kwa namna moja ama nyingine,” alisema.

Soldier anaelezea ushindani uliopo kuwa unachangia kukuza soko la sanaa kwa ujumla, hivyo ni jukumu lake kuhakikisha kuwa anaweza kutangaza kipaji chake kwa wadau wa sanaa nchini.

Msanii huyo anasema kuwa japo sanaa ni moja ya sekta zinazowalipa wasanii, lakini baadhi yao wameshindwa kutumia ubunifu kwenye kazi zao, jambo linaloweza kuharibu soko lao.

Anasema baadhi ya watu wamekuwa wakitunga filamu zisizojitosheleza kwa hadithi nzima, mpangilio wa matukio, uongozi na hata wachezaji kutovaa uhalisia wa mambo kwenye filamu kwa ujumla.

Jambo hili lilifanyika, baadhi ya wadau ambao ndio wanaoiweka sanaa juu 
hujikuta wakiishiwa na mapenzi ya kuwaunga mkono wasanii wa Tanzania na kuendelea kuangalia kazi  za nje za Nigeria, India na Marekani ambako kazi zao zinaangaliwa na kila mtu.

“Kwa kulijua hilo, kwenye filamu yangu hii ya More Fire na nyingine nitakazobarikiwa kuandaa nitahakikisha kuwa wadau wangu wanaendelea kuniunga mkono kwa kuwapa kazi nzuri.

“Nimepigania sana kulionyesha hilo, hivyo naamini mashabiki wa sanaa Tanzania ni wakati wao kusubiria na kuitazama filamu hiyo yenye ujazo wa kila aina kuanzia mtiririko wa matukio na wasanii waliyocheza,” alisema Soldier.

Msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1985 kijiji cha Mzenga, wilayani Kisarawe mkoani Pwani, anasema kwa sasa hana cha kupoteza zaidi ya kuongeza ubunifu kwenye kazi zake kwa ajili ya kuonyesha makali yake.

Soldier anawataka Watanzania, mashabiki na serikali kushirikiana kwa pamoja ili kukuza soko la sanaa Tanzania ili iwe njia ya kuwapatia maisha bora vijana wanaojiingiza kwenye tasnia hiyo.

Bila hivyo, sanaa itaendelea kusua sua na kuwa mradi wa watu wachache wasiokuwa na huruma na watu wanaotumia gharama zao kubwa na muda kuandaa filamu na anayekuja kunufaika ni mtu mwingine ambaye hajui tabu alizokutana nazo muandaaji.

Soldier ni miongoni mwa vijana ambao wamekuwa na mapenzi makubwa na sanaa Tanzania, huku nikiamini kuwa huenda akatimiza ndoto zake kama ataendelea kukaza msuri na kujituma bila kuchoka.

No comments:

Post a Comment