Pages

Pages

Monday, May 27, 2013

Ngassa na hadithi ya wamoja havai mbili?



SIWEZI KUVUMILIA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WASWAHILI wana msemo wao maarufu unaosema kuwa siku zote wa moja havai mbili. Msemo huu kama ni uongo, basi upo karibu na ukweli. Binafsi nauamini msemo huo nikiorodhesha na matukio yetu kwenye jamii.
Mrisho Ngassa, akiwa kwenye jezi ya timu ya Taifa, Taifa Stars
Matukio ambayo yanaendelea kutokea na kutuacha tunajiuliza maswali kede kede, ukizingatia kuwa kila mtu ana maoni na mtazamo wake. Mapema wiki iliyopita, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Mrisho Ngassa alitambulishwa kwenye uongozi wa Yanga, kuwa amesajiliwa kwa ajili ya kukipiga kwenye timu hiyo msimu ujao wa ligi.

Ngassa ni kama amerejea tu Yanga, maana aliwahi kukipiga kwenye timu hiyo kabla ya kutimkia katika timu ya Azam FC na baadaye kusajili Simba, alipoitumia kama njia ya kumrejesha Jangwani.

Si vibaya kwa Ngassa kurudi Yanga, maana katika mazungumzo yake na wanahabari alisikika akisema kuwa ana mapenzi na klabu hiyo. Ni mnazi mkubwa wa Yanga.

Anaipenda kuliko kitu chochote duniani. Sawa, ila Dunia ya leo mipra ni kazi na sio unazi tena. Kama unazi, basi mchezaji wa aina hiyo hawezi kusonga mbele katika soka la Kimataifa.

Ndio, hivyo siwezi kuvumilia, ndio maana Ngassa ameonekana kucheza soka kwa ajili ya Tanzania tu. Kamwe hana maono ya kufika mbali. Hana lengo lolote la kuwa nyota Kimataifa.

Mchezaji huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kwa wadau wa soka Tanzania, alikataa dau nono la timu ya El Merreikh ya Sudan. Kama angekubali kwenda huko, huenda ingekuwa njia yake ya kusonga mbele.

Lakini bila sababu za kueleweka, aliamua kuikataa ofa hiyo. Watu walijuliza maswali lukuki. Maswali ambayo sasa yamepata majibu kuwa hana anachoangalia zaidi ya soka la Simba, Yanga na Azam FC.

Hii ni aibu kubwa. Aibu ambayo itaendelea kumsumbua Ngassa miaka nenda rudi, maana hata mapato ya Tanzania na Sudan ni tofauti. Kwa kawaida, anaposajiliwa kwenye timu moja, ni njia ya kwenda kwingine.

Kama Ngassa angeenda Sudan, huenda angepata nafasi ya kuonekana nchi nyingine na kuonyesha uwezo wake. Labda amejijua kuwa hana tena muda mrefu uwanjani.

Kwamba uwezo wake unaelekea ukingoni? Hapana, mbona hadi leo Athumani Idd Machuppa yupo nje anacheza soka? Ni mipango tu. Umri wa Ngassa hauna tofauti kubwa na kiungo wa Tanzania, Henry Joseph Shindika anayecheza soka la kulipwa nchini Norway.

Huyu Ngassa ana mshauri kweli? Nani ameshika funguo ya mafanikio ya kijana huyu ambaye Taifa bado linamuhitaji? Hatukatai kucheza soka la ndani, lakini kwa Ngassa ameshavuka.

Ilitakiwa aende kwanza nje kucheza soka, kabla ya kurudi nyumbani kumalizia soka lake kama inavyojulikana. Je, kurudi kwake Yanga, ndio kusema amefanikiwa?

Ina maana amenufaika na maisha yake ya kusajiliwa kwa gari? Wenzake Ulaya wanaishi kwa fedha nyingi mno. Gari ambalo mara nyingi linaonyeshwa kama danganya toto, ila soka la kulipwa lina manufaa makubwa mno.

Kwanza hata usajili wake si wa kiubabaishaji. Uliona wapi Dunia ya leo mchezaji anawekewa mezani milioni 20 na akishapewa kuishia kwa madalali, waliompigia chapuo kusajiliwa kwenye timu hiyo?

Hatuwezi kukubali wachezaji wetu wa Tanzania washindwe kutumia fursa kuwafilisi mabosi wa soka duniani. Hakika siwezi kuvumilia. Mtu kusajiliwa Azam na kuonyesha mapenzi kiasi cha kiubusu jezi kama sababu ya kuachwa ni ujinga wa kutupwa.

Bila hata kumsifu mchezaji huyo, anapaswa kuambiwa kuwa amefanya makosa makubwa, kiasi cha kulazimisha kurudi kule ulipotoka. Soka la Tanzania ni wazi lipo kwa Simba, Yanga na sasa kwa Azam.

Hivyo kama timu zote hizi umevaa jezi zao, kwanini usikwee pipa kutafauta maisha mengine ya soka? Kila la kheri Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Ivo Mapunda, Shindika, Danny Mrwanda na wengineo mnaohaha kutafuta maisha katika soka, maana Bongo ni porojo tu.
Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment