Pages

Pages

Sunday, May 12, 2013

Lundenga atembelea mazoezi ya Miss Kibaha 2013


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMATI ya Miss Tanzania, ikiongozwa na Mkurugenzi wake Hashim Lundenga, juzi jioni ilitembelea mazoezi ya washiriki wa Miss Kibaha 2013, yanayofanyika katika Ukumbi wa Vijana Social Hall Kinondoni.
                                      Hashim Lundenga
Katika msafara huo, Kamati hiyo ilifanya majadiliano na washiriki hao wa Miss Kibaha pamoja na kuonyeshwa sehemu ya shoo itakayotolewa katika fainali hizo zitakazofanyika Mei 17 mwaka huu katika Ukumbi wa Kibaha Kontena.

Akizungumza katika msafara huo, Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ndio waandaaji wa Miss Tanzania, Lundenga, alisema kuwa Miss Kibaha ni kati ya mashindano yenye mvuto mkubwa kwa mwaka huu kutokana na umakini wa waandaaji wake.

Alisema watu wengi wamekuwa wakiliangalia shindano hilo, hivyo kutoa picha kuwa huenda siku chache zijazo Pwani ikawa na ushindani mkubwa hasa kwa warembo wa Kibaha.

“Sisi tunaendelea kujiuliza kwanini Miss Kibaha ina mvuto mkubwa kiasi cha kila mmoja kuona kila kinachoendelea kwenu, hivyo ni vyema washiriki mkaliona hilo na kulifanyia kazi zaidi.

“Tunajua haya ni maisha yenu ya urembo, ndio maana tumeamua kuwatembelea kuangalia nini mnakifanya pamoja na kuwakumbusha taratibu na kanuni za Miss Tanzania,” alisema Lundenga.

Aidha, muandaaji wa Miss Kibaha 2013 ambaye pia ni Mkurugenzi wa Linda Media Solution, Khadija Kalili aliishukuru Kamati ya Miss Tanzania kutembelea kwenye kambi yao.

“Nashukuru sana kwa ujio wenu, maana mmenifanya nijisikie faraja kubwa na kuona kuwa ni wakati wa kuongeza bidii kuwaandaa washiriki ambao wao ndio waliotukusanya pamoja,” alisema.

Katika fainali hizo zilizopangwa kufanyika Mei 17 mwaka huu, burudani zitaongozwa na bendi ya Mashujaa ikiwa chini ya Charles Gabriel Baba, maarufu kama Chalz Baba.

No comments:

Post a Comment