Pages

Pages

Wednesday, May 15, 2013

Asha Baraka: Napenda kupambana na wanaume


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa bendi ya African Stars Twanga Pepeta, Asha Baraka, amesema katika maisha yake anapenda kupambana na wanaume kulilia mafanikio, hasa katika tasnia ya muziki wa dansi nchini.
                 Asha Baraka, Mkurugenzi wa Twanga Pepeta
Akizungumza mwishoni mwa wiki na Handeni Kwetu Blog, Asha alisema bendi ya Twanga Pepeta imepitia katika misuko suko mingi, huku akilazimika kupambana vilivyo kwa kukwaruzana na wanaume waliokuwa na lengo la kuiangusha.

Alisema hali hiyo imempa ukomavu wa aina yake kiasi cha kuona kwamba yeye ni imara na hawezi kuogopa kusikia kuna mwanamuziki anataka kuondoka kwakuwa ndio kawaida ya muzki.

Asha alisema kuwa endapo asingekuwa mkomavu kwenye muziki, huenda angeachana na muziki au kukubali Twanga Pepeta ife, maana wapo watu hasa wanaume waliokuwa wanapigania kwa faida walizojua wenyewe katika soko la muziki wa dansi.

“Napenda kupambana na wanaume na sio wanawake, hivyo katika hilo nimefanikiwa ndio maana hadi leo Twanga Pepeta ipo imara licha ya watu wengi, hasa wanaume kufanya bidii kuiangusha.

“Nilikuwa juu katika kipindi chote cha uwapo wa bendi ya FM Academia, Akudo Impact, Stono Music na nyinginezo ambazo zote niliweza kupambana nazo,” alisema.

Twanga Pepeta ipo chini ya Luiza Mbutu akishirikiana na wanamuziki wengine kama vile Dogo Rama, Salehe Kupaza Mwana Tanga, Kalala Junior, Badi Shaban Bakule, Janet Isinika na wengineo wanaoiweka juu bendi hiyo.

No comments:

Post a Comment