Pages

Pages

Monday, March 25, 2013

Yanga wanawaza maendeleo, Simba wanapiga soga



SIWEZI KUVUMILIA

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WACHAMBUZI wa soka waliowengi wanasema hakuna maendeleo ya mpira wa miguu bila kuzitaja klabu za Simba na Yanga. Sawa, kutokana na ukongwe wao, hilo haliepukiki.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

Wao Simba na Yanga lazima watajwe, ingawa mara kadhaa wamekuwa wakitajwa kwa mabaya na sio mazuri. Kwasababu hiyo, huwezi kutaja mafanikio ya soka kwa miaka ya hivi karibuni, eti ukaitaja Simba na Yanga na kuiacha Azam FC.


Kwanini? Umetumia vigezo gani? Hata hivyo, katika kuwaza yote hayo, najikuta nikiangalia nyendo za viongozi wa klabu hizi za Simba na Yanga, na kuona kuna dalili kubwa za mmoja wao kusonga mbele na kumuacha mwenzake akibaki kama alivyo.

Kwanini nasema hivyo? Ukiangalia nyendo za viongozi wa Simba, utagundua kuwa wamekuwa wakipiga porojo na kukosa mbinu nzuri za kuendeleza klabu yao.

Simba ikiwa chini ya Ismail Aden Rage, imekuwa ikiandamwa na malalamiko ya wanachama wao, kiasi cha kutangaza mkutano wao na kufikia kusimamisha uongozi huo.

Uamuzi huo ni baada ya Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange Kaburu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope kujiuzulu nafasi zao.

Hata hivyo, mkutano wa wanachama uliofanyika katika Hoteli ya Star Light Kariakoo, ulitangaza kuwaingiza katika uongozi huo Pope na Rahma Al Khgarous, jambo ambalo uongozi wa Simba umepinga na kudai kuwa mkutano wao ulikuwa ni kama kikao cha harusi.

Sawa, huenda ni kweli wanachama hao wamefanya kikao cha harusi, lakini huu ni mwendo mzuri kwa ajili ya Simba? Binafsi naona kama vile Simba imezidi sana porojo kuliko vitendo.

Ukiangalia wenzao Yanga, wamekuwa na mipango mingi yenye tija katika siku za usoni. Juhudi zao zinaonekana, lakini sio hawa wanaojiita Wekundu wa Msimbazi.

Kuna hatari kuwa miaka mitatu ijayo, Yanga wao watakuwa wamefanya mambo makubwa, wakati wenzao Simba wanaendelea kutukana na kuitana vikao vya harusi kama anavyodai mwenyekiti wao.

Hakika siwezi kuvumilia. Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, alitangaza kumuingiza katika Kamati ya Maendeleo ya Mafia, mtoto wa rais, Ridhiwani Kikwete kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Yanga inakuwa na jingo kubwa la kibiashara.

Hakika uwezekano huo upo. Wakijipanga na kuweka mtaji huo wenye dhamira ya aina yake, mambo mengi mazuri yatapatikana kwa namna moja ya kuiweka Yanga sehemu nzuri.

Haya lazima yasemwe na kupingwa kila yanapoonekana kuwa baadhi yao hawataki na wanaendelea kufanya mambo ya kushangaza. Simba hii inataka kuwa mtani wa jadi kwa mechi tu au hata mipango ya kimaendeleo kwa klabu yao?

Simba hii ambayo haina uhakika wa kutetea taji lao, hivi kweli ina walau mpango wa kumiliki uwanja wao wa michezo? Ukisema hivi wenye Simba yao watakwambia ndio. Kisa, Rage aliahidi. Rage aliahidi siku 90 za mafanikio ya Simba, je, bado hazijafika?

Rage huyu amekuwa hana jipya katika uongozi wake, hivyo kuna hatari kuwa kama mambo yakiendelea hivi, basi Simba itakuwa mtazamaji mkubwa wa masuala ya maendeleo ya Yanga.

Hii itakuwa aibu ya karne. Na ndio maana nimeshindwa kuvumilia, nikiamini kuwa viongozi wa Simba sasa watashtuka na kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya klabu yao.

Huu ndio ukweli. Vingine, nitaendelea kuwa karibu na wanachama maana ndio wenye klabu yao, maana uongozi wao hauna mpango mzuri zaidi ya kutaka kuipoteza klabu yao.

Namaliza kwa kuwapongeza Yanga na kuwatakia mipango mema kwa ajili ya maendeleo ya soka na klabu yenu kwa ujumla.
Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment