Pages

Pages

Tuesday, March 05, 2013

Kaseba afurahia ushindi wake dhidi ya Oswald




Japhet Kaseba pichani

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BONDIA wa ngumi za kulipwa hapa nchini. Japhet Kaseba, amesema mazoezi makali kwa ajili ya kumchakaza mpinzani wake, Maneno Oswald, yamempa ushindi huo, jambo linalompa imani kuwa amekuwa juu zaidi kimasumbwi.

Pambano hilo lilifanyika Jumamosi ya wiki iliyopita na Kaseba kushinda kwa pointi, pambano lililofanyika katika Ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa na kuhudhuriwa na watu wengi waliokwenda kushuhudia mbabe wa patashika hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaseba alisema kwamba anaamini kuwa mazoezi makali kwa ajili ya pambano hilo, yamempa ushindi, hivyo wanaotarajia mteremko kutoka kwa mabondia nafasi hiyo kwake itakuwa ngumu.

Alisema ingawa Oswald alionyesha kiwango cha juu katika mwanzo wa mchezo huo, lakini umakini wake ulingoni, ulimpa imani kuwa lazima atomize ndoto zake za kumtwanga bondia huyo mwenye uzoefu mkubwa katika masumbwi.

“Nashukuru kwakuwa nimefanikiwa kuibuka na ushindi kutoka kwa Oswald, ukizingatia kuwa pambano letu lilikuwa na ushindani wa aina yake, kutokana na malengo ya kila mmoja wetu kutaka kushinda mbele ya mwenzake.

“Mimi nilijiandaa vizuri zaidi kwa ajili ya kupata ushindi mbele ya mpinzani wangu, ukizingatia kwamba hata uwezo wangu ni mkubwa ndio maana baadhi ya mabondia wa Tanzania wamekuwa wakiniogopa mara kwa mara,” alisema.

Kaseba alishinda katika pambano lake mbele ya Oswald, baada ya majaji watatu, akiwamo Anthon Ruta, kutoa pointi 100 kwa 90, Aga Peter, aliyetoa pointi 99 kwa 91 na Pembe Ndawa alimpa Kaseba pointi 97 kwa 93, hivyo kumpa Ubingwa huo bondia huyo aliyewahi kuwika pia katika Ngumi za mateke Kick Boxing.

No comments:

Post a Comment