Pages

Pages

Tuesday, March 05, 2013

Victoria Sound sasa ni kazi kwenda mbele



Mwinjuma Muumini, kushoto, katika uzinduzi wa bendi yake ya Victoria

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
RAIS wa bendi ya Victoria Sound, Mwinjuma Muumini, amesema kwamba baada ya kuizindua bendi yao kwa mafanikio makubwa, mipango yao kwa sasa ni kuendeleza na ratiba ya shoo zao sambamba na kuandaa nyimbo kwa ajili ya albamu yao ya kwanza.

Victoria Sound ilizinduliwa rasmi Ijumaa iliyopita na kuhudhuriwa na watu wengi, wakiwamo wale wadau maarufu katika tasnia ya muziki wa dansi, ambao baadhi yao wameweka kambi katika bendi nyingine hapa nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Muumini maarufu kama Kocha wa Dunia alisema kwamba watu wengi walihudhuria kwenye uzinduzi wa bendi yao, hivyo kwa sasa kitu anachokifanya ni kuonyesha kwanini wameanzisha bendi hiyo.

Alisema wanamuziki wake wote wamejipanga kuhakikisha kuwa wanakwea kileleni, hivyo juhudi kubwa wanayoifanya ni kutunga nyimbo nzuri, kubuni namna ya kuwapa burudani mashabiki wao kwa ajili ya kujiletea mafanikio yao.

“Huu ni wakati wa kuonyesha kwanini tulikaa na kuanzisha bendi hii kwa ajili ya kuwapatia burudani kamili mashabiki wetu, hivyo naomba waendelee kutuunga mkono ili tufanikiwe zaidi katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini.

“Naamini kila kitu kitafanikiwa katika hali ya kuleta mapinduzi, maana tumejipanga imara, sambamba na kufanikiwa kuizindua kwa shangwe tukipata mashabiki wengi waliokuja kujionea burudani za aina yake kutoka kwa Victoria Sound,” alisema Muumini.

Muumini ni miongoni mwa wanamuziki wanaopendwa na wengi katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini, akiunda bendi ya Victoria Sound, akiwa sambamba na wakali wengine, akiwamo Waziri Sonyo, aliyerudi upya kwenye sanaa.

No comments:

Post a Comment