Pages

Pages

Sunday, March 17, 2013

Full Tank: Kibonge mtukutu anayetikisa fani ya uchekeshaji



 Full Tank, mkali wa comedy Bongo
 Full Tank: Soma makala yake hapo chini


 Full Tank
EDWARD PETER CHAGULA ‘FULL TANK’

  Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA vitu ambavyo binafsi huwa napenda kuviangalia, vikiwamo hivi vya kuangalia komedy kutoka kwa wasanii mbalimbali wa Tanzania. Hata kama nikiwa na mawazo vipi, hakika kazi hizo zinanifanya nijione mwenye furaha na amani tele.

Katika kuangalia filamu hizo, ni wasanii wengi wanaovutia akiwapo Edward Peter Chagula, maarufu kama Full Tank. Ni kibonge kweli. Ni mkali pia katika sanaa, huku akimudu kuutumia mwili wake kwa uwezo wa juu kupita kiasi.

Kwa wasiofahamu uwezo wa kijana huyu, waangalie komedy nyingi, ikiwamo ile ya Kibonge Mtukutu, Miss Tandale, Choo cha Kulipia na nyinginezo . Katika mazungumzo yaliyofanyika mapema wiki hii, Full Tank, anasema kwamba sanaa ni kipaji chake.

Anasema tangu zamani alipenda kuigiza, hasa upande wa vichekesho, ndio maana aliweza kupigania maendeleo kwa kupitia ndani ya jukwaa hilo kwa ajili ya kuonyesha makali yake katika tasnia ya filamu hapa nchini.

"Nilikuwa napenda kuigiza tangu zamani, hivyo nadhani katika njia ya kutafuta jinsi ya kutoka, nimefikia hatua hii nzuri, huku nikiamini kuwa nitaendelea kuwa juu na imara kwenye maisha ya sanaa.

"Nafanya juhudi kubwa katika kuonyesha sanaa yangu ikiwamo ya uchekeshaji, hivyo wadau wangu na wanaopenda kazi zangu naomba waendelee kuniunga mkono katika maisha sana yangu,” alisema Full Tank.

Mkali huyo mwenye uwezo wa juu katika sanaa ya maigizo na uchekeshaji anasema kuwa sanaa ni ngumu na yenye ushindani wa aina yake, lakini anaamini kuwa changamoto hizo wasanii wanazitumia vyema kwa maisha yao.

Full Tank anasema kutokana na kufanikiwa kujitangaza katika kipaji chake, wadau wengi, zikiwamo taasisi zimekuwa zikifanya naye katika kazi katika sherehe mbalimbali za kiofisi ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam, ikiwamo mkoani Kilimanjaro.

Huko, msanii huyo kazi yake kubwa ni kuwachekesha kwa kuelimisha jamii katika matukio ya wafanyakazi alipoalikwa, jambo ambalo limezidi kumuweka katika nafasi nzuri katika tasnia ya filamu na uchekeshaji Tanzania.

“Huwa najisikia faraja kuona kuwa ndani ya saa moja au mawili naona kazi yangu kwenye luninga, yakiwamo matangazo ya kampuni mbalimbali yanayorushwa kwa kasi muda wote.

“Hilo linanipa imani na hamu ya kuendelea kupiga hatua katika kutafuta maisha yangu kwa kupitia sanaa, maana nimechagua kuwa msanii, ingawa naelewa sanaa ni ngumu na idadi kubwa ya watu wanaingia kwa nia ya kujikomboa,” alisema.

Full Tank anasema kwamba wasanii wote ni wazuri, ingawa kwa kipaji cha Mzee Majuto, hakika ni sehemu ya kuwapatia mwangaza wakali wengine, huku mzee huyo akiwa na ushirikiano na wasanii wengi, wakiwamo wale wanaochipukia.

Full Tank aliyetokea kupendwa na kuhitajika na watu wengi kutokana na umahiri wake wa kutumia mwili mkubwa, anasema kuwa yeye ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya mzee Peter Chagula, huku akiwa na watoto wawili, ambao ni Mathias mwenye miaka tisa na Veronica, akiwa na miaka sita.

Aidha msanii huyo anajiwa na kumbukumbu mbaya ya kuona wazazi wake wameshindwa kuona vipaji vyake baada ya kutangulia mbele ya haki miaka kadhaa iliyopita.

Full Tank anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa mambo yake yanakuwa mazuri zaidi, amepania kufanya kazi yenye maana kwa kutunga filamu zake au kushirikishwa na wandaaji wengine wanaothamini vipaji vyake.

Kijana huyo mwenye mwili mkubwa anasema kuwa sanaa ni kipaji chake alichozaliwa nacho, ingawa rasmi alianza mwaka 1995. Kundi lake la kwanza kujiunga nalo lilikuwa la Mahokazi likiwa chini ya Bambo na kushiriki kwenye filamu kadhaa.

Mbali na filamu hizo nyingi zikiwa za uchekeshaji, pia Full Tank ameshiriki katika tamthilia ya Ndio Mzee iliyokuwa ikirushwa na televisheni ya DTV mwaka 2002 ambapo nyota yake ilizidi kuonekana na kujitabiria mafanikio makubwa.

Full Tank aliyezaliwa mwaka 1986 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, amecheza filamu kadhaa, ikiwamo ya Grammar, Pete ya Ajabu, Sangoma, Sabra, Mpango uliokwenda Vibaya, Born Stone, Akili ni Nywele na nyingine zipo njiani kutoka.

Mbali na kucheza filamu hizo, pia kijana huyo amefanikiwa kutengeneza filamu zake za mtindo wa uchekeshaji ‘komedy’, ambazo ni Kibonge Mtukutu, Miss Tandale, Choo cha Kulipia na nyinginezo zilizotangaza zaidi makali yake.

Mkali huyo anasema kuwa sanaa ni ngumu na inahitaji ujasiri wa aina yake, hivyo wasanii wachanga wanatakiwa kuongeza bidii katika kutangaza uwezo wao.

Anasema hakuna haja ya kurudi nyuma au kuogopeshwa na ugumu uliopo, ukiwamo ule wa kusota katika makundi kwa miaka kadhaa kabla ya kufanikiwa kutoka, wakati wote huo, wengineo wakiendelea kuishi maisha ya raha.

Kibonge huyo mtukutu anasema katika kuliweka juu zaidi jina lake, lengo kubwa ni kufanya kazi zenye ujazo wa juu, ikiwa ni njia ya kumletea mafanikio, ingawa atakuwa mwepesi wa kuiga nyendo zenye tija kutoka kwa wasanii anaowakubali.

No comments:

Post a Comment