Pages

Pages

Monday, February 04, 2013

Zama za uchawi kwenye soka zimepitwa na wakati



SIWEZI KUVUMILIA

Jerry Teegete, mshambuliaji wa Yanga.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INASIKITISHA kama wapo wadau au wanamichezo wanaendelea kuamini kuwa ili wajiweke kwenye kiwango cha juu, au kuzipatia mafanikio timu zao, basi ni lazima wapate waganga makini wa kuwapaatia dawa za kienyeji.

Kama watu hao wapo katika Dunia ya leo, hakika wanajidanganya, maana hatupo huko leo. Dunia ya leo, kuweka ushirikina mbele hasa katika masuala ya michezo, ukiwamo mpira wa miguu ni kuharibu zaidi mfumo na harakati zote za kimaendeleo.

Kwanini nasema hivyo? Soka linahitaji muda wa kufanya mazoezi makali na wala sio kushindana kwa tunguli. Kama ushirikina ni jambo jema katika soka, basi mikoa inayosifika kwa uchawi leo hii ingetoa wachezaji wengi wa timu ya Taifa, au kuwajaza katika timu zetu.

Kama upo uganga wa kuleta tija katika michezo, kwanini Tanzania haishiriki michuano mikubwa, ikiwamo Kombe la Mataifa ya Afrika, bila kusahau Kombe la Dunia?

Nasema hivi huku nikiamini licha Dunia kubadilika zaidi, lakini baadhi ya wachezaji wetu wanaamini uchawi. Ingawa huwezi kuwataja kwa majina, lakini hakika huo ndio mtindo wao.

Kwasababu hiyo tu, mfumo mzima unachafuka. Hatuzalishi wachezaji wanaotafuta au kulinda viwango vyao kwa kuvuja jasho uwanjani zaidi ya wanaowaza miti shamba.

Huo sio mpango mzuri. Na sio muarobaini wa mafanikio yetu katika viwanja vya michezo. Kwa kulijua hilo, hakika siwezi kuvumilia kamwe na kuna haja ya kujifanyia marekebisho.

Sisi wadau wa michezo, wanamichezo na wengineo tuwakosoe au kuwapa mawazo mapya vijana wetu kwa kuwaaminisha kuwa uchawi sio njia ya mkato katika maisha yao.

Kuna haja ya kupangilia muda wao. Kuhakikisha kuwa wanafanya mazoezi ya kutosha ili miili yao kuwa imara zaidi. Wahakikishe pia wanakuwa na wataalaamu wa viungo. Vijana hao lazima pia wajuwe ili wawe na nguvu, lazima wapangilie mlo wao.

Kama mchezaji anakula chips kavu na soda moja, hata kama achanjwe mwili mzima, hawezi kushindana na wachezaji wenye nguvu, kama vile Samuel Et’oo, Didie Drogba na wengineo wanaowika katika soka la Afrika kwa timu zao za Taifa.

Hawa wachezaji haswa wa Afrika Magharibi, ambao Ulaya wamekuwa na soko zaidi, hawagombaniwi eti kwakuwa nchi zao ni wachawi sana, bali kwakuwa wamedhaamiria kuvuna fedha za wazungu.

Mtu ambaye hapangilii mlo wake, muda wake wa mazoezi kama ilivyokuwa kwa nyota wengine duniani, bado hawezi kuwika duniani, japo nyumbani kwao kuna mkoba wa uganga.

Huo ndio ukweli wa mambo. Yule mchezaji ambaye ana ndoto za kucheza soka kulipwa na bado akawa hodari wa (misumari) uchawi, hakika anajidanganya na kupoteza muda wake.

Dawa ni moja tu. Kufahamu hitaji husika, kujiwekea malengo kuanzia hatua ya chini hadi anapohitaji mchezaji husika. Kinyume cha hapo Taifa litazidi kupata hasara bure.

Kwa sisi ambao tumekuwa tukifuatilia soka kwa ukaribu zaidi, malalamiko ya baadhi ya wachezaji kuwa wanarogwa yameshakuwa kawaida mno hadi kutia kinyaa.

Kwa mfano, nyota wa kulipwa wa timu ya Yanga, Didier Kaavumbagu, alimtangaza hadharani Jerry Tegete kuwa anamroga. Kauli kama hii ni chungu na endelezo la uchawi kwa soka letu.

Ingawa madai ya Kavumbagu yanaweza kuchukuliwa kama uongo, lakini kwa soka la Tanzania, ni wazi ushirikina upo na unapewa nafasi kubwa hata na baadhi ya viongozi wa timu hizo.

Kwa mfano, wapo wanaoamini kuwa benchi la ufundi, lazima likamilike kwa kuundiwa pia mtu wa kuhakikisha kuwa uchawi unafanya kazi ili washinde mchezo husika.

Tena mambo kama haya hutokea zaidi kwa mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga, timu kongwe zenye ‘madudu’ mengi mno. Utaona vioja vya kila aina, yakiwamo mayai viza au ndege wa ajabu kurushwa angani.

Hatuwezi kwenda hivyo waungwana. Siwezi kuvumilia kamwe, hivyo Shirikisho la Soka nchini (TFF), lazima liwabane wote wenye kuendekeza vitendo vya ushirikina maana ni kaburi la sokaa letu.

Kwa wale wasioamini kuwa wapo watu wanaofanya ushirikina kwa soka la Tanzania, waanze kufuatilia zaidi maisha ya wanasoka wetu, viongozi wetu na siku za mechi zao.

Utashangaa pale kipa au beki anavyohaha kutaka kufukia uchafu wake uwanjani, akiamini ni silaha ya kumfanya awike uwanjani, wakati ni uongo mtu na kuharibu kiwango chake.

Swali, unaweza kuroga upate namba kwa wachezaji wenzako Tanzania, vipi ukienda kujaribiwa Manchester United? Je, utahangaika katika Uwanja wa Old Trafford ili ufukie hirizi?

Acheni hizo, chezeni soka, maana uchawi ungekuwa tija, mikoa inayoheshimika kwa ndumba ingetwaa Kombe la Dunia au kuwa na klabu zinazonyakua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment