Pages

Pages

Monday, February 04, 2013

Michael Wambura atupwa mchakato wa Uchaguzi TFF




Michael Wambura, akisisitiza jambo, sio leo.

Na Mwandishi Wetu, TFF
Jamal Malinzi amepeta, sasa ni mgombea rasmi wa urais TFF

MATUMAINI ya Katibu Mkuu wa zamani wa Chama Cha Soka Tanzania (FAT), sasa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Michael Wambura, yametoweka rasmi leo baada ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF, ikiwa chini ya Deogratius Lyato, kumtupa nje.

Sababu zilizomuondoa katika mchakato huo wa uchaguzi wa ni ule ule wa kupeleka mambo ya soka katika mahakama za kawaida, sambamba na kukosa uadilifu. Aidha, wagombea wa Urais, Jamal Malinzi na Athumani Nyamlani wao wamepita, huku nafasi ya Makamu wa Rais sasa ikibaki kuwaniwa na Wallace Karia na Ramadhan Nassib.

Mbali na Wambura, wagombea wa nafasi mbalimbali ukiwamo Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wapatao 1o nao wametupwa nje, akiwamo mwandishi wa habari za michezo, Shafii Dauda, aliyetupwa kwasababu za kudanganya umma baada ya kuenguliwa katika Uchaguzi wa IDFA.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo mchana, Lyato alisema Wambura ameondolewa katika mchakato wa Uchaguzi huo kwa madai ya siku zote, yakiwamo uadilifu na kuwahi kupeleka masuala ya soka, klabu ya Simba, katika Mahakama za kawaida, hivyo kujitilia gundu la kutupwa nje kila anapojaribu kuota nafasi za uongozi.

Alisema kuwa wapinzani wake, Wallace Karia na Ramadhan Nassib, sasa wamepeta kuelekea kwenye Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Februari 24, ambapo pia katika nafasi ya Urais, wagombea Malinzi na Nyamlani nao wakipeta, huku Omary Mussa Nkwarulo naye akiwekwa kando  kwasababu za kukosa ufahamu katika nafasi anayoomba ya kuwania Urais wa Shirikisho hilo.

Mbali na matokeo hayo, Kamati ya Uchaguzi imewapitisha wagombea wa nafasi ya Bodi ya Ligi, Yusuph Manji na Hamad Yahya Juma kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, huku Said Mohamed akipita kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, wakati wajumbe waliopitishwa ni Kazimoto Miraji na Omary Khatib.

Alisema kwa ujumla kila aliyewekwa kando katika uchaguzi ametolewa kwa kutokidhi vigezo kwenye Kanuni na Katiba wa TFF, vikiwamo elimu, uadilifu ama mkanganyiko ulitokea katika fomu za maombi ya kupitishwa kwenye mchakato huo.

Mbali na Wambura ambaye ametolewa kwasababu za kupeleka soka mahakamani, lakini wapo ambao nao wametupwa nje, akiwamo waliomba kugombea nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wakiongozwa nao Abdalla Mussa, Mbasha Matutu, Charles Mugondo,  Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Iliud Mvella,Farid Nahdi,  Hassan Hassanoo, Omary Isaac na Shafii Dauda.

“Wajumbe waliopitishwa kuwania nafasi ya Ujumbe ni pamoja na Alex Kamuzelya, Juma Pinto, Muhsin Said Balhabou, waliopitishwa katika Kanda ya 13, ambayo ni jiji la Dar es Salaam, huku Davis Mosha, Khalid Abdallah, Kusianga Mohamed waliopitishwa kwa Kanda ya 12 ambayo ni Mkoa wa Kilimanjaro na Tanga.

“Wajumbe wengine waliopitishwa kwa Kanda ya 11 ni Riziki Juma na Twahil Twaha, huku nafasi ya kutoka Kanda ya 10 ya Mkoa wa Dodoma na Singida, wakati Kanda ya 9 ambayo ni Mtwara na Lindi ikienda kwa Athuman Kambi, Francis Kumba, Zafarani Damoder,  huku Kanda ya 8 kwa mikoa ya Ruvuma na Njombe, ikichukuliwa na James Mhagama, Stanley Lugenge,” alisema.

Lyato aliwataja wengine kuwa ni kutoka Kanda ya 7 ambayo ni Iringa na Mbeya, ikienda kwa Davis Samson, John Exavery na Lusekelo Mwanjala, wakati Kanda ya 6 ilienda kwa Blassy Mghube, Selemani Bandiho Kameya, wakati Kanda ya 5 ambayo ni Tabora na Kigoma wametangazwa Msafiri Mgoi na Yusuph Kitumbo.

Wengine waliopitishwa Kanda ya 4 wakiwa ni Elley Simon, Omary Ally, wakitoka mikoa ya Arusha na Manyara, wakati Kanda ya 3 ambayo ni mikoa ya Shinyanga na Simiyu imeenda kwa Epaphra Swai, huku Kanda ya 2 ikienda kwa Jumbe Magali, Mugisha Garibona, Samuel Nyalla,  Vedastus Lufano hawa wakipitishwa huku wakitoka mikoa ya Mwanza na Mara, wakati Kanda 1 ikiwa na mikoa ya Kagera na Geita na kupitishwa Kalilo Samson na Salum Hamis Umande.

Uchaguzi wa TFF umepangwa kufanyika Februari 24, wakati ule wa Bodi ya Ligi ukitarajiwa kufanyika Februari 22, ambapo patashika ya kuelekea kwenye tukio hilo ukizidi kupamba moto.

Kumalizika kwa mchakato huo wa usaili, sasa unasababisha kuweka msuguano zaidi kwa nafasi mbili za Malinzi na Nyamlani, kutokana na mvuto wao katika soka nchini.

No comments:

Post a Comment