Pages

Pages

Wednesday, February 27, 2013

Dawa zaadimika Hospitali ya Wilaya Kilwa



Mkuu wa Wilaya Kilwa, Abdallah Ulega.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HOSPITALI ya Wilaya ya Kilwa imelalamikiwa na wananchi wilayani humo kwa kukosa dawa, hali inayowapa wakati mgumu wagonjwa wanaopelekwa hapo kupata matibabu, huku dawa pekee inayopatikana ikiwa ni Panadol.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya wananchi wa wilayani Kilwa walisema kuwa kukosekana kwa dawa kwenye hospitali hiyo kunasababisha watu waishi kwa tabu, huku wengine wakipata madhara makubwa zaidi.

Alisema mara kwa mara majibu yanayotolewa  na viongozi kwenye hospitali hiyo ni kukosekana kwa dawa, jambo ambalo kwa wananchi wanaotegemea uwepo wa hospitali ya serikali kunawaweka kwenye wakati mgumu.

Akizungumzia taarifa hizo kwa njia ya simu, Mkuu wa wilaya wa Kilwa, Abdallah Ulega, alisema matatizo ya dawa kwenye hospitali ya wilaya yake si habari ngeni, huku akisema kukosekana huko wakati mwingine ni kuchelewa kufika kwa fedha za kununulia dawa.

Alisema kuwa juhudi zinazofanywa na serikali ya wilaya ni kufanya mazungumzo na wanaoshughulia na usambazaji wa dawa, ambao ni Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ili kutatua changamoto ya ukosefu wa dawa katika Hospitali hiyo.

“Hospitali nyingi katika baadhi ya wilaya zetu zinaweza kufikwa na upungufu wa dawa, maana kabla ya kufika, kunakuwa na mizunguuko ya hapa na pale, ingawa lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wake wanaishi vizuri na kupata matibabu.

“Kwa pamoja tutaliangalia suala hilo na kufanya kazi kwa nguvu zote kuwahadumia Watanzania, wakiwamo wa wilayani Kilwa kwa kusimamia vyema na kushauri au kutoa taarifa inapofikia suala la kukosekana kwa dawa za aina yoyote ile katika hospitali zetu,” alisema.


No comments:

Post a Comment