Pages

Pages

Wednesday, February 27, 2013

Extra Bongo yajivunia watatu wake wapya



Nadine Conpresor, mcheza shoo mpya wa Extra Bongo akionyesha umahiri wake, mbele ya repa wake, Papy Catalogue.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENDI ya Extra Bongo, jana iliwatambulisha wanamuziki watatu, akiwamo Papy Catalogue repa aliyewahi kufanya kazi na FM Academia, Nadine Conpresor, mnenguaji aliyetoka Akudo Impact na Adam Mbombole, mwimbaji kutoka K-Mondo Sound zote za jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Choki, alisema kwamba kuwatambulisha wanamuziki hao ni ishara ya kuboresha na kuiweka juu zaidi katika kipindi chote cha muziki wa dansi nchini.


Alisema repa wao, Catalogue ni mahiri anapokuwa jukwaani, huku akiamini kuwa ataleta kitu kipya katika bendi yake mpya, akishirikiana na waimbaji wote wenye uchu wa kufanya vyema katika maisha ya muziki wa dansi.

"Naamini wadau na mashabiki wetu watapata kitu adimu kutoka kwa wanamuziki hawa ambao kwakweli ni wenye uwezo, akiwamo Nadine, Catalogue na Adam, ambao kwa hakika huko walipokuwapo awali walijiweka juu kwa kuyatangaza majina na heshima zao.

"Tunaamini hawa ni wenzetu na tutaendelea kufanya nao kazi kwa mafanikio makubwa zaidi, hivyo mashabiki wetu wawapokee vijana hawa kwa ajili ya kutuletea burudani kamili kama walivyojulikana kwa umahiri wao,” alisema Choki.

Akizungumza kwa kujiamini zaidi, Catalogue alisema kuwa hana maneno mengi ya kusema zaidi ya kuwaahidi wadau wake vitu vikali na kuhakikisha kwamba Extra Bongo inaendelea kuwa juu katika harakati zao kimuziki.

“Sitaki kusema sana zaidi ya kuwoamba ushirikiano mashabiki wangu waje hapa nilipokuwa kuanzia leo (jana), maana sijashuka kwasababu uwezo wangu hakuna repa mwingine anayeweza kufuata nyayo zangu mimi steringi,” alisema Catalogue.

Naye Nadine alisema ameondoka Akudo kwa kutafuta maisha zaidi, huku akisema kuwa hakuna mizengwe yoyote, kwakuwa hakuwa na mkataba unaombana kiasi cha kushindwa kuikacha.

No comments:

Post a Comment