Kikosi cha Yanga
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Yanga iliyopiga kambi ya
mazoezi kwa takribani wiki mbili mjini Antalya, Uturuki itaanza mzunguko wa
pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi itakayochezwa keshokutwa (Januari
27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vinara hao wa VPL
wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Azam wanaowafuatia wanaikabili
Tanzania Prisons ambayo imetumia dirisha dogo kuongeza wachezaji wawili akiwemo
mshambuliaji mkongwe Emmanuel Gabriel.
Timu hizo zilitoka
suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine, jijini Mbeya. Hivyo kiu ya washabiki ni kutaka kujua nani ataibuka
mbabe kati ya timu hizo msimu huu.
Wakati ameingiza
wachezaji wawili kwenye dirisha dogo, Kocha wa Tanzania Prisons, Jumanne Chale
amempoteza David Mwantika katika dirisa hilo. Beki huyo ametua katika timu ya
Azam.
Aidha, timu ya African Lyon ndiyo klabu
iliyoongoza kwa kusajili wachezaji wengi kwenye dirisha dogo kwa ajili ya
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaotoa bingwa wa Tanzania Bara,
lakini pia timu tatu ambazo msimu ujao zitarudi kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Kati ya wachezaji 65
waliotua katika klabu mbalimbali katika dirisha hilo, Lyon ndiyo iliyoongoza
kwa kuwanasa 12. Miongoni mwao hao, wawili (Ibrahim Job na Shamte Ally)
imewachukua kwa mkopo kutoka Yanga.
Pia watano imewapandisha
kutoka katika kikosi chake cha U 20. Wachezaji hao ni Nurdin Musa, Salvatory
Jackson, Mohamed Athuman, Athuman Kajembe na jarufu Kizombi. Wengine walioingia
katika timu hiyo katika dirisha dogo ni Juma Seif (Huru), Buya Jamwaka (Burkina
Faso), Takang Valentine (Huru) na Yusuf Mgwao (Huru).
Nayo Polisi Morogoro
katika kuhakikisha inaondoka mkiani mwa ligi imesajili wachezaji wanane katika
dirisha dogo kama ilivyofanya Oljoro JKT ya Arusha.
Wachezaji wa kigeni
walioingia katika dirisha dogo ni Humphrey Mieno, Brian Umony, Jockins Atudo
(Azam), Donald Obimma na Ulugbe Chika (Toto Africans), Zuberi Hamis na Tinashe
Machemedze (Coastal Union), Musa Mudde na Abel Dhaila (Simba).
No comments:
Post a Comment