Pages

Pages

Friday, January 04, 2013

MGODI UNAOTEMBEA



 
Tatizo ni gesi, siasa au choyo na ubaguzi?
Waandamanaji wanaopinga gesi kuja Dar es Salaam.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TANZANIA yetu inazidi kuingia katika shimo baya la uvunjifu wa amani, kutokana na baadhi yao kufanya mambo kwa faida yao. Kwa bahati mbaya, habari nyingi mbaya zinazotokea katika Taifa letu, zinapokewa vibaya na wadau wengi.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo

Sio jambo geni. Inajulikana kuwa habari mbaya ndiyo inayovuma sana kuliko ile nzuri. Vitu kama migomo na maandamano ni kawaida sasa. Leo hii kusikia kiongozi Fulani amepigwa risasi au kanisa limechomwa moto pia ni kawaida.

Kuna msomaji wangu alinitumia meseji fupi tu. Ilisomeka hivi; ‘hii ndio Tanzania uitakayo ya migomo, vurugu na maandamano’. Ujumbe wa msomaji huyo uliingia akielezea zaidi maandamano ya Watanzania wa Lindi na Mtwara kupinga gesi kusafirishwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika

Ujumbe huu sijaushangaa. Sijaushangaa maana aliyeutuma aliubadilisha kutoka kwa wanaodai haki ya kuitosafirisha gesi hiyo hadi lawama kwa Serikali, hasa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wenyewe wanadai kuwa tatizo ni CCM. Sawa, hayo ndio maono ya baadhi yao, lakini najiuliza kiini cha maandamano ya watu wa Mtwara. Kwanini nasema hivyo. Ni dhahiri kadhia hiyo imebadilishwa mbinu na kushambuliwa zaidi CCM na serikali yake.

Kama hivyo ndivyo, sioni kwanini wananchi wa Mtwara waliweza kubeba mabango yaliyosema Mtwara kwanza vyama baadaye. 

Wakati watu wanasema hivyo, wanasahau kuwa maandamano yameratibiwa kwa kiasi kikubwa na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, wakishirikiana na wananchi wa mikoa hiyo.

Maandamano hayo yalianzia katika kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.

Pamoja na kuwa na hoja nzuri ya kudai haki ya gesi asilia, lakini kwa undani zaidi sakata hilo lilipaliwa kisiasa. Watu walikuwa kwenye kazi ya kunufaisha vyama vyao vya siasa. Hili ukisema, baadhi yao hawatakubali.

Katika kulijua hilo, lazima kila Mtanzania awe tayari kutetea rasilimali za Taifa bila kuangalia zilizokuwapo katika Mkoa wake. Wananchi wa Mtwara na Lindi kazi yao ni kudai maendeleo na si kuandamana wakitaka gesi hiyo ibaki kwao.

Ndio maana nasema, huenda wazo lilikuwa zuri, lakini limeharibiwa kwa kuratibiwa kisiasa zaidi, ndio maana tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakiinua midomo yao, wakiwa na nia ya kukidhoofisha zaidi Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, ikiwa chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, rasilimali zote zinazopatikana katika Taifa hili, zinatumika kwa ajili ya Watanzania wote na sio wa eneo moja linapopatikana katika mkoa husika.

Ni kauli njema inayotoa shaka kuwa sisi sote tunaishi katika Taifa moja, hivyo sioni ubaguzi unakujaje katika jambo kama hilo. Mtwara wangekuwa na hoja kama licha ya bidhaa hiyo, gesi asilia kutoka kwao, lakini serikali haitatui kero zao.

Mtwara wangelia zaidi, kama wamegundua gesi asilia inayotoka kwao, inatumika vibaya, au ikinufaisha mataifa mengine. Kuisema hoja hii lazima ujifanye chizi usiyeumizwa na hoja dhaifu za baadhi ya Watanzania.

Kila anayepambana na suala hilo la gesi asilia, hakika kwa asilimia kadhaa anatatua kero hiyo kwa faida ya chama chake cha siasa. Watu wa aina hiyo hawastahili kuchekewa. Hatuwezi kujiendesha kwa kuangalia mikoa, majimbo au vijiji vyenye rasilimali husika.

Kama hivyo ndivyo, Taifa hili haliwezi kuwa moja. Litameguka kadri siku zinavyokwenda mbele, huku shari hiyo ikijengwa zaidi na wanasiasa. Siasa za vyama vingi hazijaletwa ili zivunje amani ya Watanzania.

Siasa hizo zimekuja ili kuwa wakosoaji wakubwa wa serikali, lakini si kwa kila linalofanywa hata kama liwe na tija linastahili kukemewa. Huo ndio ukweli. Lazima tufanye mambo yetu kwa kuangalia matokeo sahihi.

Tunajiendesha vibaya kwa kuingiza chembe chembe za siasa za vyama vyetu vya siasa, bila kuangalia hasara inayoweza kupatikana. Tangu kuibuka kwa sakata hilo la maandamano ya Mtwara, nilibaki najiuliza faida na hasara.

Mkoa wa Mtwara hauna mbunge kutoka upinzani. Wabunge wote ni CCM. Lakini Lindi kuna majimbo mawili yanayoshikiliwa na Chama cha Wananchi (CUF).

Kwa maana hiyo, nashawishika kusema kuna dalili kuwa sakata hili la gesi asilia limebebwa katika mgongo wa siasa, wakiwa na lengo la kuonyesha ukarimu wao kwa wananchi wa Mtwara.

Kama ni uongo, basi upo karibu na ukweli. Wakati mwingine nasema, kinachotakiwa ni kuweka mbele maslahi ya Taifa. Hilo suala la nani anapaswa au hapaswi kunufaika linahitaji kuwekwa kando.

Hivi kabla ya gesi hiyo haijagunduliwa, serikali haipaswi kuwahudumia watu wa Lindi na Mtwara? Je, maeneo ambayo hayana rasilimali kama hizo za gesi, madini nazo hazipaswi kuhudumiwa na serikali yao?

Mimi nilidhani viongozi wa mkoa, kuanzia madiwani, wabunge na wengineo wangekaa na kujadili namna gani Taifa linaweza kunufaika na rasilimali hizo. Lakini kuanza kuweka chokochoko kutoka katika vichwa vya walalahoi ni kuwasumbua.

Muda huo wa maandamano ungetumiwa kubuni namna gani ya kujiletea maendeleo kwa kupitia fursa za kiuchumi na sio kupambana naa nguvu za dola. Huu ndio ukweli. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu, Joseph Simbakalia, aliwajia juu watu hao kwa madai kuwa ajenda yao hiyo haina mashiko.

Simbakalia alishangazwa pia na baadhi ya watu kwenye maandamano hayo waliotaka atimuliwe katika Mkoa huo. Mambo kama haya hutokea katika migogoro na maandamano mengi kutoka katika kila mahali.

Nilipenda kauli ya John Mnyika, Mbunge wa Ubungo, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini juu ya kutumia nafasi yake bungeni kuomba nakala ya mkataba wa mkopo wa Dola za Kimarekani Bilioni 1.225, sawa na Shilingi Trilioni 1.86 kutoka nchini China kwa ajili ya kujenga miundo mbinu ya kusafirisha gesi hiyo asilia kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Kauli ya Mnyika imekuja wakati tayari chama chake kilishiriki kwa karibu kuratibu maandamano hayo. Kumbe alikuwa na malengo haya, kwanini wasingeshauri wananchi wao, kama uwezo huo wanao kusubiri hadi aone nakala hiyo?

Kikubwa ni maendeleo ya Tanzania na sio mkoa gani unastahili kubakiwa na rasilimali husika. Hatuwezi kujiendesha kimkoa, kimajimbo au wilaya kama wanavyotaka baadhi ya watu, maana ajenda hii ni mbaya na haina mashiko.

Ifikie wakati watu waache porojo, nyimbo za kisiasa kwa kuangalia zaidi maendeleo ya Tanzania, iwe kwenye gesi, madini na mengineyo. Tusipofanya hivyo, hatari itakuwa kubwa, maana tunazalisha sumu ya kuleta mapigano wakati ingeweza kujadiliwa kwa amani kwa kutumia vikao na nia ya dhati ya tunu ya Taifa letu.

Tusimtafute mchawi, lakini pia watu wa Mtwara na Lindi wajuwe hawapaswi kufanya vurugu kwa kulala barabarani, kuandamana au kurushiana maneno na viongozi wa serikali, huku ajenda yao ni kutaka rasilimali walizonazo zisiende kwingine kwa sababu za choyo, roho mbaya na fitina zinazojengwa zaidi na wanasiasa wetu wenye sera ya kujiendesha kwa majimbo.

0712 053949
0753 806087


No comments:

Post a Comment