Pages

Pages

Friday, January 04, 2013

Safari ya mwisho ya Sajuki leo

R.I.P Sajuki


Msanii wa filamu, Jini Kabula akiwa kwenye msiba wa marehemu Sajuki, maeneo ya Tabata Bima jana
  
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
LEO saa tano za asubuhi, mwili wa msanii maarufu nchini, Juma Kilowoko, Sajuki unazikwa katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam kuashiria kuwa ni kweli mwisho wa uhai wa kijana huyo umefika.

Msanii Tuesday Kihangala akiwa msibani kwa Sajuki

Sajuki alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhuzunisha wengi, wakiwamo wasanii, mashabiki na serikali kwa ujumla kutokana na ubora wake kwenye sanaa.

Taratibu za mazishi za Sajuki zimeshakamilika huku kamati mbalimbali za kuratibu shughuli hiyo zikifanywa kwa umakini mkubwa.


Eneo la nyumba ya Sajuki, Tabata Bima, mashabiki wengi walijitokeza kuomboleza msiba wa msanii huyo aliyeuigua kwa muda mrefu kabla ya kifo chake.

Awali, ilitarajiwa kuwa Sajuki angezikwa kwao Songea, lakini wasanii waliomba familia ya Sajuki ili Watanzania wanaoishi jijini Dar es Salaam washiriki kwa karibu kwakuwa ndipo alipoishi marehemu kwa muda mrefu.

Serikali kwa kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, walionyesha kuguswa na msiba huo mzito.

Kabla ya kifo chake, marehemu Sajuki, aliugua kwa miaka miwili, hali iliyosababisha aende India kutibiwa, ambapo safari hiyo ilitokana na michango ya Watanzania wenye mapenzi na kijana huyo.

Hata hivyo, safari ya Sajuki ilizua ugonjwa mwingine katika uchunguzi wa madaktari ambao kwa pamoja walisema msanii huyo alikuwa na ugonjwa kansa ya ngozi.

Mara baada ya kurudi jijini Dar es Salaam, msanii huyo alikuwa kwenye afya kwa kiasi kidogo, hata hivyo changamoto za kupata fedha za kumrudisha tena nchini India Desemba mwaka jana, zilimfanya Sajuki ashindwe kurudi huko, licha ya kuhangaika kwa kiasi kikubwa, ikiwamo kufanya shoo mbalimbali.

Mwaka jana mwishoni, Sajuki alifanya shoo jijini Arusha, ambapo matokeo yake yalikuwa machungu zaidi baada ya msanii huyo kuanguka na kuwahishwa hospitali ya Amana, alipomzishwa kwa muda na baadaye kupelekwa Muhimbili alipoiaga Dunia na kuacha majonzi kwa Watanzania wapenda sanaa za maigizo na filamu hapa nchini.

No comments:

Post a Comment