Pages

Pages

Friday, January 04, 2013

Kilindi yaapa kula sahani moja na wenyeviti wa vijiji

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

MKUU wa Wilaya ya Kilindi (pichani), mkoani Tanga, Selemani Liwowa, amesema watakuwa wakali zaidi na wenyeviti wa Serikali za vijiji ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kunufaisha matumbo yao, ikiwamo kuingiza wafugaji bila utaratibu. 

 Liwowa aliyasema hayo mapema leo kutokana na wilaya yake kuathiriwa sana na uingiaji wa wafugaji wanaovamia katika vijiji vyao kutokana na kufadhiliwa na wenyeviti wa vijiji. 

Akizungumza zaidi, Liwowa alisema serikali haipo tayari kusumbuliwa na wenyeviti ambao wamekuwa wepesi kuvunja sheria kwa kuwaingiza wafugaji kinyume cha utaratibu kwa makubaliano wanayojua wenyewe. 

Alisema wapo wafugaji ambao wamekuwa wakiingia katika vijiji kila kukicha kutokana na kuwa na makubaliano na viongozi wa vijiji jambo ambalo huwa na mashaka makubwa pale mifugo inapofanya uharibifu kwa wakulima. 

“Tanzania ni yetu wote na kila mmoja anaweza kuishi mahali anapotaka, ila lazima utaratibu ufuatwe hasa kwa ndugu zetu wafugaji ambao hawa sehemu nyingi wanapoingia baadaye huzuka tafrani kubwa na kuleta balaa.

“Kilindi tutakuwa makini na wenyeviti hao kwa sababu hatupo tayari kuona sheria zinavunjwa na “kuleta mgogoro kwa wakulima na wafugaji kama uliowahi kutokea hivi karibuni katika wilaya yangu,” alisema Liwowa. 

Wilaya ya Klindi ipo mkoani Tanga, huku ikikabiriwa na wimbi kubwa la wafugaji wanaoingia kwa wingi kutafuta hifadhi yao pamoja na mifugo yao.

No comments:

Post a Comment