Pages

Pages

Tuesday, December 11, 2012

SIWEZI KUVUMILIA

Nidhamu iangaliwe upya na wanasoka wetu
Mshambuliaji tegemeo wa Simba, Haruna Moshi 'Boban'.
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATAALAMU wengi katika mpira wa miguu wanailezea nidhamu kama silaha ya kuwaletea mafanikio makubwa wachezaji wetu. Sio Tanzania tu, bali na Dunia nzima suala la nidhyamu hupewa kipaumbele na wanasoka wetu.

Bila nidhamu, wachezaji ni ngumu kwao kuwika, ndio maana katika kila timu, wamewekwa watu wa kuwaongoza wana michezo wetu, hasa wa mpira wa miguu, ili iwe nafasi yao ya kuonyesha makali yao.

Licha ya kuwa na vipaji vya aina yake, lakini wachezaji ambao nidhamu kwao ni mtihani mgumu, hakika hawana sababu ya kukubalika katika soka. Ni watu wa kucheza nyumbani kwao. Wakivuka mpaka, hushindwa na kurudi tena kwao.

Wakiwa kwao nao huvuma na kusahaulika, kwakuwa makocha wenye kanuni zao haswa, kuwatumia wachezaji wa aina hiyo ni ngumu sana. Hayo ni matatizo ya wachezaji wa Tanzania. Wengi wao hawaipendi nidhamu.

Wapo tayari kukwepa mazoezi au kusingizia ugonjwa. Wasipokwepa mazoezi, basi hujiweka bila kufuata ushauri wa walimu wao, hivyo kuanza kuibua mzozo mzito unaosababisha vurumai katika nyakati mbalimbali.

Kwa kulijua hilo, wachezaji wetu wana kila sababu ya kuangalia malengo yao katika soka. Kama wana ndoto za kucheza soka la kulipwa, basi wajuwe bila kuwa na nidhamu, kuwaheshimu wachezaji wenzake na makocha wao ni ngumu.

Kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, kunaleta mvuto na ufanisi mkubwa wa kujiweka juu katika ramani ya soka. Angalia, mshambuliaji tegemeo wa Simba, Haruna Moshi Boban, amekuwa akiingia lawamani kila wakati.

Juzi aliwaambia viongozi na kocha wake kuwa ni mgonjwa, hivyo hataweza kwenda Tanga kucheza na Mgambo Shooting, mchezo uliomalizika kwa timu hizo kugawana pointi.

Lakini, siku moja baadaye Boban alionekana uwanjani akicheza kwenye timu za mchangani, jambo ambalo ni baya sana. Hili haliwezi kumsaidia kamwe.

Ndio, huenda ameshajua kwa umri wake ni ngumu tena kufikia mafanikio yaw engine duniani, lakini tabia yake inaharibu kizazi cha wanamichezo, ukiwamo huo mpira wa miguu.

Wale wachezaji wadogo wanaopenda kuwa kama yeye, wanajifunza nini kutoka kwake? Sio Boban tu, baali wachezaji wengi wa Tanzania hayo ndio mapungufu yao. Mara kadhaa wanachofundishwa katika mazoezi ni tofauti na wanachokionyesha.

Haya hayastahili kuchekewa kamwe. Wachezaji wetu lazima wajuwe na namna ya kung’amua namna ya kujiendesha kama kweli wanahitaji kuwa wana soka wa kulipwa. Bila hivyo wataendelea kupoteza muda wao au kuishia vihela vya kula nyumbani kwao.

Ukiangalia kwa haraka, utagundua kwamba kila anayevuma duniani nidhamu anayo. Mchezaji kama huyu Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, wanaweza kutimiza ndoto zao, maana nidhamu wanazo na wana kiu ya mafanikio.

Mtu kama vile Henry Joseph Shindika anayecheza soka la kulipwa Norway, nidhamu anayo, ndio maana alikuwa chaguo la kocha Marcio Maximo na wengine waliorithi kiatu chake. Hatuwezi kukimbia nidhamu. Yoyote anapaswa kuwa nayo, wakiwamo wanamichezo.

Wachezaji wetu wa Tanzania lazima wajuwe kuwa mafanikio yao yatachangiwa na mambo mengi sana, ikiwamo hiyo nidhamu inayoliliwa na kila mmoja wetu. Maximo, aliwahi kusema hilo mara kwa mara kuwa wengi aliowafungia vioo hawana nidhamu.

Wachezaji kama vile Juma Kaseja, Boban, Athuman Idd na wengine, aliwalilia sana. Waliokuwa hawataki uamuzi wake huo, walilazimishwa kuukubali. Makocha hao wanafanya hivyo kwakujua kuwa ni muhimu kwa ajili ya mafanikio yao.

Kinyume cha hapo, wachezaji wetu wa Tanzania wasiopenda kuikumbatia nidhamu ndani na nje ya uwanja, wajaribu na kazi nyingine maana kuvuna fedha nyingi kama wanavyofanya wengineo duniani, hilo ni jambo gumu mno.

Kwa bahati mbaya, wapo wachezaji ambao kitu kama hicho kwao ni kigumu na ndio maana wanashindwa kuwika. Wanacheza soka la ndani miaka yote. Kuna wachezaji ambao husingizia wanaumwa, lakini baadaye huonekana wakicheza soka la mchangani.

Ama wengine kutoripoti kambini kwa wakati au kutoa visingizio vya kila aina, hivyo kuwaharibia kwa kiasi kikubwa. Huu ni muda wa mabadiliko kwa wachezaji wetu. Na ndio maana siwezi kuvumilia katika hilo.

Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment