Pages

Pages

Tuesday, December 11, 2012

CCM Handeni wapiga mkwara wenyeviti wa vijiji


Na Kambi Mbwana, Handeni
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Handeni, Athuman Malunda, amesema kuwa baadhi ya wenyeviti wa serikali ya vijiji ni watu wanaopenda kujiweka juu na kushindwa kuongoza kwa ufanisi.

Hali hiyo inaweza kuwaangusha kama hawataweza kujirekebisha kwa faida ya vijiji vyao, chama na serikali kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, baadaye mwakani.

Akizungumza jana mjini hapa na Handeni Kwetu, Malunda alisema wenyeviti hao wanajiona wao ni miungu watu kwa kutaka waabudiwe, sambamba na kushindwa kuitisha mikutano ya vijiji vyao, hivyo ni jambo baya.

Alisema kwakuwa wenyeviti hao wapo chini ya chama chao, watahakikisha kuwa wanawaongoza vizuri kwa ajili ya kufanya kazi zao kwa ufanisi ikiwa ni hatua nzuri ya kushinda katika uchaguzi huo wilaya nzima.

“Wenyeviti wa aina hiyo hatuwezi kuwachekea kwa kuwafanya wawachukize wananchi wao, badala yake tunataka wajishushe kabisa kwa wananchi, ukizingatia kuwa ni hatua nzuri katika hali ya kuleta maendeleo.

“Bila hivyo, wananchi watakuwa na chuki nao, hivyo kushindwa kuleta maisha bora sambamba na kukiangusha chama chetu kinachopendwa na kuheshimiwa na Watanzania wote, ndio maana Handeni hakuna mwenyekiti wa upinzani wa vijiji vyetu,” alisema.

Wilaya ya Handeni ni miongoni mwa wilaya za Tanzania Bara ambazo vyama vya Upinzani vimeshindwa kufurukuta katika chaguzi mbalimbali, tangu kuingia kwa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

No comments:

Post a Comment