Pages

Pages

Tuesday, December 25, 2012

REA na ufujaji wa fedha za umma



Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATAALAMU wa biashara wanaelewa kuwa ili uweze kuendelea lazima utumie fedha zako kimpango pamoja na kujua somo la kubana matumizi.

Kwa Tanzania hii ambayo wimbo wetu mkuu ni ukosefu wa bajeti, hatupaswi kufumba macho na kutumia Mamilioni ya shilingi kwasababu zisizokuwa na msingi.

Badala yake, viongozi na watendaji wa serikali kwa ujumla wanapaswa kuwa makini zaidi katika ufanyaji wao wa kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Wiki niliandika makala iliyokwenda kwa jina la “Sera ya umeme vijijini ipo kwenye makaratasi”.

Sikuwa na lengo la kuwasema vibaya watendaji zaidi ya kuwakumbusha wajibu wao, huku nikiamini kuwa wakati mwingine Mkurugenzi hawezi kujua kinachoendelea katika sehemu za vijiji hadi apelekewe ripoti na watu wake, huku baadhi yao wakishindwa kutembelea vijijini.

Katika hoja yangu hiyo, nilishangazwa na vitendo vya vijiji vinavyofaa kuwa na umeme vinaendelea kuwekwa kando, huku huduma hiyo ikipelekwa sehemu za mijini.

Nikatolea mfano wa vijiji vya Komsala na Kwakiliga kama mfano wangu kwa wilaya ya Handeni ambapo umeme umepita kutoka Korogwe kwenda Handeni na kuviacha vijiji hivyo bila sababu za kueleweka.

Kabla ya sijaendelea, nashukuru sana Wakala wa Nishati Vijijini REA, wametolea ufafanuzi kwa kutoa matangazo kwa magazeti mawili kwa kurasa mbili.

Kwa kutoa matangazo hayo, kuna uwezekano mkubwa REA wametumia kiasi cha pesa kisichopungua Milioni 10, ambapo sitaki kuamini kuwa fedha hizo zisingetosha kununua walau transfoma moja kwa ajili ya kijiji kimoja katika Taifa hili.

Lakini wapi. Fedha hizi zimetolewa bila sababu za msingi. Nabaki najiuliza maswali. Hizi fedha za serikali zinatumiwa kwa mtindo gani?

Naomba kuwa muwazi. Sina ugomvi na REA, Wizara ya Nishati na Madini au Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania TANESCO kama nilivyosema wiki iliyopita.

Makala yangu yana lengo la kukumbushana baina ya sisi watawala na waliokuwa kwenye nafasi za kutuongoza, huku tukijua hawawezi kufahamu yote.

Kwa bahati mbaya, REA wameitumia makala hiyo kuelezea kile kile nilichokisema katika makala yangu. Hata vile vijiji nilivyotaja, wamekiri tatizo hilo na kuahidi kulitatua kabla ya mwaka ujao kumalizika.

Ni jambo zuri. Kila Mtanzania wa kweli lazima apongeze jambo lolote la maendeleo. Na maendeleo hayawezi kuja bila kuwa na umeme wa uhakika.

Nanukuu. “Mwandishi wa makala hii amesema vijiji vya Komsala, Kwamatuku na Kwakiliga wilayani Handeni havijapitiwa na umeme licha ya nguzo na nyaya kupita katika vijiji hivyo.

Mtazamo wa mwandishi huyu unafanana na mtazamo wa wananchi wengi wanaoishi maeneo yaliyopitiwa na umemena Kwamatuku,” mwisho wa kunukuu.

Hapa Serikali kwa kupitia REA haijapinga mtazamo wangu huu kwakuwa nimewazungumzia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kusema.

Kwa mujibu wa REA kwa kupitia tangazo hilo lililosambazwa bila sababu za msingi, vijiji kukosa umeme hutegemeana na mazingira ya awali kwenye upimwaji au ukosefu wa bajeti ya kuweza kupelekewa huduma hiyo.

Ni kweli tatizo ni bajeti? Serikali na taasisi nyingine zimekuwa zikijiendesha ovyo ovyo. Hazina malengo zaidi ya kufuja fedha za umma.

Huu ndio ukweli. Kwa mfano, kama REA walikuwa na hamu kweli ya kutolea ufafanuzi wa suala hilo, kwanini wasitumie utaratibu wa kutuma press release kwenye vyombo vya habari au hata kuzungumza nao?

Badala ya kutumia fedha hizo kwa kutangaza ukweli, wangeziongeza kwenye bajeti yao kwa ajili ya kuwapatia huduma wananchi wao.

Sina utaalamu sana na mambo ya umeme, lakini Milioni 10 kama haitoshi kununua transfoma moja kwa ajili ya kijiji kimoja, pengo hilo lingepungua.

Nililipitia tangazo hilo zaidi ya mara tatu kwa ajili ya kulielewa na kuliweka kichwani mwangu. Kwakweli sijaona cha maana.

Zaidi nikajiuliza aliyoidhinisha tangazo hilo liende kwenye vyombo vya habari, wakati lenyewe linakiri mapungufu yaliyoelezwa na mwandishi.

Mbaya zaidi, REA wamefikia kujichanganya kwakusema kuwa kijiji cha Kwamatuku hakina umeme. Hapana.

Katika makala yangu sijasema kuwa kijiji hicho hakina umeme. Ninachojua, Kwamatuku kina umeme na wameupata baada ya kijiji hiki kuwa na wazungu waliokwenda kuwekeza kwenye kilimo.

Ajabu REA wenyewe hawajui hili. Kama tusiposema ukweli, kuna uwezekano baadaye wajanja wachache wakaandika kuwa wanapeleka umeme huo mwakani kama walivyosema katika tangazo lao.

Ukiangalia kwa haraka, utagundua kuwa REA wao wanalifanyia mzaha tatizo hili. Maneno waliyosema kwenye Tangazo, kuna uwezekano mkubwa wa kuyaingiza katika bajeti ya mwaka 2013 ili isomwe na mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Ina maana kila siku Watanzania watakuwa wanaambiwa kitu kile kile bila faida yoyote.

REA wanasema, vijiji 726 vitaunganishiwa umeme vikiwamo vya vilaya ya Handeni mkoani Tanga, hasa vile vilivyokuwa na njia ya umeme (underline).

Vijiji hivyo ni Komsala, Kwamatuku, kijiji ambacho najiuliza kimeingiaje kwenye orodha hiyo kwasababu hawa wana umeme, wakati vingine vilivyotajwa ni pamoja na Msasa, Kwedisemi, Kwakiliga, Kwinji na vinginevyo.

Kwanini tunaendelea kuishi kwa porojo? Kwanini tunaipa hasara serikali na kupalilia ugumu kwa Watanzania?

Ndio maana nasema, REA, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TANESCO wapeleke umeme katika vijiji hivi kabla ya wananchi hawajaichukia serikali yao.

Kama kweli fedha hakuna, pia wasitumie gharama kubwa kutangaza vitu visivyokuwa na msingi. Fedha hizo zihamishiwe katika miradi ya maendeleo ikiwamo umeme vijiji ili kuyakomboa maisha yao.

Makala yangu hayakuwa na nia ya kuwaharibia bali kuwakumbusha wajibu wao. Naamini serikali ina viongozi makini pamoja na uwezo wa Waziri wa Nishati na Madini mwenye mipango madhubuti.

Itakuwa safi kama vijiji vilivyotajwa na REA kuwa vitapata umeme, kero hiyo itatuliwe kabla ya bajeti ya mwaka ujao ili serikali iangalie lingine.

Huo ndio ukweli. Vinginevyo, tutakuwa watu wa kupiga stori bila faida yoyote. Jamii itatucheka. Viongozi wetu hawatakuwa na heshima mbele za jamii.

Hata Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete ataonekana hana lolote kwasababu ya kuangushwa na watu wake, wakiwamo REA na TANESCO.

Namaliza kwa kusema, uongozi bora ni kufanyia kazi dosari zetu, kukubali maoni ya wadau ili tusonge mbele na sio kufanya mambo kinyume.

Vinginevyo porojo zetu, hadithi zetu zitatubakisha hapa tulipo, huku baadhi yao wakibuni njia za kula ikiwamo kusainisha matangazo yasiyokuwa na kichwa wala miguu, kwakuwa wamekosolewa.

Mbaya zaidi matangazo yanapelekwa mahali pasipoibuliwa hoja hiyo, hivyo hata wale waliosoma mwanzo majibu hawayapati.

Hilo linashangaza uamuzi wa watendaji wetu wakati mwingine kukimbia kivuli chao, wakati siku zote mkubwa akivukwa na nguo huchutama.

Mabadiliko ni lazima. Nafasi zenu zilete tija kwa Watanzania wanaoishi kwa kuwategemea uwepo wenu.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment