Pages

Pages

Wednesday, December 12, 2012

DC Handeni azindua ufyatuaji wa matofali ya madarasa Kwamsisi


Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu mwenye miwani, akichanganya udongo katika ufyatuaji wa matofali.

Na Kambi Mbwana, Handeni
MKUU wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, amezindua ufyatuaji wa matofali katika Shule ya Msingi Kwedikabu, yenye wanafunzi 540, huku ikiwa na vyumba viwili vya madarasa na kusababisha idadi kubwa kusomea nje.
 
Uzinduaji huo aliufanya mwishoni mwa wiki akiwa na wananchi wengi katika kijiji hicho kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kwa umoja na kuweza kuwakomboa wanafunzi wa shule hiyo yenye changamoto nyingi, ikiwamo ya kosomea nje.
 
 Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, kushoto akizungumza na wanakijiji wa Kwedikabu, baada ya kuzindua ufyatuaji wa matofali wa shule ya kijiji hicho.

Akizungumza katika uzinduaji huo shuleni hapo, Mkuu wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema shule ni mali ya watu wote, hivyo wananchi wanatakiwa wachangie kwa hali na mali ili watoto wao wasomee sehemu nzuri.
 
Alisema kuamua yeye kuingia katika shimo la tope na kuponda udongo ni kuonyesha kuwa kazi hiyo inahitaji ushirikiano na kufanya kazi kwa moyo wote, ukizingatia kwamba watoto wao wanasomea nje huku wazazi wao wakiangalia kwa macho.
 
“Hatuwezi kwenda hivi kwa kuangalia watoto wakisomea nje wakati wazazi tupo, ndio maana nimekuja kwa ajili ya kushiriki kikamilifu ufyatuaji wa matofali haya, nikijua pia shughuli hii itaendelea wakati wote.
 
“Kijiji kinaingia aibu, maana watoto wao wanasomea nje na kushuhudia utoro mwingi, maana kipindi cha mvua, hakuna motto anayekubali aende shule akapigwe na mvua, badala yake kuamua kulala tu nyumbani,” alisema Rweyemamu.
 
Mbali na ufyatuaji wa matofali, DC Muhingo pia ameitumia fursa hiyo kuzungumza na wananchi juu ya umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano, sambamba na kuwa makini na ardhi yao inayowaniwa na watu wenye nia ya kujineemesha kwa kuwalaghai na  visenti vya kula.
 

No comments:

Post a Comment