Pages

Pages

Wednesday, December 12, 2012

Tunaacha ya maana, tunajadili sare za CCM na Nyerere



 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, enzi za uhai wake.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NAFIKIRI akili zetu zina matege. Matege yanayofanya tuwaze hata yale yasiyokuwa na tija kwa maisha yetu, katika kipindi hiki ambacho gharama za maisha zimezidi kuwa juu kupita kiasi, huku masikini wakizidi kuwa kwenye wakati mgumu.

Katika Tanzania ya leo inayokabiriwa na upepo wa kisiasa, baadhi yao wamekuwa wakikaa na kubuni propaganda zisizokuwa na mashiko siku hadi siku. Huu ni ujinga, hasa ukiwazwa kwa muda mrefu bila sababu za msingi.

Kwanini nasema hivi. Kuna watu wamekuwa wakikaa chini na kuandika vitu ambavyo ukivifikiria mwanzo na mwisho wake unabaki unacheka. Kama sio kucheka, unajiuliza, hivi mawazo haya yanawazwa kwa faida gani?

Kwa wiki moja sasa baadhi ya watu wamekuwa wakitoa swali linalomhusu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Swali linahoji endapo kuna picha inayoonyesha kuwa Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kuvaa jezi za Chama cha Mapinduzi, huku yeye akiwa ni mwenyekiti hadi kuja kuwa Rais wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 20.

Hata mimi niliulizwa swali hilo. Lakini aliyeniuliza na mimi nikampa swali la kufana na hilo. Nilimwambia baada ya kujua Nyerere aliwahi kuvaa jezi za CCM au hajavaa Taifa hili litavuna kitu gani kwa kutokana na swali hilo?

Hata kama kweli mtu huyo anasema zawadi nono itatolewa endapo nitamfikishia picha ya Nyerere juu ya maisha yake na namna gani alikuwa mwenyekiti bila kuvaa jezi za chama chake, ingawa huo ni utaratibu wa kawaida kwenye siasa.

Kwa kuliangalia suala hilo, nadhani baadhi ya Watanzania upeo wao wa kufikiria namna ya kujikomboa kimaisha umefikia mwisho na badala yake unawaza vitu ambavyo kwa kawaida havina umuhimu wowote.

Zaidi utapoteza muda wa Watanzania hata wale wanaofanya kazi na kukuza uchumi wao, maana wanaingizwa katika kuwaza upuzi usiokuwa na umuhimu wowote. Hali kama hiyo imekuwa ikitokea mara kwa mara.

Ilishawahi kuandaliwa propaganda ya kuhesabiwa watoto wa vigogo waliongia katika uongozi wa chama tawala, wakidai ni mbaya kwao. Eti wamekifanya chama kiwe cha kindugu wakisema pia Watanzania wachukizwe na suala hilo.

Hawa nawaita kuwa daima mawazo yao ni kuchafua watu. Katika kuchafua huko, hawaangalii umuhimu wala hadhi ya wanayetaka kumchafua. Ndio maana imekuwa kawaida sasa kuamka asubuhi na kukuta habari za kuchefua.

Kwa bahati mbaya, wanaowaza haya wengi kati yao wana ndoto za kugombea au ni viongozi katika Taifa hili lenye changamoto nyingi. Watu hawawazi namna ya kujikomboa kimaisha kwa kutumia fursa zinazopatikana.

Wakitoka kuwaza jezi za Nyerere, hurudi kwenye malalamiko ya uhaba wa ajira au maisha magumu yanayowasumbua Watanzania. Hatuwezi kwenda hivi. Wenye mtazamo wa aina hii, hata kama wana elimu kubwa, lazima tuwe na mashaka nao.

Hivi ni kweli kuvaa au kutowahi luvaa sare za chama ni hoja kwa kizazi cha leo? Tutapata nini? Njaa zetu, shida ya maji katika baadhi ya maeneo zitatoka kama jibu linalotafutwa na wana propaganda litapatikana?

Wewe daktari unayewaza haya ndio faida yako ya kukaa darasani kwa miaka mingi kutafuta namna ya kuwatumikia binadamu wenzako? Wewe mfanyabiashara na wengine wa kada hii, sare za CCM ndio kila kitu katika majukumu yako?

Nadhani ifikie wakati tuseme basi. Mada za kupotoshana, zisizokuwa na mashiko kwa Watanzania zikome pale tu zinapobuniwa na wanapropaganda. Kuna mengi ya kulifanyia Taifa hili. Wasomi na wanasiasa wote walione hilo kwa kulipatia ufumbuzi.

Ni ujinga anyejiona ni msomi huku elimu yake ikiwa haina faida kwake na kwa Taifa lake. Elimu zetu, uelewa wetu uwe na faida. Kuwaza hata yale yasiyokuwa na faida ni uhaba wa fikra katika vichwa vyetu.

Nilidhani Watanzania tutamuombea dua Mwalimu Nyerere kwa kukumbuka fadhira zake, mchango wake katika Taifa hili. Amelifanyia mambo mengi mazuri. Amewafanya Watanzania waishi kwa amani na upendo na ushirikiano wa makabila zaidi ya 120 nchi nzima.

Kwa sababu hiyo, hakuna haja ya kutafuta mabaya kwa ajili ya kumdhalilisha au kuidharau serikali na chama alichokiongoza katika harakati za kutawala nchi yetu.

Huu ndio ukweli. Tunapaswa kuufikiria kwa kina na faida yetu. Yoyote anayetaka kuhoji sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya Mwalimu Nyerere, ajiangalie faida yake akipata ukweli, hasa kama alichokihitaji amekipata.

Kuna watu ambao wanajidanganya kwamba kubuni propaganda zisizokuwa na faida kwao ni kukiharibia chama tawala. Wanashindwa kujua kwamba, sio kila mmoja anaabubu sare za vyama vya siasa.

Watu wanataka utendaji bora na wenye faida na sio kujadili kwamba Jakaya Mrisho Kikwete, Benjamini William Mkapa na viongozi wengine wa chama na serikali kama waliwahi kuvaa au hawawezi kuvaa nguo za CCM.

Katika kuliangalia hili, ofisi za CCM zipo wazi katika kila Mkoa. Mtu mwenye kutaka kujua maswali hayo, aende kuuliza au kuonyeswa, lakini pia akajiuliza kama njaa yake, umaskini wake na wa familia yake utakwisha.

Sidhani kama kweli nikijua kuwa Nyerere alivaa au hajawahi kuvaa sare za CCM kipato changu kitaongezeka. Zaidi nitaongeza mawazo ya kuwaza mengine yasiyokuwa na tija, maana siku zote mwisho wa safari moja huanzisha na nyingine.

Watanzania tuachwe kuaminishwa uongo. Tusikubali kabisa kupotoshwa au kupewa mzigo wa kufikiria sare za vyama vya siasa. Badala yake tukubali kuhoji namna ya utendaji kazi wenye maslahi na Taifa lote.

Badala ya kuhoji sare za vyama vya siasa, Watanzania tuwaweke kitimoto viongozi wetu kuanzia serikali za mitaa, vijiji, kata na wilaya kwa ajili ya kuangalia utendaji kazi wao na mipango ya kufanikisha maisha bora.

Ndio tumepewa macho ya kuona na kusikia. Lakini tusikubali kusikia hata vile visivyopendeza kusikiwa na masikio yetu. Wanaofanya hivyo wanajua kuwa baada ya kuwajaza ujinga, mtataka kuchukua hatua.

Siku zote, raha ya propaganda ni ile inayofanikiwa na kuaminiwa na watu, hata kama haina faida kwa Watanzania. Kwa hali inavyoendelea, tujiandae kusikia mengi, maana kutokana na harakati za kisiasa, kila mmoja anafanya anavyojua mwenyewe.

Hata hivyo, nadhani viongozi wa vyama hivyo vya siasa vinapaswa kukaa chini na kuangalia maono au mipango yao kisiasa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Katibu Mkuu wake, Wilbroad Slaa wanapaswa kuwaambia watu wao namna ya kuhoji vitu vyenye faida na sio kupoteza muda kuwaza sare za vyama vya siasa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wengine wa chama hicho wanapaswa kushirikiana na serikali iliyokuwapo madarakani kwa ajili ya kuwapatia maisha bora Watanzania na sio kutaka waulizane sare za mwasisi wa CCM, Mwalimu Nyerere aliyetangulia mbele ya haki.

Kwa bahati mbaya, harakati kama hizi za kuaminishwa uongo, vijana ndio waathirika wakubwa, maana ni wepesi kuchukua yanayosemwa na kuwasambazia wengine. Huu ni ujinga na inashangaza unavyozidi kusambazwa na baadhi yao.

Huu ndio ukweli. Ukweli ninaopenda uangaliwe upya na sio kila linalosemwa au kuandikwa na wenye jukumu la kutunga propaganda hata zile zisizokuwa na faida kwa Taifa hili, ambalo gharama za maisha zimezidi kupanda juu zaidi.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

1 comment:

  1. Mbona unaruka swali kaka?
    Maneno mengi ya nini, rusha hiyo picha.

    Inaonekana ni kweli ndio maana Umekuja na maneno kibao.

    ReplyDelete