Pages

Pages

Wednesday, October 17, 2012

Mwanaharakati haogopi jina la kigogo


MGODI UNAOTEMBEA

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WASWAHILI ni wajuzi sana wa maneno. Katika kipindi cha maisha yao, walijikita katika kubuni misemo ambayo mingi kati yao imekuwa na mashiko wakati wote. Hata kama ukiishiwa nguvu, lakini ukiumbuka mmoja wapo, nguvu za ziada huibuka.

                                          Mwasisi wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere
Angalia msemo huu. Kwenye nia pana njia. Msemo huu unatufundisha kuwa chochote tunachohitaji kufanya, lazima tuweke nia maana itazalisha njia ya kufanikisha dhamira hiyo kwa kila binadamu anayeandamwa na vikwazo.
                                          Ridhiwan Kikwete
Mwenda pole hajikwai. Msemo huu unatufundisha kufanya kazi zetu kwa utulivu bila kuacha papara, ndio maana hapo pia ukatungwa msemo mwingine wa haraka haraka haina baraka.

Sio lengo langu kuoredhesha misemo ya wahenga, maana ni mingi na haiwezi kujaa kwenye ukurasa wote huu wa Mgodi Unaotembea. Lengo langu ni kuwambusha Watanzania juu ya mabadiliko ya kisiasa na wale wanaojiita ni wanaharakati.

Wanaharakati ambao baadhi yao ni watunga uongo na uzandiki bila ukomo. Wanaharakati wa Tanzania, wengi wao wanapotunga hasidi zao, wanashindwa kuupangilia ili uonakane una ukweli japo kwa asilimia chache.

Kwa wiki kadhaa sasa kumekuwa na maoni mbalimbali ya juu ya uchaguzi wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Uchaguzi huo umebadilisha hisia za wanaharakati na kuanza kuleta porojo mahali ambako si mahali sahihi.

Watu hao wanahoji uhalali wa watoto wa vigogo kuingia kwa wingi katika uchaguzi huo. Ati wameihodhi CCM na kuifanya ya kindugu. Hapo yanasemwa maneno mengi, akitajwa Rdhiwan Kikwete, kama mfano wa wanachama hao.

Wanaharakati hao waliandika meseji na kutuma kwa kila wanayehisi kuwa hajaelewa somo la mabadiliko yasiyojengwa kwa hoja na watu hao.

"HATARI: Angalia watoto wa vigogo waliopita UVCCM ngazi ya Taifa; Dickson Membe, Fredy Lowassa, Ridhiwani Kikwete, Ashura Hussein Mwinyi, Beny Samuel Sitta, Debora Mwandosya, Irene Pinda, Felister Ndugai, Chrisopher Ndejembi, Sharifa Bilali, Hawa Kigoda, Judith Mukama, na Jerome Msekwa.

“Nchi imekwisha, inatia hasira, wacha watoto wa masikini tupambane kupitia mlango mwingine, "CHADEMA" ili kutetea masikini wenzetu, wazazi na wadogo zetu. Vita hii inaanza sasa upatapo meseji hii tuma kwa wazalendo wenzako,” mwisho wa ujumbe huo na kumalizia kuwa aliyetuma meseji hiyo ati ni mwanaharakati.

Hizi ni meseji za kijinga mno. Na wenye akili timamu hawawezi kubabaishwa nazo, maana zimebuniwa kwa nia ya kujiridhisha kuwa utakaowaingia wanaweza kuwaelewa, hata kama sababu zao ni ndogo mno.

Kwanini nasema hivi? Kwangu mimi siwezi kubabaishwa na jina la mtoto wa kigogo katika sehemu husika, kama lengo langu ni kugombea mahali Fulani. Tena ndio kwanza naona raha juu ya kupambana na mtu huyo.

Mtoto wa kigogo hakatazwi kuwa mwana CCM kama walivyokuwa wapinzani na kushika nafasi mbalimbali za vyama vyao. Ila sitamuelewa mtoto wa kigogo nitakapobaini kuwa anakwenda kinyume au ni mwizi.

Yani, anatumia nafasi yake vibaya kwa ajili ya kujitajirisha mwenyewe. Sina ugomvi na Ridhiwan ati kwasababu ameamua kuchukua fomu za kuwania ujumbe wa CCM. Kila mmoja ana haki na wajibu sawa wa kuchagua na kuchaguliwa.

Naandika makala haya kama mwanzo wa kuwaelimisha hao wanaharakati na wasiokuwa wanaharakati juu ya kutetea wanachokiamini. Hakuna haja ya kubabaishwa na jina la mtoto wa kigogo hata kama tunajua ghiriba inaweza kufanywa wakati wowote.

Tangu uchaguzi huo wa CCM ulipoanza kutimua vumbi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, majina mapya nay a zamani yameingia. Tena, wapo ambao hawakutarajiwa lakini hatimae wameibuka na ushindi.

Unaotakiwa kujengwa ni ujasiri na kujituma hadi mwisho wake. Lolote kwenye uchaguzi linaweza kutokea na sio kulalama kuwa ni wengi watoto wa vigogo.

Mjini Nachingwea, kijana wa kidato cha sita, Fadhili Liwaka ameweza kumuangusha Waziri wa Sheria na Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mathias Chikawe katika uchaguzi wa CCM.

Hawa walikuwa wanawania nafasi moja ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nachingwea mkoani Mtwara, huku matokeo hayo yakishangaza wengi. Chikawe mwenyewe hakujua kwamba angeweza kuangushwa na kijana huyo.

Kama Liwaka angekuwa mwoga kama wanavyowaaminisha hawa wanaharakati, sidhani kama angekuwa na ujasili wa kupambana na kigogo huyo wa Serikali ya Jakaya Mrisho Kikwete, ukizingatia kuwa ana nafasi kubwa.

Kwa bahati mbaya, mbinu inayoganywa na wapinzani ni kueneza sumu hata zile ambazo hazina kichwa wala miguu. Kukaa na kufikiria haya ni kuishiwa hoja. Wangapi wanarithi kazi za wazazi wao na bado halisemwi?

Mbona wapo wazazi madaktari na watoto wao nao wanaingia kwenye sekta hiyo? Wangapi ni walimu na watoto wao ni walimu? Au wanaharakati wanaona kwenye siasa tu? Hizi ni sababu zisizokuwa na mashiko hata kidogo.

Nitawaona wanaharakati wana akili timamu watakapowajengea uwezo wa kupambana na majina hayo na sio kuwaaminisha kushindwa. Mwanaharakati makini ni yule anayepanga kila mbinu kuweza kukabili vishindo hivyo.

Tena, haya majina yanayooogopwa ni ya kawaida kabisa. Mtu unaweza kujieleza vizuri na bado mtoto wa Kikwete, Mwinyi wakakosa nafasi hiyo. Hata kama wakipata leo, lakini uchaguzi utakaofuata watashindwa tu.

Kikwete ndio kipindi chake cha mwisho hiki. Huenda kama uwepo wake umewafanya watoto wake wapewe nafasi basi wakaikosa katika uchaguzi ujao. CCM sio mali ya mtu mmoja. CCM ni mali ya kila mmoja.

Ila kinachofanywa ni kupeana zamu katika nafasi hizo, maana wote hawawezi kuwa viongozi wa chama na serikali. Ili mmoja wao apewe nafasi, ni lazima awashawishi wajumbe ili wampigie kura.

Huo ndio ukweli. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa makini katika nyendo zake na harakati zenye ushawishi na dhamira za kweli. Wapambanaji wasiamgalie nani ni mtoto wa kigogo au nani wa mkulima, maana wote wana haki sawa.

Wasiamgalie jina la mtoto wa Kigoda na wengine. Na kama huo ndio utaratibu wao, basi unapaswa kukoma kama lengo lao ni kukipa nguvu chama chao na sio kuendeshwa ovyo kisa watu Fulani wanataka mabadiliko ya kisiasa.

Sio kila tunaloambiwa na wanaharati tunataka kuliweka kichwani, maana hakika mengine hayana kichwa wala miguu. Mwanaharakati anataka kuwakomboa watu wake, lakini bado anawaaminisha kuwa hakuna linaloweza kufanikiwa kama vigogo wataachwa watoto wao.

Wanasahau kuwa wapo vigogo ambao nao wanahitaji nafasi hizo za chama nab ado wanakosa baada ya kuangushwa kwenye chaguzi hizo. Nakerwa sana na mwenendo huo. Mtu aliyenitumia meseji hiyo nilimlaumu kupita kiasi.

Akili yake huenda ina matege. Anafanya siasa nyepesi ama rahisi. Haina tija kwake na Taifa kwa ujumla. Kwa bahati mbaya, akiambiwa ukweli mtu wa aina hiyo, atawaka kwa hasira. Atajiona yeye ndio kila kitu, wakati sio mkweli.

Atajiita yeye ni mjuzi wa kila jambo akilingia vyeti vyake ambavyo huenda amevipata kwa ujanja ujanja kama wafanyavyo baadhi yao. Hapana. Huu sio mwendo sahihi na lazima Watanzania na wale wanaharakati wajifanyie mabadiliko.

Huwa simpendi mtu asiyejiamini. Mtu ninayempenda ni yule anayeona anaweza kupata kile anachotaka hata kama kuna vizingiti vya kila aina. Hayo ndio maisha mazuri. Katika hilo, nami najifunza kuacha woga katika kile ninachokitaka na kukiamini.

Mawazo haya yaenee kwa kila mmoja wetu. Tusiangalie vigogo waliopo kwenye Chama tawala CCM, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na wengineo maana siku zote kwenye ukweli uongo hujitenga.

Baada ya kusema hayo, naomba nikuage msomaji wangu wa Mgodi Unaotembea na tukutane tena wiki ijayo katika dhmira ya kweli ya kujenga nchi kwa kushirikiana sote bila kuangalia nani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi au CCM.

Ndugu msomaji wangu mpendwa. Sasa unaweza kujadili na mimi mambo mbali ya kisiasa katika group la Handeni Kwetu, ambao ni uwanja mpana zaidi, baada ya huu Mgodi Unaotembea unaotoka kila Jumatano katika Gazeti lako la Mtanzania.

Ndudu msomaji wangu mpendwa. Sasa tunaweza kukutana katika uwanja mpana zaidi, kwenye group la face book linaloitwa Handeni Kwetu na kuchambua mambo mbalimbali ya kisiasa, kimichezo na kiutamaduni na naomba uwe pamoja nami.
 
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment