Pages

Pages

Monday, October 15, 2012


BABA WA TAIFA

Nyerere asingekufa kwa maradhi, angeuliwa na CCM

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
LEO ni Oktoba 14. Tanzania nzima inaingia katika kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekufa Oktoba 14, mwaka 1999 nchini Uingereza alipokwenda kwa matibabu.

Kwa mujibu wa madaktari wake, Nyerere mtu muhimu kabisa katika Taifa hili, alikufa kwa maradhi ya kansa ya damu (leukemia), akiwa katika harakati nyingi za kuokolewa maisha yake, katika Hospitali ya St Thomas, London, Uingereza.

                                         Mwalimu Julius Nyerere
Kifo chake kilitetemesha wengi, wakiwamo wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wale wasiokuwa na vyama vya siasa. Katika kuiangalia kumbukumbu yake, naweza kusema kifo chake kitaendelea kuwa pigo hasa kwa CCM.

Chama ambacho licha ya kukipenda na kukiheshimu kupita kiasi, kimegeuzwa na wachache wao, walioamua kuja kufanya biashara kwa mgongo wa kisiasa.

Nathubutu kusema kwamba, uhakika wa kuendelea kuishi kwa baba wa Taifa, ungekuwa mdogo mno kwa mwenendo wa CCM kuanzia miaka ya 2000 hadi muda huu.

Kama asingeshikwa na maradhi hayo, basi ni dhahiri msiba huo ungekuwamba, huku sababu kubwa ikiwa siasa chafu, rushwa ya uchaguzi, hasa ndani ya CCM, sambamba na siasa za makundi na kushughulikiana wao kwa wao.

Nyerere, asingeweza kudumu, maana watu anaowaamini wanageuka na kuvaa joho la ukatili, wakiwa ndani ya chama kilichounganisha watu wengi. Chama ambacho kwa namna moja ama nyingine, kimeundwa kwa jasho la walalahoi.

Watu ambao kwa miaka 35 sasa, maisha yao, uhuru wao ni mdogo mbele ya matajiri wachache wanaoingia kulangua kwenye siasa. Kwanini nasema hivyo. Nyerere kwa mtazamo wake, alisema bila CCM nchi hii itayumba.

Aliyasema haya kwa imani kubwa aliyokuwa nayo kwa Watanzania na  mbele ya chama chake hicho cha CCM, ambacho kwa sasa kipo chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Mrisho Kikwete.

Hali ya mambo inavyoendelea, uwezekano wa CCM kutawala milele ni mdogo mno. Kumekuwa na mabadiliko makubwa ya upepo wa kisiasa. Chuki za wazi wazi ndani ya uongozi wa chama hicho kikongwe zimetamalaki.

Uhai wake ungekuwa mdogo mno. Watu wanageuka na kufanya siasa zisizokuwa na tija kwa CCM na bado wanachekewa. Wenye maono yao wanatembea na kusema vibaya juu ya kauli za Nyerere, wakisema hazitakiwi kufuatwa.

Kinachofuata sasa ni kuona kejeli za wazi wazi kwa baba wa Taifa, maana waliobakia kwenye mfumo wa chama, hawana mawazo mazuri ya kukitetea chama mbele ya umati wa watu wanaona kwamba chama kimezeeka na kinatakiwa kufa.

Wale ambao wanatembea kwa matao wakisema kifo rasmi cha CCM ni mwaka 2015. Wanasema kaburi lake limeshaandaliwa. Hizi ni kejeli ambazo nachelea kusema kuwa zingemfurahisha Nyerere, hata kama leo angekuwa hai.

Hizo tu na nyingine nyingi zingempa presha na jaka moyo, hivyo uhai wake kuwa mdogo mno. Kama huo sio ukweli, basi upo mbali na uongo. Nikiwa kama Mtanzania, naheshimu kwa dhati mchango wa Baba wa Taifa.

Amefanya mengi mazuri, ikiwamo kuruhusu kwa kauli moja mfumo wa vyama vingi vya siasa, kama ishara nzuri ya kukua kwa Demokrasia ndani ya nchi hii ambayo kwa sasa inaendelea kutafunwa na mchwa aliowasema.

Mchwa hao wamekuwa wakijenga mtandao wao kwa njia za hatari mno. Wengine wanafika mbali kwa kuingia ubia na wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kuitafuna nchi hii.

Watanzania masikini hawana haki tena. Kila kinachofanyika ni usanii mtupu. Bado tu hiyo suio dalili za kuangamiza roho za wapendwa wetu? Je, Nyerere angechekea haya yanayofanyika sasa, ikiwamo fedha kutumika nyingi hata kwenye chaguzi za ndani?

Wanataka nini? Mgombea kumwaga noti katika Uchaguzi wa Umoja wa Vijana CCM, (UVCCM) anatafuna nini? Fedha hizo anazitoa wapi na ili apate nini? Chama kimehamshwa kutoka kwa wakulima na wafanyakazi na kuingia kwenye mikono ya walanguzi, wafanyabiashara wakubwa wenye malengo yao kisiasa.

Ukifanya hesabu za wafanyabiashara wakubwa wanaoingia kwenye siasa utachoka. Ni wengi mno. Kila mtu humo ni mwanasiasa na mgongo wake ni CCM. Hao ndio wanaoharibu mfumo mzima wa CCM, ingawa wakiambiwa watabisha.

Tuambiane ukweli hata utatuuma. Tusidanganye kuwa tunamuenzi Nyerere wakati mambo yanaendeshwa kienyeji na wajanja wachache wananufaika. Huo ndio ukweli wa mambo.

Kila mmoja awe na nia ya kuwakomboa Watanzania wenzake kwa kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana na rasilimali zilizopo. Kama madini yetu yanachimbwa na sisi kuambulia mashimo, bado tunamuenzi Nyerere?

Kama wazee wetu wasiokuwa na elimu waliwabaini wajanja, watumia nguvu zao vibaya, wakoloni na kuwatimua, vipi wasomi wa leo wanawaingiza kwa mgongo wa uwekezaji?

Elimu yao ipo wapi na inatumika vipi kuwakomboa watu wote. Hili lazima lisemwe hadharani kwa ajili ya kujenga haki ya kila mwananchi. Tanzania hii sio ya watu wachache wanaonufaika na familia zao, huku walalahoi wakiendelea kushinda njaa.

Kwa bahati mbaya, haya yanatokea wakati serikali ipo chini ya CCM, chama ambacho mwasisi wake, Nyerere alikitabiria kutawala milele kwa kusema bila hicho nchi itayumba. Kama hivyo ni kweli, ina maana Rais huyo wa Kwanza wa Tanzania, hajajua kuwa kuna siku hali itakuwa mbaya kwa chama chake.

Kwa wataalamu wa mambo ya siasa wanajua kuwa bila chama cha Mapinduzi chini ya Kikwete kukaa na kuangalia tatizo, uwezekano wa kushinda katika chaguzi tatu zijazo, yani mwaka 2015, mwaka 2020 na 2025 ni mdogo mno.

Na hilo likitokea, basi damu nyingi itamwagika kama inavyomwagika sasa, maana wenye nia ya kutawala wamekuwa wakipakaza sumu na kushitaki kwa nguvu ya umma (wananchi), wakisema CCM imeshindwa kuwakomboa Watanzania kwa kuwaacha kwenye madhira ya umasikini huku viongozi wao wakila raha na familia zao.

Nadhani kwa kupitia kumbukumbu ya kifo cha mwalimu Nyerere, Watanzania na viongozi wa Taifa hili, wakiwamo wana CCM wana kila sababu ya kujitazama upya kama kweli wanahitaji kumuenzi mwenyekiti wao wa zamani.

Wafanyie kazi ushauri wake, uongozi wake na sera zake zilizotukuka badala ya kusema kwenye vijiwe vya siasa, wakati chama chao kinayumba. Kuna mchambuzi mmoja, aliwahi kuandika katika makala yake, Nyerere akifufuka leo anakufa tena.

Najaribu kuyaelewa mawazo yake, maana akifufuka leo, atakuta CCM mpya yenye kila aina ya uozo, huku dalili za kubaki madarakani kwa miaka mingi ijayo ikikosekana, kama hali itaendelea kuwa kama ilivyokuwa sasa.

Wakati ni huu. Bado CCM imara, Taifa imara linawezekana kwa kuangalia makosa yao, mapungufu yao kwa ajili ya kusonga mbele na sio kurudi nyuma wala kubaki lilipo.

Mungu ibariki Tanzania.

0712 053949
0753 806087

Mwisho


No comments:

Post a Comment