Pages

Pages

Wednesday, October 17, 2012

Mabondia kufanya mazoezi pamoja Jumamosi

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MABONDIA mbalimbali wa uzito wa juu hapa nchini, wanatarajia kukutanishwa Jumamosi na kufanya mazoezi ya pamoja, huku wakishuhudiwa na mmoja wa wafadhili wa Evender Hollfied, Andrew Jowel.

Kufanya mazoezi kwa pamoja ni sehemu ya kufanya mchakato wa kujitafutia mafanikio makubwa katika sekta ya masumbwi na kuinua kiwango cha mchezo huo hapa nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, muandaaji wa tukio hilo, ambaye pia ni bondia mahiri hapa nchini, Japhet Kaseba, alisema lengo ni kutathimini namna ya kuendeleza mchezo wa masumbwi Tanzania.

                                          Japhet Kaseba 
Alisema anaamini mabondia watakaofika siku hiyo katika kambi ya ngumi ya Kaseba, iliyopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam watakuwa na mwamko zaidi wa kufikia malengo yao.

“Tayari mabondia mbalimbali wanajua kuwa tutakuwa na mgeni huyo aliyekuja kutembelea Tanzania, huku akiwa anajua mambo mengi yanayohusu mchezo wa masumbwi duniani.

“Kuanzia saa tisa alasiri, mabondia wote tutaanza mazoezi ya pamoja katika gym yangu, hivyo kila anayependa kushiriki afike maana lengo ni kuangalia namna ya kujitangaza na kuonyesha kwamba Tanzania wapo mabondia wenye vipaji na dhamira ya kweli ya kufika mbali,” alisema Kaseba.

Kaseba ni miongoni mwa mabondia wenye mafanikio makubwa katika mchezo wa masumbwi, huku akiogopwa na mabondia wakali wanaoshindwa kucheza naye kila anapojitokeza promota wa kumkutanisha nyota huyo ambaye pia aliwahi kuwa bingwa wa Dunia wa Kick Boxing.

No comments:

Post a Comment