Pages

Pages

Tuesday, October 30, 2012

Waigizaji waanzie kwenye makundi

                            Wema Sepetu, msanii wa filamu Tanzania
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KWA wasanii wa maigizo, wanafahamu namna gani makundi yanavyoweza kuwaibua na kuwapa vipaji halisi, kuliko wale wanaoingia kwenye sanaa kwasababu ya mwonekano wao, mvuto wao wa sura au uwezo wa kuzungumza lugha ya Kingereza.

Hata kama uwe na mvuto wa kiasi gani, lakini uwezo wako utazidi kuimarika endapo utapata nafasi ya kufanya mazoezi na vikundi vya sanaa vinavyofundisha sanaa ya ukweli. Kwanini nasema hivyo?

                          Jacob Steven (JB) mkali wa filamu Tanzania
Wasanii waliobukia kwa miaka miwili hii, wengi wao wamekutwa klabu wakinywa pombe au vileo vingine na kuombwa washiriki kwenye filamu zao. Kwa makubaliano wanayojua wenyewe, wasanii hao hupewa (Script) maneno yanayoandikwa kwenye karatasi kwa ajili ya kuzungumzwa na yule anayetakiwa kupigwa picha.

Akishafanya hivyo, masuala mazima ya kurekodi filamu hiyo huanza kwa kutafuta (location) maeneo ya kupigia picha yao, kabla ya miezi miwili baadaye filamu hiyo kutangazwa eti tayari imeshakamilika.

                   Wolper akionyesha mvuto wake mbele ya kamera
Msanii wa aina hiyo siyo tu anasumbua katika filamu zake kwa kutovaa uhusika wa kweli, bali pia hukosa maadili na namna gani ya kujiweka katika kundi la wasanii muhimu wa Tanzania, huku pia akikosa kufahamu mbinu za uigizaji.

Msanii wa aina hiyo, kamwe hawezi kufahamu kuigiza jukwaani, wenyewe wanaita (Stage Drama). Ingawa wasanii walio wengi hawawezi sanaa ya aina hii maana ni ngumu, lakini sio kweli kama watakuwa hawajui taratibu za uigizaji huo.

Sitaki kuamini kuwa wasanii waliopitia kwenye makundi hawajui jinsi ya kuigiza jukwaani huku mwiko wa kwanza wa kutowapa mgongo watu wete ukumbini humo akitakiwa kuzingatiwa kwa ajili ya kuonyesha umahiri wao.

                     Mkali mwingine wa filamu, Aunt EZEKIEL
Atakuwa anajua tu. Lakini sio wasanii wa leo. Wasanii hawa wanachoangaliwa wao ni sura zao au wanavyoweza kujikwatua na kuvaa ngozi za wazungu. Mimi sio mtaalamu sana wa sanaa ya maigizo, lakini nafahamu vitu vingi.

Pia naelewa umuhimu wa kuigiza sanaa za majukwaani. Ni nzuri zaidi. Wasanii wa wanaotaka kupewa Script leo wanafahamu lolote? Kama hawajui basi ni wakati wao kutafuta makundi na kupewa sanaa hiyo nzuri.

Wasipende kuigiza kwenye filamu tu. Sanaa hiyo ni nyepesi na kila mtu anajua. Sanaa ya filamu na tamthiliya kwenye luninga ni nyepesi na kila mtu ana uwezo wa kuifanya. Hata kama akishindwa kulia, basi atakamuliwa ndimu ili machozi yatoke.

                        Mkali mwingine wa filamu Tanzania, Irene Uwoya
Lakini sio sanaa ya jukwaani. Nani atakubali kuangalia mtu anakamuliwa ndimu kuonyesha machozi yake jukwaani. Ni wazi hawawezi. Lakini waliokomaa katika sanaa, wakianzia na makundi, walau mbinu hizo watakuwa wanajua.

Msanii aliyebobea katika uigizaji, akianzia kwenye makundi, hawezi kukosa chozi lake hata kwa dakika tatu tu. Lazima alie. Anajua mbinu zote. Namna ya kufanya na mbinu za kuonyesha ukomavu wake kwa wadau wa sanaa.

                             Mrisho Mpoto, msanii wa filamu na muziki wa asili
Nasema haya baada ya kuona sanaa yetu ya maigizo inazidi kupoteza dira ingawa wengi wanaibuka na kujipatia majina makubwa. Hao wote waliokuwa na majina makubwa leo sio wasanii wazuri.

Ukitaka kuamini hilo, wachukuwe ili waonyeshe ukomavu wao kwa kuonyesha sanaa ya jukwaani, ambayo mvuto wake ni mkubwa na inaweza kuwaingizia kipato. Sanaa ya majukwaani ni nzuri na ni ajira tosha kwa wasanii husika.

Kwa mfano, wasanii wa aina hiyo wanaweza kujiunganisha na kufanya maonyesho katika kumbi mbalimbali na watu wakaingia. Kwanini wasiingie? Wema Abraham Sepetu, ambaye kila mtu anamjua kwa urembo wake na jinsi anavyowika katika sanaa nani hatapenda kuingia ukumbini kumuona anavyofanya manjonjo yake.

Lakini ni dhahiri hawezi. Kwanza hata sauti yake ameijenga katika sanaa ya filamu tu na sio jukwaani. Ili aweze lazima kwanza ajitengeneze upya. Kwa kuhakikisha kwamba anaweza kufanya sanaa za aina zote.

                            Vicent Kigosi, Ray 
Kwa kulijua hilo, kuna kila sababu ya wasanii wetu kupenda kwanza kuanzia chini, kwenye vikundi vya sanaa mitaani kwao. Hata kama wakipata bahati ya kupita moja kwa moja kama walivyotoka wengine, lakini watafute sasa vikundi hivyo.

Vikundi vinaweza kuwafanya wakaishi maisha mazuri zaidi na heshima ya kujiita msanii mzuri anayeweza kubadilika wakati wowote. Kwa mfano, msanii kama vile Mrisho Mpoto, huyu hawezi kufa njaa hata kidogo.

Ni mjuzi wa sanaa za aina hiyo. Na ndio maana anapata safari nyingi za nje ya nchi kwa ajili ya kuonyesha sanaa yake. Nadhani hilo lazima watu walijuwe kwa ajili ya faida yao wenyewe. Naamini bila hivyo, watakuwa wasanii wenye majina makubwa, lakini kiuwezo wa uigizaji wanakuwa wepesi na badiliko lolote linaweza kuwaangusha.

Niwatakie sanaa njema.

0712 053949
0753 806087

UVCCM wamemeza yai la kuchemsha

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

UVCCM wamemeza yai la kuchemsha. Tabu yake ni kwamba, hadi lipasuke tumboni linahitaji kudra za aina yake. Kwa wadudu kama vile kinyonga, nyoka na kenge wanajua jinsi mayai ya kuchemsha yanavyowasumbua viumbe hao.

Kule kwetu kijijini, tulikuwa tunamchemshia mayai nyoka mwenye kawaida ya kuja kula  mayai ya kuku wetu, kama njia ya kumnasa mtegoni.

                                      Mwenyekiti mpya wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis
Lakini anajisumbua. Kwani mayai hayo hayawezi kabisa kupasuka, hivyo kusababisha kifo chake kwa uroho wake. Ndivyo ninavyoifananisha jumuiya ya vijana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), UVCCM.

Jumuiya hiyo wajumbe wake wote wamemeza yai la kuchemsha. Sasa wanahangaika kupasua, jambo ambalo ni aghalabu kutimiza nia yao. Jumuiya hiyo waliingia kwenye uchaguzi wao mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.

Wao kwa ridhaa yao, wamemuweka madarakani Mwenyekiti wao, Sadifa Juma Khamis na Makamu Mwenyekiti Mboni Mhita na wajumbe sita wa NEC, walioshinda katika Uchaguzi huo uliokuwa na joto la aina yake.

Ni upuzi tu. Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, baadhi ya wanachama wa CCM, wanaanza kukataa matokeo au kumpa mwenyekiti wao wa Taifa, Jakaya Mrisho Kikwete saa 24 kutengua matokeo hayo badala ya siku 14 kama kanuzi za chama zinavyojieleza.

Malalamiko yao ni rushwa iliyotumika kwa ajili ya kuwapa ushindi Khamis na Mboni, jambo linalowashangaza wengi. Wanajiuliza, hivi hawa wanaolalamikia rushwa, nao walipokea au walikataa?

Kama waliipokea, wamesahau kila mla cha mwenziwe na chake pia huliwa? Hivi hawa waliopiga kura, walishindwaje kuwakacha wagombea watoa rushwa? Hivi kama kweli rushwa imetumika, watoaji na wapokeaji hawaoni kama wana kesi ya kujibu?

Haya malalamiko ya wapiga kura, wanaosema rushwa imetumika, hawaoni wanajishushia heshima mbele ya jamii, maana hawautaki uamuzi wao? Ngoja niwe mkweli.

Naichukia sana rushwa. Lakini ni zaidi ninavyouchukia unafiki, uzandiki na siasa za mihemko zinazofanywa na baadhi yao. Woliopiga kura UVCCM, wanawezaje kulalamika wakati wao ndio chanzo cha mzozo huo?

Kinacholalamikiwa hapo ni utoaji wa rushwa, ambao siku zote umekuwa ukikemewa na kila mtu, ingawa baadhi yao hawaeleweki kichwa wala mguu.

Hata Kikwete, alizungumzia hilo kwa chaguzi zote za chama hicho, wakiwamo mama zao, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na UVCCM saa chache kabla ya uchaguzi huo.

Ningeweza kukubaliana na UVCCM kama malalamiko yao ni upinduaji wa matokeo, lakini si kura zilizopigwa na kuhesabiwa. Kinachofanywa sasa, ni kukipasua CCM chama hicho kikongwe chenye heshima kubwa mtaani.

Kwanini nasema hivyo? Kama watu wanapita mitaani wakilalamikia rushwa isiyochukuliwa hatua kila siku, hayo ni matusi ya CCM. Hivyo basi, baadhi ya vijana hao kusema kuwa wataandamana au kurudisha kadi nayo ni hujuma ya chama.

Jibu linalokuja hapa, vijana hao wamedhamiria kuiangusha CCM, waliojigamba kwamba wanaipenda na ipo moyoni. Waliosema kuwa watafuata miiko yote ya uongozi wa chama hicho. Waliosema kuwa hawatatoa wala kupokea rushwa.

Waliosema kuwa binadamu wote ni sawa. Huu ni wizi na uongo wa kisiasa. Kila anayetaka kupinga hayo matokeo ya Sadifa na Mboni wajitazame upya. Malalamiko na vilio vyao ni kukipaka matope chama chao.

Kama wao wanasema hivyo, waliokuwa nje ya CCM nao waseme nini? CCM ndio inayoongoza dola, kwanini washindwe kukemea kwa vitendo rushwa kwa kuwakamata watoaji na wapokeaji wanaosemwa mchana na usiku?

Hivi kweli rushwa inayotumika chooni, watu wanashindwaje kuidhibiti? Ndio maana nimesema hapo mwanzo wa makala haya kuwa UVCCM wamemeza yai la kuchemsha. Na kinachofuata sasa ni kukisambaratisha chama chao.

Kitakufa. Mpasuko unaoibuka utakiua chama maana sijaona mwenye dhamira ya kweli ya kuikomboa na kuitetea kwa nguvu zote CCM inayobanwa na ufisadi na uzandiki wa watu wake wenye nyuso mbili kwa wakati mmoja.

Nilijua baada ya uchaguzi huo, kila mtu avunje kundi lake kwa ajili ya kuijenga CCM imara, yenye nguvu na dhamira ya kushinda katika uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015, utakaowakutanisha na vyama vya upinzani vyenye matamanio ya kuongoza dola.

Vyama kama vile Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na vinavyoibuka siku hadi siku hapa nchini.

Wagombea kama vile Ally Salum Hapi, Rashid Simai Msarika, Paul Makonda, bila hata kuleta chokochoko, wangewapa ushirikiano washindi wao, maana ndio demokrasia inayotakiwa iheshimiwe na kila mmoja nchini.

Lakini kwa wafuasi wao kukataa, kulia na kulalala bila aibu, wakisema rushwa imetamalaki ni kujisumbua wenyewe. Hakuna anayewasikiliza. Jamii itawacheka na kuwadharau kwa kiasi kikubwa, ukizingatia wao ndio waliosababisha matokeo hayo.

Wao ndio tatizo na unafiki wao. Umepiga kura mwenyewe kwa kumchagua mtu wako, halafu unabadilika kama kinyonga na kupinga matokeo kama ishara ya kujikomba bila kujua kuwa unatangaza ujuha wako kwake.

Kila aliyeshindwa katika uchaguzi wa UVCCM, lazima ajuwe hakubaliki, hata kama wanakuja baada ya uchaguzi na kukushawishi upinge matokeo hayo, wakisema rushwa imetumika.

Sawa imetumika rushwa. Je, nao walipewa ikawabadilisha mapenzi yao kwako, wakati walikuimbia nyimbo nzuri, kubebeba kwenye kampeni za uwazi, ikiwamo mitandao ya kijamii wakisema wewe ni zaidi ya unaoshindana nao na chumba cha uchaguzi wakakumwaga?

Huo ndio ukweli. UVCCM na watu wote ndani ya CCM wabadilike kwa ajili ya kujenga chama chao kinachoyumbishwa na vyama vya upinzani kwa kuleta amani, mshikamano wa kweli usiyoyumbishwa na chochote.

Kulalama hakujengi. Ufa ni hatari kwa  maisha ya chama, hasa kama watu wana lengo la kuiweka madarakani CCM 2015, ukizingatia kwamba kinachofanyika sasa, sio sahihi na kuja haja ya kuweka mikakati imara kwa watu wote.

Nasema hili kama njia ya kuwafanya wale wenye mtazamo tofauti wajiangalie mara mbili na kukumbuka kuwa wakati anapiga kura, hakushikiwa bastola. Alimpigia kura aliyemhitaji kwa mapenzi yake, hivyo kulalama leo ni ujinga.

Hivyo kulia lia, kujivuta vuta ni dalili kuwa yai la kuchemsha walililomeza linashindwa kupasuka na huenda likasababisha vifo vyao. Kwakuwa wao ni binadamu, kuna njia ya kufanyiwa upasuaji kulitoa yai hilo ili wanusuru maisha yao.

Upasuaji ninaosema mimi ni mazungumzo, maridhiano kuwa waliyoshinda, wamewekwa madarakani na wao wenyewe, hivyo hakuna haja ya kuwachukia, kuwaona vituko katika mitaa yetu, au vikao vyetu tunapokutana.

UVCCM na wote ndani ya CCM wawe kitu kimoja na kuwapa ushirikiano watu waliowachagua na wala sio kuchekea ujinga wao.

UVCCM wajiulize mara mbili, wanawezaje kuwashinda jumuiya kama yao, Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), chini ya John Heche na wengineo wanaoviweka juu vyama vyao vya siasa.

CCM lazima ijuwe nini mustakabali wao. Kuchekea ujinga wa vijana wao wanaopinga matokeo hayo, au kuwanyamazisha na kuwataka wawe kitu kimoja kwa ajili ya kuijenga CCM yenye kuzinduka toka usingizini.

Kuijenga CCM yenye kila zuri la kujivunia mbele ya wanachama wake wapya na wa zamani, ili wavune katika Uchaguzi Mkuu, wakimaliza vita yao ya urais inayoendelea kuwasumbua wenye kujua wana haki ya kuziweka sawa kambi zao.

Nasema hili kwa mapenzi makubwa na siasa za Tanzania, maana kichefuchefu cha vijana kitaendelea na kukiangusha chama chao, wakati wamepiga kura wenyewe na kuwaweka madarakani waliowataka.

Huo ndio ukweli. Ukinichukia kwa makala haya jua wewe ni kati ya wale waliomeza yai la kuchemsha na haliwezi kupasuka kamwe zaidi ya kusababisha kifo chako au chama chako cha siasa, hasa CCM yenye heshima hapa nchini.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087


Thursday, October 25, 2012

Yasome mateso ya mtoto Godfrey John

Veronica, akionyesha sehemu za tumbo za mwanae mwenye matatizo, baada ya kutobolewa tumbo lake ili aweze kujisaidia. Mama huyo anaomba msaada kwa jamii ili aweze kwenda India kufanyiwa upasuaji...


Amezaliwa bila sehemu ya haja kubwa
Ahitaji msaada wa kwenda India


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INAPOTOKEA ndugu au sehemu ya familia yako amezaliwa mtoto akiwa mwenye afya njema, hakika hilo ni jambo la kumshukuru Mungu. Katika hilo, kila mmoja huzaliwa kwa kudra za Manani na kuishi kupo mikononi mwake.

Wengi huzaliwa na mateso ya aina yake. Wanazaliwa wakiwa na matatizo makubwa, jambo linaloweza kukufanya ujiulize maswali mengi juu ya matakwa ya Mungu kumuumba mtoto huyo na kuzaliwa katika hali hiyo.

Katika kuwaza huko, binadamu tunatakiwa tumshukuru yeye aliyeweza kuimba Dunia na kuufanya watu wauone usiku na mchana.

Binadamu pia wanatakiwa wamshukurru yeye maana ndio kila kitu katika Dunia, huku ule msemo usemao hujafa hujaumbika ukitimia, kama sio kwake leo basi kwangu kesho.

Nimelazimika kuanza hivi baada ya kuona mateso ya mtoto Godfrey John, mwenye umri wa mwaka mmoja, aliyezaliwa katika Hospitali ya Mwananyamala, mwaka jana, huku akiwa hana sehemu ya haja kubwa, hivyo kulazimika kuishi kwa tabu.

Mama mzazi wa John, Veronica Lawrant, alizungumza na HANDENI KWETU, juzi kuwa mtoto wake alizaliwa akiwa hana njia hiyo huku madaktari wakishindwa kubaini hilo mapema, hadi baada ya siku tatu, alipoanza kujaa mwili wake.

“Nilishangaa mwanangu anavimba mwili wake ikiwa ni siku chache baada ya kumzaa katika hospitali ya Mwanyamala, nikiwa na matumaini makubwa dhidi yake, nikimshukuru Mungu baada ya kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Hali yake ilinishtua sana, hivyo kuamua kwenda katika hospitali ya Mnazi Mmoja kupata matibabu ya mtoto wangu mpendwa, hata hivyo madaktari nao hawajabaini lolote zaidi ya kunipa dawa ambazo hazikuwa na msaada,” alisema Veronica, mkazi wa Bunju, jijini Dar es Salaam.

Anasema kwamba baada ya kurudi nyumbani, usiku wake mtoto wake alianza kupata haja kubwa kwa njia yam domo, jambo ambalo lilizidi kumuumiza kichwa na kuamua tena kwenda tena katika Hospitali ya Mwanyamala.

Alipofika, alipata bahati ya kupokelewa vyema, ingawa hakukaa zaidi ya kutakiwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi, ikiwa ni baada ya daktari aliyempokea, aliyemjua kwa jina la Dk Isayo, ingawa hakuwa wa watoto, lakini alijua tatizo kwa kumuangalia tu na kumtaka apelekwe usiku huo.

Huku akiwa na masikitiko makubwa, mama huyo anasema alifika Muhimbili saa saba za usiku na kupokelewa vizuri tayari kwa mtoto wake kuanza kuchunguzwa juu ya afya yake, maana mwili wake ulianza kubadilika sambamba na kujisaidia mara kwa mara kwa njia ya mdomoni, hivyo kuibua wasi wasi mkubwa katika maisha yake.

“Dakika chache baada ya kufika, nilifuatwa na daktari akasema kama nipo tayari nitie sahihi kwa ajili ya mtoto wangu kufanyiwa upasuaji wa tumbo, maana waligundua kuwa hana njia ya haja kubwa, jambo linalomfanya ajisaidie kwa mdomoni.

“Sikuwa na la kusema zaidi ya kukubaliana na uamuzi huo, maana nilijua mwanangu atapata ahueni kama sio kupona kabisa, jambo ambalo naweza kusema namshukuru Mungu kwakuwa yeye ndio muweza wa yote,” alisema.

Kwa mujibu wa Veronica, mtoto wake anaweza kupona kabisa kama atapata upasuaji katika hospitali za Nchini India, ukizingatia kuwa madaktari wamemshauri hivyo ili kurudisha hali ya kawaida ya binadamu, juu ya upasuaji wa Jonh.

Anasema huku akijua hata kula yake ni tabu, anajiuliza wapi kwa kupata kiasi cha fedha cha kumpeleka mtoto wake India kwa matibabu zaidi, maana maisha yake kwa sasa yamekuwa magumu kupita kiasi.

Mama huyo mzaliwa wa Kitiongoji cha Buru, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, anasema kwamba mtoto huyo analea peke yake kwa kusaidiwa na baadhi ya Watanzania wanaojitolea walichokuwa nacho.

Baba yake Godfrey (John) alimkataa mtoto huyo siku chache baada ya ujauzito huo na hata alipozaliwa, hasa alipogundua kuwa mtoto wao amezaliwa na matatizo ya kukosa njia ya haja kubwa, hivyo kuishi kwa mashaka makubwa.

“Sikujali tangu zamani juu ya kutekelezwa na baba watoto wangu, ila naumia kwa kukosa kazi ya kuniingizia kipato hata ya kumudu dawa ya kumsafishia mwanangu anapomaliza kujisaidia au mifuko ya kumvalisha, maana kwa sasa kukosa maradhi ni kudra zake Manani peke yake, ukizingatia kwamba namfunga kitambaa tumbo mwake.

“Wapo wadudu wakali wa bacteria wanaweza kuingia na kumshambulia mwanangu, lakini nabaki sina la kufanya, maana hata ndugu zangu nao hawana cha kunisaidia zaidi ya kuniacha kama nilivyo na kuhangaika na mtoto wangu John,” alisema Veronica.

Veronica anasema kabla ya kupata ujauzito huo, alikuwa akifanya kazi kwa Muhindi mmoja, anayejulikana kwa jina la Ghafur, maeneo ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, alipofanya kazi kwa miaka mitatu, huku akilipwa Sh elfu 60,000 kwa mwezi.

Baada ya kujifungua mtoto huyo na kuwa kwenye tatizo hilo, bosi wake alimwambia apumzike ahangaikie afya yake, jambo ambalo lilizidi kumchanganya, ukizingatia kwamba maradhi ya mtoto wake yanahitaji fedha.

Mama huyo anasema anaomba msaada kutoka kwa Watanzania wote wenye moyo wa huruma juu ya kumsaidia mtoto wake ili apate mwarobaini wa tatizo lake, ukizingatia kwamba wataalamu wa afya  wamesema uwezekano huo upo akifika India.

“Wamesema utaalamu huu upo India hivyo kunitaka niende kama uwezo ninao, lakini mimi maisha yangu ni magumu na wakati mwingine nabangaiza hata kula yangu, sasa hiyo hela ya kunifikisha huko India nitapata wapi?

“Naomba waandishi mfikishe maombi yangu, maana mwanangu anateseka na inapofikia wakati wa mawingu mazito analia na kuumia sana au pale anapotaka kupata haja kubwa,” alisema.

Veronica anasema kwamba anaowaomba watu wote wajitolee chochote walichokuwa nacho, au afikishwe India na kugharamiwa mahitaji yote, ili afya ya mtoto wake iwe kama ya watoto wengine wenye amani katika maisha yao.

Veronica amemzaa mtoto wake huyo Oktoba 23 mwaka 2011 katika Hospitali ya Mwanyamala, jijini Dar es Salaam, alipomzaa kwa njia ya kawaida.

Anachokumbuka, ni kwamba ujauzito wa mtoto wake ulimpa tabu, ikiwamo kutokwa na damu puani pamoja na kugundulika kuwa ana ugonjwa wa malaria, ambapo baadaye damu zilikata.

Mama huyo mwenye miaka 29, licha ya kukosa uwezo wa kumsaidia mtoto wake, pia maisha yake ni magumu, ingawa mwenyewe hayo ameyaweka pembeni zaidi ya kuangalia kwanza afya ya mtoto wake na awe kwenye afya njema.

“Najua kwa sasa sina kazi wala biashara yoyote, ila haya yatakwisha kama nitaingia kwenye shughuli zangu, ukizingatia niliachishwa kazi kwa Muhindi, akiwa na nia njema tu ya kunipa nafasi ya kuhangaikia afya ya mwanangu, lakini hakujua kama uamuzi ule ni mchungu mno, ukizingatia kwamba hata huo mshahara mdogo kutoka kwake niliukosa,” alisema Veronica.

Watanzania wenzangu, sambamba na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto chini ya waziri wake, Sophia Simba, Wizara ya Afya na kampuni mbalimbali nchini tuna kila sababu ya kumsaidia  mtoto huyu ili aweze kupelekwa nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Kama unahitaji kujua chochote juu ya mtoto Godfrey John, wasiliana na mama yake kwa namba 0715 837700.



Wednesday, October 24, 2012

MGODI UNAOTEMBEA




Washindi chaguzi za CCM, wapime viatu vyao


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAGUZI za ndani za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimekuwa zikiendelea huku kukiwa na malalamiko mengi ya rafu kutoka kwa baadhi ya wagombea. Wapo wanaolalamika juu ya kufanyiwa mchezo mchafu, ukiwamo kumwaga fedha kwenye uchaguzi wao.

Malalamiko hayo yamekuwa yakisemwa baada ya uchaguzi au kabla, jambo ambalo hata hivyo ni kawaida katika chaguzi zenye upinzani na ushindani wa wagombea.

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Mrisho Kikwete
 
Kwa mfano, juzi katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), wapo watu waliolalamika kuwa kuna kundi likikuwa likitoa rushwa chooni, ikiwa ni muendelezo wa vituko vilivyotokea kwa wingi kwenye uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma.

Kituko kingine cha aina yake ni purukushani iliyoibuka baada ya mwanachama wa CCM, ambaye pia Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy Rose Bhanji, alipomuuliza mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba namna ya kuitumikia nafasi yake ipasavyo na kwa manufaa makubwa ndani ya chama chake hicho.

         Siphia Simba, mwenyekiti UWT

Majibu ya Simba inaonyesha hayakumfurahisha Shy hasa aliposema kuwa bado ni mchanga kisiasa na hajui watu wanavyofanya. Ni majibu mepesi katika uchaguzi mzito unaotingisha nchi nzima, hasa jumuiya hiyo, ambayo kila mtu anaifuatilia.

Ikumbukwe kuwa, ndani ya CCM yenyewe, uchaguzi wa jumuiya hiyo ulikuwa na nguvu kiasi cha kutingisha makundi mawili ambayo yalikuwa kati ya Simba na Anne Kilango.

                             Shy Rose Bhanji, mbunge wa Afrika Mashariki
 
Kila mtu alikuwa akiamini kuwa ana ari na sababu ya kuongoza kiti hicho, ambacho ni dhahiri kina manufaa makubwa na chama chao.

UWT endapo inatumika vizuri, inaweza kutangaza sera za chama pamoja na kuwavuta akina mama wengi zaidi kwenye chama chao pamoja na kuwabakiza waliopo kwa kunadi vitu vya kimaendeleo ama kuwaunganisha wanawake Tanzania Bara na Visiwani.

Ni kwa kulijua hilo, naamini sasa kuna haja ya washindi wa chaguzi za ndani za chama hicho, kujipima kama viatu walivyovaa vinawatosha. Nimekuwa nikilisemea hili katika makala zangu mara kwa mara kwa ajili ya kuijenga CCM imara.

Nimekuwa pia nikiikosoa mwenendo wowote mbaya ndani ya CCM, ikiwamo rushwa, ingawa wachache wao wanashindwa kunielewa na kuanza kunitumia meseji zisizokuwa na kichwa wala miguu kwa sababu wanazojua wenyewe.

Ukiacha nafasi za mwenyekiti wa Mkoa, wilaya, mweka hazina au Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, chaguzi za jumuiya za CCM ni nyeti na zimeanza zamani mno.

Umoja wa Wanawake Tanzania pamoja na Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), ulianzishwa zamani, huku Bibi Titi Mohamed akiwa mwenyekiti wa kwanza wa umoja wa wanawake Tanzania.

Kwa mujibu wa historia na harakati za CCM, tangu wakati huo inaitwa TANU, jumuiya hizo ziliundwa kwa ajili ya kukiweka chama hicho katika hali nzuri, sambamba na kuwavuta wengine, mfumo ambao hadi leo umeendelea.

Kwa bahati mbaya, nyakati za leo, mambo yamekuwa yakibadilika kutokana na wanaopewa nafasi hizo, baadhi yao kutokuwa na jipya. Ni watu ambao viatu wanavyolilia kupewa na chama, haviwatoshi.

Kwa wale wanaojua adha ya kuvaa vatu visivyokutosha, iwe kidogo au kikubwa, watakubaliana na mimi kuwa ni mbaya mno. Ndio maana nasema, walau sasa wale ambao wameshapata bafasi hizo za chama, wajiangalie tena.

Wajipime wenyewe kama kweli wanaweza kuwa na mchango na CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Wameingia madarakani katika kipindi kigumu mno. Kipindi ambacho fikra za watu wengi zinaamini enzi za CCM zimekwisha.

Kipindi ambacho wakati wao wanawania nafasi hizo, wengine wanapita chini chini kujaribu kutafuta namna ya kupenyeza watu ambao baadaye iwe turufu kwao. Hizi ni dalili mbaya kwa CCM, hasa kama watu hao wamefanikiwa.

Ni wakati sasa wa Viongozi wa CCM Taifa, akiwamo mwenyekiti wake, Jakaya Mrisho Kikwete na wenzake kukaa na kuwapima kwa vitendo washindi wao. Hili sio baya likifanywa na CCM, maana lengo ni kuwaweka sawa.

Kama walitoa sera zao mbele ya wajumbe na wapiga kura wao katika uchaguzi huo wa ndani, basi waseme pia namna ya kukisaidia chama ili kiende sambamba na presha ya vyama vya upinzani vyenye hamu ya kuongoza dola.

Ni dhahiri CCM ipo kwenye kipindi cha hatari. Kama juhudi zisipochukuliwa, dalili za kuanguka katika uchaguzi mkuu ujao ni kubwa. Hili lisemwe hata kama watu wachache halitawafurahisha.

Wale waliozea kusifiwa au kudanganywa kuwa mambo yapo vizuri, wakati hali ni mbaya na jamii imekuwa ikiweka chuki za wazi wazi kwa viongozi wa ndani wa chama na wanachama wao kwa ujumla.

Kwa mfano, kampeni za kuwania nafasi za udiwani katika baadhi ya maeneo zimekuwa zikiendelea kwa vyama kuwania viti hivyo. Ingawa wakati wa kura bado, lakini matokeo katika chaguzi hizo pia ziwe kipimo cha CCM.

Wanachama na viongozi wa CCM wasikubali kuweka viongozi ambao kwa miaka mitano hawatakuwa na mchango wowote. Wasiwe viongozi wa kukaa ofisini tu, au wafanya kazi kwa simu, wakizungumza kwa  wao.

Viongozi wa chama, kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa wapende kuzungumza na wananchi ambao hao ndio walengwa wakuu. Wazungumze na wapiga kura, ambao hao ndio watakaokuwa na kazi moja ya kuibakisha CCM madarakani au kuimwaga.

Kama hivyo ndivyo, basi tuanze kwanza kuangalia uhalali wa nafasi za chama na kuangalia pia viatu vya washindi ili wajipime pia utendaji wao katika kipindi cha uongozi wao.

Najua wapo watakaohoji sababu hiyo ukizingatia kwamba asilimia kubwa ya viongozi wameshapatikana, ila huko kushinda, ndio iwe sababu ya wao wenyewe kuangalia namna ya kuongoza kwa manufaa na CCM.

CCM wilaya, mkoa na Taifa hili lazima walijuwe ili chama kibaki salama katika Uchaguzi Mkuu ujao, utakaofanyika mwaka 2015. Uchaguzi ambao huenda ukawa mchungu sana kwa CCM, maana watu wengi, wakiwamo vijana ambao ndio wapiga kura, wamekuwa na hasira na chama hiki kikongwe na kutamani kukiweka kando.

Wapinzani wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali, zikiwamo za mikutano katika maeneo tofauti, jambo ambalo CCM nao lazima walijuwe.

Wasikae kucheka, kuwaona wapinzani ni majuha, wakati elimu ya uraia inasambazwa kwa kasi ya ajabu na watu wanaanza kujua wajibu na haki zao za kuongozwa na vyama tofauti na CCM.

Nasema hili bila kuangalia wale rafiki zangu wanaonisema au kunitukana. Wale ambao nia yao haswa watu tubaki kimya, tuchekee matatizo ya CCM, ili iwe nafasi ya kuanguka katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Nalisema hili pia bila kuangalia wanachama wangapi wa CCM na viongozi wake watanikosoa, wakisema makala yangu yameegemea kukichafua. Huo ndio ukweli. Daima hauwezi kuwafurahisha kila mmoja duniani.

Sitarajii kukaa kwa bashasha na kusubiria kuwafurahisha kila mmoja, maana katika Dunia hilo jambo sio rahisi. CCM wajiangalie katika kipindi ambacho chama kimewaona wanafaa hivyo nafasi zao lazima ziwe na tija kwa chama.

Yale makundi hasimu za wagombea yavunjwe na wanachama wote wawe kitu kimoja, bila kuangalia aliyeshinda au aliyeshindwa. Bila hivyo, makundi hayo pia yatazidi kuwa mwiba mchungu kwa chama hicho, ndio maana ninahoji uhalali wa viatu vya watu hao.

Huo ndio ukweli, ikiwa ni mwelekeo wa mwisho mwisho katika chaguzi za Chama cha Mapinduzi zenye joto kali katika wilaya na mikoa mbalimbali, huku kila mtu akiona ana kila sababu ya kuwa kiongozi wa chama, ingawa lengo lake haswa linashindwa kujulikana, hasa eneo lake linapotawaliwa zaidi na upinzani siku baada ya siku.

0712 053949
0753 806087

Watoto wa Mukajanga waanzisha kampuni ya mitindo



 Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATOTO wa Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubu Mukajanga, wameanzisha kampuni yao ya mitindo, inayojulikana kama TRIDASHANZ Business  Modeling kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao vya mitindo.

        Watoto wa Kajubi Mukajanga, Patricia na dada yake Sanza katikati 

Watoto hao ni Sanza Mukajanga na ndugu yake Patricia, ambao kwa vipindi tofauti walishiriki mashindano ya urembo, likiwamo Miss Dar City Centre kwa Patricia na Sanza, aliyeshiriki shindano la Miss Chang’ombe na wote kuingia katika nafasi nzuri katika patashika hizo za urembo.

Akizungumza jana na HANDENI KWETU jijini Dar es Salaam, Sanza, alisema kwamba wameamua kuanzisha kampuni hiyo kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali zinazohusu sanaa, ikiwamo ya kuandaa shoo za mitindo, urembo na mengineyo.

    Katibu wa Baraza la Habari (MCT), Kajubi Mukajanga 
Alisema ujio wa kampuni hiyo ni mwelekeo mpya wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sanaa hapa nchini, wakiamini kuwa malengo yao waliyojiwekea yatatatimia kwa kuwa karibu na mitindo.

“Ni harakati za kimaendeleo zaidi  huku nikiamini kuwa tufanikisha mipango yetu ya kuibua pua vipaji vipya vya mitindo au urembo, ukizingatia kwa miaka kadhaa tumefanya sanaa ya aina hiyo.

“Kwa sasa tunachofanya ni kuweka mikakati ya kushirikisha wanamitindo mbalimbali katika programu zetu tulizoweka kabla ya kuanzisha kampuni hii ambayo kwa kiasi Fulani itakuwa na mafanikio makubwa,” alisema Sanza.

Kwa mujibu wa Sanza, tayari warembo zaidi ya 10 wameanza mazoezi ya mitindo katika Ukumbi wa Golden Bridge, uliopo maeneo ya Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam mapema wiki hii.

Tino kuzindua filamu ya mapigano Ijumaa





Tino Muya

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKALI wa filamu hapa nchini, Tino Muya, kesho Ijumaa anatarajia kuizundua filamu yake mpya ya mapigano, inayojulikana kama (CID), katika Ukumbi wa Biashara Complex.

Filamu hiyo imeandaliwa kwa kiwango cha juu, huku ikiwa ya kwanza kwa msanii huyo kucheza filamu za mapigano, ukizingatia kwamba kwa muda mrefu amekuwa akicheza zile zinazoelezea uhusiano wa kimapenzi tu.

Akizungumza muda mfupi na HANDENI KWETU, Tino alisema kwamba filamu hiyo ipo kwenye ubora wa hali ya juu, huku akipanga kuizindua Ijumaa katika Ukumbi wa Biashara Complex, Kijitonyama.

Alisema wadau na mashabiki wa filamu watapata kutu kizuri kutoka kwake, akiandaa chini ya Kampuni yake ya Tino Muya Films Company, aliyoanzisha mwaka 2009 kwa ajili ya kujihusisha na sanaa hapa nchini.

“Ni matarajio yangu kuwa watu watapata kitu kizuri kutoka kwangu, huku nikiachana kabisa na filamu za mapenzi kwa ajili ya kubadilisha soko la filamu hapa nchini kutoka mapenzi hadi mapigano.

“Naamini wadau na mashabiki watakuja kwa wingi kujionea jinsi gani watu wanaingia katika ulimwengu mpya wa filamu, maana wasanii wengi na waandaaji wamekuwa wakitayarisha filamu za kimapenzi tu,” alisema Tino.

Filamu nyingine zilizoaandaliwa na kampuni hiyo ni pamoja na Hatia, Shoga Yangu, Nzowa, One Blood, Hazard, My Heart, Olopong, Means Day Out, End of the Day, Good Fellow, Rooleen na sasa CID, filamu ambayo imeandaliwa kwa ufanisi kwa nia ya kuleta mapinduzi kisanaa.

Tuesday, October 23, 2012

ALBERT SANGA





                                       Aliyepania kuwakomboa Watanzania

                                         Albert Sanga, Mkurugenzi wa Fresh Farm T (Ltd)

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUNA juhudi kubwa zinazofanywa na baadhi ya Watanzania, hasa kwa kuanzisha makampuni ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuwakomboa wenzao.

Makampuni hayo yanajishughulisha kwa biashara mbalimbali, hivyo kuwa njia nzuri ya kuwapatia maisha bora kama wataendeleza mikakati hiyo.



Miongoni mwa watu hao ni Albert Sanga, mjasiriamali aliyeanzisha Kampuni ya utunzaji wa mazingira ya Fresh Farm (T), yenye makazi yake wilayani Mufindi, mkoani Iringa.

Kusudio kubwa ni kuokoa mazingira na kuwatajirisha watanzania kwa kuwekeza kwenye kilimo cha miti ambayo ni biashara nzuri kwa miaka ya leo na kesho, hivyo kujikomboa zaidi katika maisha yao endapo watajiingiza humo.

“Lazima nikiri kilimo cha miti kimepata umaarufu kwa miaka ya karibuni kutokana na ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya mazingira, huku Iringa tukiongoza kwa misitu mikubwa ya kupandwa.


“Sasa hii miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea pamoja na utengenezeaji wa karatasi na kuyaachia mashirika ya kimazingira kutoka Ulaya wakati ardhi ni ya kwetu na utajiri huo unakwenda kwao,” alisema.

Kwa kupanda shamba la miti na kukusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae na kuvuna mbao, nguzo ama miti ghafi ya kutengenezea karatasi, ni uokoaji wa mazingira kwa kiasi kikubwa.

Anasema alianzisha biashara hiyo kwa miaka minne iliyopita na kujiwekea malengo ya kupanda miti ekari ishirini kila mwaka, huku kilimo hiki cha miti kikiwa ni uwekezaji wa muda wa kati na mrefu, ingawa Watanzania wengi hawavutiwi na uwekezaji wa muda mrefu.

Sanga ambaye ni mtaalamu wa biashara anasema kwamba namna bora ya kunufaika kiuchumi, ni uwekezaji wa muda mrefu, Waingereza wanasema ‘Information is power’, hivyo Ulaya na Amerika wananunua hewa ya Ukaa na kutajirika zaidi kwa kupitia kilimo cha miti.

Anasema zipo ekari zinauzwa kwa utaratibu rasmi na kwa mujibu wa sheria ya ardhi ukizingatia kuwa ekari moja ya shamba inachukua wastani wa miti mia sita na wastani wa chini wa mti mmoja uliokomaa ni elfu 20,000.

“Ina maana katika ekari moja ukiwa na miti iliyokomaa unakusanya jumla ya shilingi milioni 12,000,000, ikiwa ni fedha za kadirio la chini ikiwa mkulima atauza bei ya jumla miti inapokuwa shambani.
 
“Lakini kama ukiamua kupasua mbao mwenyewe unaweza kuvuna mbao hadi za milioni ishirini na tano 25,000,000 kwa ekari moja huku kukiwa hakuna gharama za moja kwa moja hapa, ukizingatia kuwa Iringa ni mkoa wenye miundombinu nafuu,” alisema Sanga.

Sanga anasema kwamba gharama za kununua shamba tupu ni shilingi laki mbili hadi milioni moja na kutegemea na maeneo yanayotakiwa na mhusika, huku gharama za kuandaa shamba, kununua miche na kupanda ni kati ya shilingi 400,000 hadi laki 600,000.

Kilimo cha miti ni rahisi kwa sababu haihitaji uangalizi mkubwa muda wote na mvua inyeshe au isinyeshe, maana mti ya mbao, nguzo ama karatasi ukishachipua huwa haufi kwakuwa huendelea kutumia unyevu wa ardhini.

“Muhimu ni kutengeneza njia za kuzuia moto walau mara moja kwa mwaka, kazi ya pili ni kufyekea miti inapokua walau kwa mwaka mara moja (prooning) na kudai kuwa gharama hizi hazizidi laki laki mbili kwa mwaka.

“Kwa mfano ukichukua shilingi laki mbili kugharimia shamba kila mwaka ukazidisha mara sita unapata sh 1,200,000 na ukizidisha mara 10 unapata 2,000,000,” alisema.

Mkurugenzi huyo wa Fresh Farm (T) anasema mtu akiwa na shamba la miti leo; thamani ya ardhi hivyo kupata faida bila kuangalia umbali wa kuikuza miti hiyo kama wengi wao wanavyojidanganya kwamba biashara hii si ya muda mfupi.

Anasema mtu akishapanda shamba la miti la ekari moja na kuamua kuuza baada ya mwaka mmoja, basi mauzo yake hayatakuwa chini ya milioni mbili hadi nne.

Hivyo mtu huyo atakuwa amekusanya shilingi 4,000,000 kwa mtaji wa shilingi 600,000 bila kupata usumbufu wowote wa kusimamia.

Sanga anasema kwao msimu wa kutafuta na kuandaa mashamba ni Agosti na Oktoba, huku upandaji ukiwa ni Novemba, Desemba na Januari, ikiwa ni njia ya kuwasaidia wengine ili wawekeze katika biashara hii ya mashamba.
 
“Siku zote napenda kuendeleza wafanyabiashara na wawekezaji wapya kwa kupitia mfumo wa biashara zetu, hivyo tumeanzisha kitengo maalumu cha Fresh Farms (T) na kazi yetu kubwa itakuwa ni kupitia kitengo hiki itakuwa ni kutoa ushauri wa kibiashara, kutafuta maeneo ya kilimo cha miti hapa Iringa pamoja na kiasi heka anazotaka mteja,” alisema Sanga.

Kwa mujibu wa Sanga, Fresh Farm (T) inatumia sheria ya ardhi ya mwaka 1999, pia taratibu na tamaduni zote za wenyeji zinazohusiana na umilikaji ardhi, hivyo kuwa na uhakika wa kutunza mazingira na kuwatajirisha watanzania.

0712 053949
0753 806087

Saturday, October 20, 2012

Teknolojia ya Live line ni mkombozi kwa Taifa



       Mc Donald Mwakamele wa pili kutoka kulia waliosimama mstari wa mbele
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUKUA kwa maendeleo ya Teknolojia, kunawafanya binadamu wengi kuendelea kuumiza kichwa kwa ajili ya kuufaidisha ulimwengu kwa namna moja ama nyingine.

Watu wengi, wakiwamo wana taaluma wa aina mbalimbali, wamekuwa wakikaa na kusumbua vichwa kwa ajili ya kubuni au kuendeleza yale yanayoweza kuikomboa Dunia katika vitu vya aina aina.

Licha ya Dunia kupiga hatua katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini kwa Watanzania, imekuwa vigumu kuona ndugu zao wamefanikiwa kugundua vitu ambavyo baadaye vitakuwa tegemeo la Dunia.

Ndipo hapo kila kitu utakuta kimebuniwa na watu wa nchi zilizoendelea, huku sisi tukiwa hodari wa kutumia teknolojia hizo kwa gharama kubwa.

 Mc Donald Mwakamele akiwa juu ya nguzo

Wakati naendelea kuwaza hayo, nashangazwa na hatua ya Mtanzania mwenzetu, Donald Mwakamele, anayejenga chuo cha Mc Donald Live Line Training Centre, katika mji wa Dakawa, wilaya ya Mvomelo, mkoani Morogoro.

Ni chuo cha kisasa kitakachojishughulisha na masuala ya kutengeneza bila kuzima umeme, hasa ikizingatia kwa sasa Taifa linakabiriwa na matatizo mengi yanayosababisha muda mwingi kuwa gizani.

HANDENI KWETU ilitembelea eneo la chuo, ambapo pia siku hiyo, wakati ambao wageni kutoka kutoka nchi mbalimbali duniani walikwenda kujifunza namna chuo hicho kitakavyofanya kazi zake.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete 
Mmiliki na Mkurugenzi Mkuu wa chuo hicho, Mc Donald Mwakamele, anasema anaingia kwenye teknolojia hiyo, huku akiwa na mwarobaini wa umeme wa uhakika miaka michache ijayo.

Teknolojia hiyo ya umeme, inaingia huku ikiwa ngeni katika nchi nyingi duniani, zikiwamo za Barani Afrika, ambazo zinaendelea kutengeneza umeme usiokuwa wa uhakika, pamoja na kuzima bila sababu za msingi.

“Kwa mfano, hapa naweza kuchomoa kikombe chochote katika mitambo iliyopo hapa na jamii inayopata umeme kutokana na njia hii, kamwe haiwezi kuathiriwa na ukarabati huu ambao hapo kabla ulikuwa mpaka wazime umeme.

“Hii Dunia ya leo inahitaji ubunifu wa hali ya juu, ndio maana nikaona ipo haja ya sisi watu tulioingia katika mambo haya ya mitambo ya umeme, kuwa makini mno na kubuni mbinu mbadala za kusaidia tatizo la umeme,” alisema Mwakamele.

Mwakamele aliyewahi kuwa mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania Tanesco, anasema wazo hilo la chuo cha umeme, limetokana na kuendeleza mawazo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Miaka ya 1988, Jakaya Kikwete, alikuwa na mawazo ya Tanzania kuwa na chuo cha namna hiyo, kitakachokuwa kinafundisha masuala ya umeme, hasa teknolojia ya kutengeneza bila kuzima umeme.

Chuo cha namna hiyo kinahitaji mtaji mkubwa, ndio maana kwa upande kimechukua muda mrefu kuweka mipango na mikakati ya kufanikisha suala hilo, huku akiamini kufanikiwa kwa teknolojia hiyo, ni msaada mkubwa kwa vizazi vya leo na kesho vinavyokabiriwa na matatizo ya umeme.

Kwa kuanzia, chuo hicho kitafundisha wakurugenzi, maprofesa na wengineo, kwa ajili ya kuwapa makali zaidi, ili waende kutoa elimu hiyo katika sehemu zao za kazi.

Baada ya hapo, elimu hiyo itaanza kutolewa kwa watu wa kawaida, bila kuangalia elimu zao, maana suala la ufundi, linahitaji vichwa zaidi pamoja na wale wenye uthubutu wa kufanya kazi.

Hata hivyo, katika kuangalia nani anaweza kuingia kwenye chuo hicho, kutahitaji kwanza vipimo vya wanafunzi hao, ukizingatia kwamba lengo lake haswa ni kuendeleza taaluma hiyo ya umeme.

“Tangu niache kufanya kazi katika shirika la umeme la Tanesco, mengi nimegundua ikiwamo watu kushindwa kujifunza zaidi, badala yake wanafanya mzaha na kuendeleza majungu sehemu za kazi.

“Hayo yamesababisha Taifa lishindwe kuendelea, ndio maana Tanesco ya leo inachojua wao ni kuzima umeme bila sababu za msingi, bila kujua hasara kiasi gani inapatikana kwa kuzima umeme japo kwa nusu saa tu,” alisema.

Mwakamele anasema katika mwendelezo wa chuo hicho, taaluma hiyo ya umeme itaendelezwa zaidi, ikiwamo kufua umeme wa kutokana na jua (solar panel), akiamini kuwa huo pia utasababisha huduma hiyo kuwa ya rahisi zaidi.

Ili mteja apate umeme, anahitaji kuwa na fedha nyingi, huku Shirika lenyewe likiendeshwa bila mipango, jambo ambalo anaamini Mc Donald Training Centre litaondosha matatizo hayo.

Kufanikisha mikakati hiyo, kutalisaidia Taifa, maana bila umeme wa uhakika, nchi haiwezi kupiga hatua katika masuala mbalimbali, yakiwamo uchumi, unaohitaji kuwa na viwanda vinavyoendeshwa na umeme.

Hadi sasa, Chuo hicho kimetumia zaidi ya Sh Milioni 900, huku taratibu za usajili zikitarajiwa kuanza hivi karibuni.

Mwakamele, anasema utaalamu wake na elimu yake imetokana na kusomeshwa na serikali, ambayo leo anapanga namna ya kuinufaisha kwa teknolojia hiyo.

Mbali na kuanzisha chuo hicho, Mwakamele anamiliki Kampuni ya Mc Donald Live Line Technology Ltd. Injinia huyo anasema, ni budi wataalamu wote wanaohusika na mambo ya umeme kuichukia tabia ya kuzima nishati hiyo inayosababisha Taifa kupata hasara kubwa.

Kutokana na kadhia hiyo, kampuni mbalimbali pamoja na watu wa majumbani wamekuwa wakipata hasara, hasa pale kifaa kinapoungua kutokana na umeme kukatika, eti kwa sababu ya matengenezo ya Tanesco.

“Taifa linaweza kutoka huko, ndio maana leo nimepokea ugeni kutoka nchi mbalimbali, wakija kwa nia ya kujifunza juu ya hili, ukizingatia kwa sasa napenda kutoa elimu tu, huku uinjinia nikiachia watu wengine nje au waliokuwa kwenye kampuni yangu ya Mc Donald Live Line Technology Ltd inayopiga hatua kubwa zaidi kwa kushuhudia ugunduzi huu mpya.

“Katika hili, naomba jamii iendelee kuniunga mkono huku wale wasionitakia mema wakikaa chonjo, maana nimeingia kwa kasi na siwezi kuogopa hujuma na vitisho kutoka kwa wapinzani wangu, kwakuwa lengo si kuonyeshana umwamba, bali ni kutangaza vipaji na uwezo wa kufanya kazi kwa ajili ya Tanzania yetu,” alisema.

Kwa mujibu wa Mc Donald, ugeni wake kwenye chuo hicho ulitembelea Septemba 13 ingawa njia ya kupeleka umeme kwenye eneo hilo zilizimwa kwa sababu ya matengenezo mafupi, kama walivyosema Tanesco, hivyo kuwafanya watu hao wasionyeshwe teknolojia hiyo, zaidi ya kushuhudia mitambo ya aina mbalimbali iliyofungwa katika chuo hicho.

0712 053949
0753 806087

Friday, October 19, 2012

Wambura aangusha kigogo DRFA

Michael Wambura, aliyemkatia rufaa Bakherea. Picha na Maktaba yetu.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imechukua uamuzi magumu, baada ya kumwengua Mwenyekiki wa Chama cha soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Amin Mohamed Bakhresa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa chama hicho.

Bakhressa ambaye alikuwa madarakani zaidi ya miaka 10 hatima yake ya  kuendelea kuwania tena ndani ya chama hicho ilifikia tamati jana, baada ya kubainika hana sifa inayostahili kwa mujibu wa katiba ya DRFA.

Uchaguzi huo ambao ulipangwa kufanyika Oktoba 14, umesongezwa mbele hadi Desemba 8, mwaka huu, baada ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliyochini ya Mwenyekiti wake, Muhindin Ndolanga kufutwa.

Kamati hiyo ilihusika kwa kiwango kikubwa katika ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi na kutozingatia matakwa ya katiba ya DRFA katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratias Lyatto, alisema kwa kuzingatia katiba ya TFF ibara ya 40(1), kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF ibara ya 10(6), 12 (1) na 26 (2) na (3), imeifuta kamati ya DRFA.

Lyatto alisema DRFA imeagizwa kuteuwa kamati mpya ya uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya DRFA.

Alisema uteuzi huo unatakiwa kufanyika kabla ya Oktoba 25 mwaka huu, ambapo mchakato wa uchaguzi utaanza upya utaanza Oktoba 29 mwaka huu.

Hata hivyo, Lyatto alisema kamati yake ilipitia rufani mbalimbali zilizowasilisha na vyama vya soka vya Mkoa wa Mbeya, Shinyanga na Dar es Salaam.

Kamati hiyomilipokea rufaa dhidi ya Mohamed Salim Bakhressa, ambaye aliomba kuwania nafasi ya mwenyekiti wa DRFA iliyowakilishwa na  Michael  Wambura na Juma Jabir iliomba jina liondolewa katika orodha ya wagombea kwa kuwa hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo kutokidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara ya 29(2).

 ‘Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya DRFA hana budi awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne," alisema Lyatto.

Lyatto alisema baada ya kupitia vielelezo kuhusu rufaa dhidi ya maamuzi ya kamati ya uchaguzi ya DRFA na kujadili maelezo ya warufani, Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na ilijiridhisha  Bakhressa  hana elimu ya kiwango hicho.

Alisema kwa  kutokidhi matakwa hayo ya katiba ya DRFA, hastahili kugombea nafasi ya mwenyekiti wa DRFA na kamati ya uchaguzi ilikubaliana na maombi ya warufaa.

 Kamati ya uchaguzi ya DRFA iliwapitisha wagombea Gungurugwa Tambaza,  Mohammed Bhinda, Benny Kisaka na Hamisi Ayoub 'Mpapai' bila kuwa na vielelezo vinavyothibitisha kuwa wana kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne.

 Kutokana na mkanganyiko, maelezo yenye utata kutoka kwa warufani na warufaniwa na maamuzi ya utata ya kamati ya uchaguzi ya DRFA, yameufanya mchakato wa uchaguzi wa DRFA, kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za uchaguzi za TFF.

TWFA yataka orodha ya wapiga kura


                Zena Chande, mgombea TWFA
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya Mwenyekiti wake Ombeni Zavala imewataka wanachama wa TWFA ambao ni mikoa ya Tanzania Bara kuwasilisha orodha ya wajumbe wao wa mkutano wa uchaguzi.
 
Wajumbe wenye sifa ya kuhudhuria Mkutano wa TWFA ni kutoka vyama vya mikoa ambavyo tayari vimefanya uchaguzi. Wajumbe hao ni Mwenyekiti, Katibu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA.
 
Mikoa ambayo imeshafanya uchaguzi mpaka sasa ni Iringa, Kigoma, Mwanza, Pwani na Tanga. Mikoa ambayo bado inahimizwa kufanya uchaguzi, na mwisho wa kutuma majina ya wajumbe kwa Mwenyekiti Zavala ni Oktoba 25 mwaka huu.
 
Mkoa ambao utakuwa haujafanya uchaguzi utakuwa umenyimwa haki ya kushiriki uchaguzi wa TWFA utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu.

Yanga na Ruvu Shooting sasa Taifa

Na Mwandishi Wetu, TFF
Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kati ya Yanga na Ruvu Shooting uliopangwa kuchezwa kesho (Oktoba 20 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi sasa umehamishiwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.
 
Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na maombi ya timu hizo mbili kutaka mechi ichezwe Uwanja wa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ambazo zimeridhiwa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwemo siku hiyo uwanja huo kutokuwa na mechi.
 
Viingilio katika mechi hiyo itakayokuwa chini ya mwamuzi Amon Paul kutoka Mara ni sh. 5,000 viti vya kijani na bluu, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP B na C na sh. 20,000 kwa VIP A.
 
Pia Kamati ya Ligi imekataa ombi la timu ya Azam kutaka mechi zake za nyumbani za ligi hiyo zichezwe dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Chamazi kutokana na sababu za kiusalama.
 
Nayo Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa kesho (Oktoba 20 mwaka huu) katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
 
Mchezo huo namba 56 wa kukamilisha raundi ya nane utachezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo atakayesaidiwa na Hamis Chang’walu na Omari Kambangwa, wote kutoka Dar es Salaam.
 
Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili (Oktoba 21 mwaka huu) kwa mechi tatu. JKT Ruvu itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi, Mgambo Shooting itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Tanzania Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Twanga na Facebook Mzalendo Pub Jumapili


    Kalala Junior akiwaimbisha mashabiki wa Twanga Pepeta
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BENDI ya muziki wa dansi hapa nchini ya The African Stars, Twanga Pepeta, jumapili inatarajia kufanya shoo ya aina yake, waliyoipa jina la Facebook Fans, itakayofanyika katika Ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama.

Kufanyika kwa shoo hiyo ni kuwaweka sawa na kuwakumbuka mashabiki wao wanaoendelea kuwaunga mkono kwa miaka 11 sasa walipoanzisha bendi hiyo inayopendwa na watu wengi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa ASET, Hassan Rehani, alisema mashabiki wao wote, wakiwamo waandishi wa habari na wadau wengine watakumbukwa na kuthaminiwa mchango wao.

Alisema kwamba bendi yao imekuwa ikipita katika vipindi mbalimbali, hivyo wanaamini mafanikio yao kwa sasa yamesababishwa na watu wengi, jambo linalowafanya waandae part hiyo hiyo usiku wa facebook na Twanga.

“Tumekuwa tukifanya vizuri katika soko la muziki wa dansi kutokana na mchango wa kila mmoja wetu, hivyo naamini wadau wote tutakutana katika Ukumbi huo wa Mzalendo na kucheza pamoja kisigino.

“Twanga ni bendi ya kila mmoja, hivyo nadhani changamoto zinazoonekana kwa sasa ni sehemu ya kutufanya tuwe juu zaidi, huku tukiamini kada mbalimbali na jinsi tofauti tutakutana ili tucheze pamoja,” alisema.

Twanga Pepeta ipo chini ya Luiza Mbutu pamoja na waimbaji mbalimbali wenye uwezo wa juu, akiwamo Kalala Junior aliyejiunga na bendi yake hiyo, akitokea Mapacha Watatu na maswahiba zake, Jose Mara na Khalid Chokoraa, huku Ally Akida, Chokoraa, Soud Mohammed au MCD na wengineo wakithibitisha kushiriki katika onyesho hilo kutokana na kuwahi kufanya kazi na bendi hiyo kwa nyakati tofauti.

Ngwasuma kesho jumamosi hapatoshi Makumbusho


     Nyosh Al Sadaat
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WAZEE wa Ngwasuma, FM Academia, kesho Jumamosi wanafanya shoo ya aina yake katika Ukumbi wa Kijiji Cha Makumbusho, uliopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, huku wakipania kuwapa burudani za aina yake mashabiki wao.

Onyesho hilo linafanyika huku bendi hiyo ikitamba na nyimbo mbalimbali, ukiwamo ule wa Otilia, wimbo unaopendwa vilivyo na mashabiki wao katika kumbi wanazokuwapo wakali hao wa dansi nchini.

Akizugumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Kelvin Mkinga, alisema kwamba mashabiki wao waende kwa wingi kujionea manjonjo yao katika tasnia hiyo nchini.

Alisema wanamuziki wao wamekuwa wakifanya shoo za aina yake, wakiwa na lengo la kuonyesha makali yao, hivyo mashabiki wao waendelee kupokea burudani safi kutoka kwa vijana wao.

“FM Academia ni bendi kongwe na imara sana katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini, hivyo naamini mashabiki wetu wataendelea kutuunga mkono kwa ajili ya kuwapatia burudani zaidi.

“Naamini sisi ni wakali na hatuna mpinzani, hivyo jukumu letu ni kufanya kazi nzuri zaidi kwa kutunga nyimbo na kuandaa shoo za aina yake, ukizingatia tuna watu mahiri kuanzia waimbaji hadi wanenguaji,” alisema Mkinga.

FM Academia ipo chini ya Rais wa Vijana, Nyosh Al Sadaat, sambamba na wakali wengine, akiwamo Patchou Mwamba, ambaye pia ni mkali katika tasnia ya filamu hapa nchini, akishiriki katika filamu mbalimbali.