Pages

Pages

Thursday, October 25, 2012

Yasome mateso ya mtoto Godfrey John

Veronica, akionyesha sehemu za tumbo za mwanae mwenye matatizo, baada ya kutobolewa tumbo lake ili aweze kujisaidia. Mama huyo anaomba msaada kwa jamii ili aweze kwenda India kufanyiwa upasuaji...


Amezaliwa bila sehemu ya haja kubwa
Ahitaji msaada wa kwenda India


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
INAPOTOKEA ndugu au sehemu ya familia yako amezaliwa mtoto akiwa mwenye afya njema, hakika hilo ni jambo la kumshukuru Mungu. Katika hilo, kila mmoja huzaliwa kwa kudra za Manani na kuishi kupo mikononi mwake.

Wengi huzaliwa na mateso ya aina yake. Wanazaliwa wakiwa na matatizo makubwa, jambo linaloweza kukufanya ujiulize maswali mengi juu ya matakwa ya Mungu kumuumba mtoto huyo na kuzaliwa katika hali hiyo.

Katika kuwaza huko, binadamu tunatakiwa tumshukuru yeye aliyeweza kuimba Dunia na kuufanya watu wauone usiku na mchana.

Binadamu pia wanatakiwa wamshukurru yeye maana ndio kila kitu katika Dunia, huku ule msemo usemao hujafa hujaumbika ukitimia, kama sio kwake leo basi kwangu kesho.

Nimelazimika kuanza hivi baada ya kuona mateso ya mtoto Godfrey John, mwenye umri wa mwaka mmoja, aliyezaliwa katika Hospitali ya Mwananyamala, mwaka jana, huku akiwa hana sehemu ya haja kubwa, hivyo kulazimika kuishi kwa tabu.

Mama mzazi wa John, Veronica Lawrant, alizungumza na HANDENI KWETU, juzi kuwa mtoto wake alizaliwa akiwa hana njia hiyo huku madaktari wakishindwa kubaini hilo mapema, hadi baada ya siku tatu, alipoanza kujaa mwili wake.

“Nilishangaa mwanangu anavimba mwili wake ikiwa ni siku chache baada ya kumzaa katika hospitali ya Mwanyamala, nikiwa na matumaini makubwa dhidi yake, nikimshukuru Mungu baada ya kujifungua kwa njia ya kawaida.

“Hali yake ilinishtua sana, hivyo kuamua kwenda katika hospitali ya Mnazi Mmoja kupata matibabu ya mtoto wangu mpendwa, hata hivyo madaktari nao hawajabaini lolote zaidi ya kunipa dawa ambazo hazikuwa na msaada,” alisema Veronica, mkazi wa Bunju, jijini Dar es Salaam.

Anasema kwamba baada ya kurudi nyumbani, usiku wake mtoto wake alianza kupata haja kubwa kwa njia yam domo, jambo ambalo lilizidi kumuumiza kichwa na kuamua tena kwenda tena katika Hospitali ya Mwanyamala.

Alipofika, alipata bahati ya kupokelewa vyema, ingawa hakukaa zaidi ya kutakiwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi, ikiwa ni baada ya daktari aliyempokea, aliyemjua kwa jina la Dk Isayo, ingawa hakuwa wa watoto, lakini alijua tatizo kwa kumuangalia tu na kumtaka apelekwe usiku huo.

Huku akiwa na masikitiko makubwa, mama huyo anasema alifika Muhimbili saa saba za usiku na kupokelewa vizuri tayari kwa mtoto wake kuanza kuchunguzwa juu ya afya yake, maana mwili wake ulianza kubadilika sambamba na kujisaidia mara kwa mara kwa njia ya mdomoni, hivyo kuibua wasi wasi mkubwa katika maisha yake.

“Dakika chache baada ya kufika, nilifuatwa na daktari akasema kama nipo tayari nitie sahihi kwa ajili ya mtoto wangu kufanyiwa upasuaji wa tumbo, maana waligundua kuwa hana njia ya haja kubwa, jambo linalomfanya ajisaidie kwa mdomoni.

“Sikuwa na la kusema zaidi ya kukubaliana na uamuzi huo, maana nilijua mwanangu atapata ahueni kama sio kupona kabisa, jambo ambalo naweza kusema namshukuru Mungu kwakuwa yeye ndio muweza wa yote,” alisema.

Kwa mujibu wa Veronica, mtoto wake anaweza kupona kabisa kama atapata upasuaji katika hospitali za Nchini India, ukizingatia kuwa madaktari wamemshauri hivyo ili kurudisha hali ya kawaida ya binadamu, juu ya upasuaji wa Jonh.

Anasema huku akijua hata kula yake ni tabu, anajiuliza wapi kwa kupata kiasi cha fedha cha kumpeleka mtoto wake India kwa matibabu zaidi, maana maisha yake kwa sasa yamekuwa magumu kupita kiasi.

Mama huyo mzaliwa wa Kitiongoji cha Buru, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, anasema kwamba mtoto huyo analea peke yake kwa kusaidiwa na baadhi ya Watanzania wanaojitolea walichokuwa nacho.

Baba yake Godfrey (John) alimkataa mtoto huyo siku chache baada ya ujauzito huo na hata alipozaliwa, hasa alipogundua kuwa mtoto wao amezaliwa na matatizo ya kukosa njia ya haja kubwa, hivyo kuishi kwa mashaka makubwa.

“Sikujali tangu zamani juu ya kutekelezwa na baba watoto wangu, ila naumia kwa kukosa kazi ya kuniingizia kipato hata ya kumudu dawa ya kumsafishia mwanangu anapomaliza kujisaidia au mifuko ya kumvalisha, maana kwa sasa kukosa maradhi ni kudra zake Manani peke yake, ukizingatia kwamba namfunga kitambaa tumbo mwake.

“Wapo wadudu wakali wa bacteria wanaweza kuingia na kumshambulia mwanangu, lakini nabaki sina la kufanya, maana hata ndugu zangu nao hawana cha kunisaidia zaidi ya kuniacha kama nilivyo na kuhangaika na mtoto wangu John,” alisema Veronica.

Veronica anasema kabla ya kupata ujauzito huo, alikuwa akifanya kazi kwa Muhindi mmoja, anayejulikana kwa jina la Ghafur, maeneo ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, alipofanya kazi kwa miaka mitatu, huku akilipwa Sh elfu 60,000 kwa mwezi.

Baada ya kujifungua mtoto huyo na kuwa kwenye tatizo hilo, bosi wake alimwambia apumzike ahangaikie afya yake, jambo ambalo lilizidi kumchanganya, ukizingatia kwamba maradhi ya mtoto wake yanahitaji fedha.

Mama huyo anasema anaomba msaada kutoka kwa Watanzania wote wenye moyo wa huruma juu ya kumsaidia mtoto wake ili apate mwarobaini wa tatizo lake, ukizingatia kwamba wataalamu wa afya  wamesema uwezekano huo upo akifika India.

“Wamesema utaalamu huu upo India hivyo kunitaka niende kama uwezo ninao, lakini mimi maisha yangu ni magumu na wakati mwingine nabangaiza hata kula yangu, sasa hiyo hela ya kunifikisha huko India nitapata wapi?

“Naomba waandishi mfikishe maombi yangu, maana mwanangu anateseka na inapofikia wakati wa mawingu mazito analia na kuumia sana au pale anapotaka kupata haja kubwa,” alisema.

Veronica anasema kwamba anaowaomba watu wote wajitolee chochote walichokuwa nacho, au afikishwe India na kugharamiwa mahitaji yote, ili afya ya mtoto wake iwe kama ya watoto wengine wenye amani katika maisha yao.

Veronica amemzaa mtoto wake huyo Oktoba 23 mwaka 2011 katika Hospitali ya Mwanyamala, jijini Dar es Salaam, alipomzaa kwa njia ya kawaida.

Anachokumbuka, ni kwamba ujauzito wa mtoto wake ulimpa tabu, ikiwamo kutokwa na damu puani pamoja na kugundulika kuwa ana ugonjwa wa malaria, ambapo baadaye damu zilikata.

Mama huyo mwenye miaka 29, licha ya kukosa uwezo wa kumsaidia mtoto wake, pia maisha yake ni magumu, ingawa mwenyewe hayo ameyaweka pembeni zaidi ya kuangalia kwanza afya ya mtoto wake na awe kwenye afya njema.

“Najua kwa sasa sina kazi wala biashara yoyote, ila haya yatakwisha kama nitaingia kwenye shughuli zangu, ukizingatia niliachishwa kazi kwa Muhindi, akiwa na nia njema tu ya kunipa nafasi ya kuhangaikia afya ya mwanangu, lakini hakujua kama uamuzi ule ni mchungu mno, ukizingatia kwamba hata huo mshahara mdogo kutoka kwake niliukosa,” alisema Veronica.

Watanzania wenzangu, sambamba na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto chini ya waziri wake, Sophia Simba, Wizara ya Afya na kampuni mbalimbali nchini tuna kila sababu ya kumsaidia  mtoto huyu ili aweze kupelekwa nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

Kama unahitaji kujua chochote juu ya mtoto Godfrey John, wasiliana na mama yake kwa namba 0715 837700.



No comments:

Post a Comment