Pages

Pages

Saturday, October 20, 2012

Teknolojia ya Live line ni mkombozi kwa Taifa



       Mc Donald Mwakamele wa pili kutoka kulia waliosimama mstari wa mbele
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUKUA kwa maendeleo ya Teknolojia, kunawafanya binadamu wengi kuendelea kuumiza kichwa kwa ajili ya kuufaidisha ulimwengu kwa namna moja ama nyingine.

Watu wengi, wakiwamo wana taaluma wa aina mbalimbali, wamekuwa wakikaa na kusumbua vichwa kwa ajili ya kubuni au kuendeleza yale yanayoweza kuikomboa Dunia katika vitu vya aina aina.

Licha ya Dunia kupiga hatua katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini kwa Watanzania, imekuwa vigumu kuona ndugu zao wamefanikiwa kugundua vitu ambavyo baadaye vitakuwa tegemeo la Dunia.

Ndipo hapo kila kitu utakuta kimebuniwa na watu wa nchi zilizoendelea, huku sisi tukiwa hodari wa kutumia teknolojia hizo kwa gharama kubwa.

 Mc Donald Mwakamele akiwa juu ya nguzo

Wakati naendelea kuwaza hayo, nashangazwa na hatua ya Mtanzania mwenzetu, Donald Mwakamele, anayejenga chuo cha Mc Donald Live Line Training Centre, katika mji wa Dakawa, wilaya ya Mvomelo, mkoani Morogoro.

Ni chuo cha kisasa kitakachojishughulisha na masuala ya kutengeneza bila kuzima umeme, hasa ikizingatia kwa sasa Taifa linakabiriwa na matatizo mengi yanayosababisha muda mwingi kuwa gizani.

HANDENI KWETU ilitembelea eneo la chuo, ambapo pia siku hiyo, wakati ambao wageni kutoka kutoka nchi mbalimbali duniani walikwenda kujifunza namna chuo hicho kitakavyofanya kazi zake.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete 
Mmiliki na Mkurugenzi Mkuu wa chuo hicho, Mc Donald Mwakamele, anasema anaingia kwenye teknolojia hiyo, huku akiwa na mwarobaini wa umeme wa uhakika miaka michache ijayo.

Teknolojia hiyo ya umeme, inaingia huku ikiwa ngeni katika nchi nyingi duniani, zikiwamo za Barani Afrika, ambazo zinaendelea kutengeneza umeme usiokuwa wa uhakika, pamoja na kuzima bila sababu za msingi.

“Kwa mfano, hapa naweza kuchomoa kikombe chochote katika mitambo iliyopo hapa na jamii inayopata umeme kutokana na njia hii, kamwe haiwezi kuathiriwa na ukarabati huu ambao hapo kabla ulikuwa mpaka wazime umeme.

“Hii Dunia ya leo inahitaji ubunifu wa hali ya juu, ndio maana nikaona ipo haja ya sisi watu tulioingia katika mambo haya ya mitambo ya umeme, kuwa makini mno na kubuni mbinu mbadala za kusaidia tatizo la umeme,” alisema Mwakamele.

Mwakamele aliyewahi kuwa mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania Tanesco, anasema wazo hilo la chuo cha umeme, limetokana na kuendeleza mawazo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Miaka ya 1988, Jakaya Kikwete, alikuwa na mawazo ya Tanzania kuwa na chuo cha namna hiyo, kitakachokuwa kinafundisha masuala ya umeme, hasa teknolojia ya kutengeneza bila kuzima umeme.

Chuo cha namna hiyo kinahitaji mtaji mkubwa, ndio maana kwa upande kimechukua muda mrefu kuweka mipango na mikakati ya kufanikisha suala hilo, huku akiamini kufanikiwa kwa teknolojia hiyo, ni msaada mkubwa kwa vizazi vya leo na kesho vinavyokabiriwa na matatizo ya umeme.

Kwa kuanzia, chuo hicho kitafundisha wakurugenzi, maprofesa na wengineo, kwa ajili ya kuwapa makali zaidi, ili waende kutoa elimu hiyo katika sehemu zao za kazi.

Baada ya hapo, elimu hiyo itaanza kutolewa kwa watu wa kawaida, bila kuangalia elimu zao, maana suala la ufundi, linahitaji vichwa zaidi pamoja na wale wenye uthubutu wa kufanya kazi.

Hata hivyo, katika kuangalia nani anaweza kuingia kwenye chuo hicho, kutahitaji kwanza vipimo vya wanafunzi hao, ukizingatia kwamba lengo lake haswa ni kuendeleza taaluma hiyo ya umeme.

“Tangu niache kufanya kazi katika shirika la umeme la Tanesco, mengi nimegundua ikiwamo watu kushindwa kujifunza zaidi, badala yake wanafanya mzaha na kuendeleza majungu sehemu za kazi.

“Hayo yamesababisha Taifa lishindwe kuendelea, ndio maana Tanesco ya leo inachojua wao ni kuzima umeme bila sababu za msingi, bila kujua hasara kiasi gani inapatikana kwa kuzima umeme japo kwa nusu saa tu,” alisema.

Mwakamele anasema katika mwendelezo wa chuo hicho, taaluma hiyo ya umeme itaendelezwa zaidi, ikiwamo kufua umeme wa kutokana na jua (solar panel), akiamini kuwa huo pia utasababisha huduma hiyo kuwa ya rahisi zaidi.

Ili mteja apate umeme, anahitaji kuwa na fedha nyingi, huku Shirika lenyewe likiendeshwa bila mipango, jambo ambalo anaamini Mc Donald Training Centre litaondosha matatizo hayo.

Kufanikisha mikakati hiyo, kutalisaidia Taifa, maana bila umeme wa uhakika, nchi haiwezi kupiga hatua katika masuala mbalimbali, yakiwamo uchumi, unaohitaji kuwa na viwanda vinavyoendeshwa na umeme.

Hadi sasa, Chuo hicho kimetumia zaidi ya Sh Milioni 900, huku taratibu za usajili zikitarajiwa kuanza hivi karibuni.

Mwakamele, anasema utaalamu wake na elimu yake imetokana na kusomeshwa na serikali, ambayo leo anapanga namna ya kuinufaisha kwa teknolojia hiyo.

Mbali na kuanzisha chuo hicho, Mwakamele anamiliki Kampuni ya Mc Donald Live Line Technology Ltd. Injinia huyo anasema, ni budi wataalamu wote wanaohusika na mambo ya umeme kuichukia tabia ya kuzima nishati hiyo inayosababisha Taifa kupata hasara kubwa.

Kutokana na kadhia hiyo, kampuni mbalimbali pamoja na watu wa majumbani wamekuwa wakipata hasara, hasa pale kifaa kinapoungua kutokana na umeme kukatika, eti kwa sababu ya matengenezo ya Tanesco.

“Taifa linaweza kutoka huko, ndio maana leo nimepokea ugeni kutoka nchi mbalimbali, wakija kwa nia ya kujifunza juu ya hili, ukizingatia kwa sasa napenda kutoa elimu tu, huku uinjinia nikiachia watu wengine nje au waliokuwa kwenye kampuni yangu ya Mc Donald Live Line Technology Ltd inayopiga hatua kubwa zaidi kwa kushuhudia ugunduzi huu mpya.

“Katika hili, naomba jamii iendelee kuniunga mkono huku wale wasionitakia mema wakikaa chonjo, maana nimeingia kwa kasi na siwezi kuogopa hujuma na vitisho kutoka kwa wapinzani wangu, kwakuwa lengo si kuonyeshana umwamba, bali ni kutangaza vipaji na uwezo wa kufanya kazi kwa ajili ya Tanzania yetu,” alisema.

Kwa mujibu wa Mc Donald, ugeni wake kwenye chuo hicho ulitembelea Septemba 13 ingawa njia ya kupeleka umeme kwenye eneo hilo zilizimwa kwa sababu ya matengenezo mafupi, kama walivyosema Tanesco, hivyo kuwafanya watu hao wasionyeshwe teknolojia hiyo, zaidi ya kushuhudia mitambo ya aina mbalimbali iliyofungwa katika chuo hicho.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment