Pages

Pages

Tuesday, October 30, 2012

UVCCM wamemeza yai la kuchemsha

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

UVCCM wamemeza yai la kuchemsha. Tabu yake ni kwamba, hadi lipasuke tumboni linahitaji kudra za aina yake. Kwa wadudu kama vile kinyonga, nyoka na kenge wanajua jinsi mayai ya kuchemsha yanavyowasumbua viumbe hao.

Kule kwetu kijijini, tulikuwa tunamchemshia mayai nyoka mwenye kawaida ya kuja kula  mayai ya kuku wetu, kama njia ya kumnasa mtegoni.

                                      Mwenyekiti mpya wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis
Lakini anajisumbua. Kwani mayai hayo hayawezi kabisa kupasuka, hivyo kusababisha kifo chake kwa uroho wake. Ndivyo ninavyoifananisha jumuiya ya vijana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), UVCCM.

Jumuiya hiyo wajumbe wake wote wamemeza yai la kuchemsha. Sasa wanahangaika kupasua, jambo ambalo ni aghalabu kutimiza nia yao. Jumuiya hiyo waliingia kwenye uchaguzi wao mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.

Wao kwa ridhaa yao, wamemuweka madarakani Mwenyekiti wao, Sadifa Juma Khamis na Makamu Mwenyekiti Mboni Mhita na wajumbe sita wa NEC, walioshinda katika Uchaguzi huo uliokuwa na joto la aina yake.

Ni upuzi tu. Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, baadhi ya wanachama wa CCM, wanaanza kukataa matokeo au kumpa mwenyekiti wao wa Taifa, Jakaya Mrisho Kikwete saa 24 kutengua matokeo hayo badala ya siku 14 kama kanuzi za chama zinavyojieleza.

Malalamiko yao ni rushwa iliyotumika kwa ajili ya kuwapa ushindi Khamis na Mboni, jambo linalowashangaza wengi. Wanajiuliza, hivi hawa wanaolalamikia rushwa, nao walipokea au walikataa?

Kama waliipokea, wamesahau kila mla cha mwenziwe na chake pia huliwa? Hivi hawa waliopiga kura, walishindwaje kuwakacha wagombea watoa rushwa? Hivi kama kweli rushwa imetumika, watoaji na wapokeaji hawaoni kama wana kesi ya kujibu?

Haya malalamiko ya wapiga kura, wanaosema rushwa imetumika, hawaoni wanajishushia heshima mbele ya jamii, maana hawautaki uamuzi wao? Ngoja niwe mkweli.

Naichukia sana rushwa. Lakini ni zaidi ninavyouchukia unafiki, uzandiki na siasa za mihemko zinazofanywa na baadhi yao. Woliopiga kura UVCCM, wanawezaje kulalamika wakati wao ndio chanzo cha mzozo huo?

Kinacholalamikiwa hapo ni utoaji wa rushwa, ambao siku zote umekuwa ukikemewa na kila mtu, ingawa baadhi yao hawaeleweki kichwa wala mguu.

Hata Kikwete, alizungumzia hilo kwa chaguzi zote za chama hicho, wakiwamo mama zao, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na UVCCM saa chache kabla ya uchaguzi huo.

Ningeweza kukubaliana na UVCCM kama malalamiko yao ni upinduaji wa matokeo, lakini si kura zilizopigwa na kuhesabiwa. Kinachofanywa sasa, ni kukipasua CCM chama hicho kikongwe chenye heshima kubwa mtaani.

Kwanini nasema hivyo? Kama watu wanapita mitaani wakilalamikia rushwa isiyochukuliwa hatua kila siku, hayo ni matusi ya CCM. Hivyo basi, baadhi ya vijana hao kusema kuwa wataandamana au kurudisha kadi nayo ni hujuma ya chama.

Jibu linalokuja hapa, vijana hao wamedhamiria kuiangusha CCM, waliojigamba kwamba wanaipenda na ipo moyoni. Waliosema kuwa watafuata miiko yote ya uongozi wa chama hicho. Waliosema kuwa hawatatoa wala kupokea rushwa.

Waliosema kuwa binadamu wote ni sawa. Huu ni wizi na uongo wa kisiasa. Kila anayetaka kupinga hayo matokeo ya Sadifa na Mboni wajitazame upya. Malalamiko na vilio vyao ni kukipaka matope chama chao.

Kama wao wanasema hivyo, waliokuwa nje ya CCM nao waseme nini? CCM ndio inayoongoza dola, kwanini washindwe kukemea kwa vitendo rushwa kwa kuwakamata watoaji na wapokeaji wanaosemwa mchana na usiku?

Hivi kweli rushwa inayotumika chooni, watu wanashindwaje kuidhibiti? Ndio maana nimesema hapo mwanzo wa makala haya kuwa UVCCM wamemeza yai la kuchemsha. Na kinachofuata sasa ni kukisambaratisha chama chao.

Kitakufa. Mpasuko unaoibuka utakiua chama maana sijaona mwenye dhamira ya kweli ya kuikomboa na kuitetea kwa nguvu zote CCM inayobanwa na ufisadi na uzandiki wa watu wake wenye nyuso mbili kwa wakati mmoja.

Nilijua baada ya uchaguzi huo, kila mtu avunje kundi lake kwa ajili ya kuijenga CCM imara, yenye nguvu na dhamira ya kushinda katika uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015, utakaowakutanisha na vyama vya upinzani vyenye matamanio ya kuongoza dola.

Vyama kama vile Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na vinavyoibuka siku hadi siku hapa nchini.

Wagombea kama vile Ally Salum Hapi, Rashid Simai Msarika, Paul Makonda, bila hata kuleta chokochoko, wangewapa ushirikiano washindi wao, maana ndio demokrasia inayotakiwa iheshimiwe na kila mmoja nchini.

Lakini kwa wafuasi wao kukataa, kulia na kulalala bila aibu, wakisema rushwa imetamalaki ni kujisumbua wenyewe. Hakuna anayewasikiliza. Jamii itawacheka na kuwadharau kwa kiasi kikubwa, ukizingatia wao ndio waliosababisha matokeo hayo.

Wao ndio tatizo na unafiki wao. Umepiga kura mwenyewe kwa kumchagua mtu wako, halafu unabadilika kama kinyonga na kupinga matokeo kama ishara ya kujikomba bila kujua kuwa unatangaza ujuha wako kwake.

Kila aliyeshindwa katika uchaguzi wa UVCCM, lazima ajuwe hakubaliki, hata kama wanakuja baada ya uchaguzi na kukushawishi upinge matokeo hayo, wakisema rushwa imetumika.

Sawa imetumika rushwa. Je, nao walipewa ikawabadilisha mapenzi yao kwako, wakati walikuimbia nyimbo nzuri, kubebeba kwenye kampeni za uwazi, ikiwamo mitandao ya kijamii wakisema wewe ni zaidi ya unaoshindana nao na chumba cha uchaguzi wakakumwaga?

Huo ndio ukweli. UVCCM na watu wote ndani ya CCM wabadilike kwa ajili ya kujenga chama chao kinachoyumbishwa na vyama vya upinzani kwa kuleta amani, mshikamano wa kweli usiyoyumbishwa na chochote.

Kulalama hakujengi. Ufa ni hatari kwa  maisha ya chama, hasa kama watu wana lengo la kuiweka madarakani CCM 2015, ukizingatia kwamba kinachofanyika sasa, sio sahihi na kuja haja ya kuweka mikakati imara kwa watu wote.

Nasema hili kama njia ya kuwafanya wale wenye mtazamo tofauti wajiangalie mara mbili na kukumbuka kuwa wakati anapiga kura, hakushikiwa bastola. Alimpigia kura aliyemhitaji kwa mapenzi yake, hivyo kulalama leo ni ujinga.

Hivyo kulia lia, kujivuta vuta ni dalili kuwa yai la kuchemsha walililomeza linashindwa kupasuka na huenda likasababisha vifo vyao. Kwakuwa wao ni binadamu, kuna njia ya kufanyiwa upasuaji kulitoa yai hilo ili wanusuru maisha yao.

Upasuaji ninaosema mimi ni mazungumzo, maridhiano kuwa waliyoshinda, wamewekwa madarakani na wao wenyewe, hivyo hakuna haja ya kuwachukia, kuwaona vituko katika mitaa yetu, au vikao vyetu tunapokutana.

UVCCM na wote ndani ya CCM wawe kitu kimoja na kuwapa ushirikiano watu waliowachagua na wala sio kuchekea ujinga wao.

UVCCM wajiulize mara mbili, wanawezaje kuwashinda jumuiya kama yao, Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), chini ya John Heche na wengineo wanaoviweka juu vyama vyao vya siasa.

CCM lazima ijuwe nini mustakabali wao. Kuchekea ujinga wa vijana wao wanaopinga matokeo hayo, au kuwanyamazisha na kuwataka wawe kitu kimoja kwa ajili ya kuijenga CCM yenye kuzinduka toka usingizini.

Kuijenga CCM yenye kila zuri la kujivunia mbele ya wanachama wake wapya na wa zamani, ili wavune katika Uchaguzi Mkuu, wakimaliza vita yao ya urais inayoendelea kuwasumbua wenye kujua wana haki ya kuziweka sawa kambi zao.

Nasema hili kwa mapenzi makubwa na siasa za Tanzania, maana kichefuchefu cha vijana kitaendelea na kukiangusha chama chao, wakati wamepiga kura wenyewe na kuwaweka madarakani waliowataka.

Huo ndio ukweli. Ukinichukia kwa makala haya jua wewe ni kati ya wale waliomeza yai la kuchemsha na haliwezi kupasuka kamwe zaidi ya kusababisha kifo chako au chama chako cha siasa, hasa CCM yenye heshima hapa nchini.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087


No comments:

Post a Comment