https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, October 14, 2011

TFF rekebisheni mwenendo wenu



WAKATI mwingine kusema ukweli ni jambo jema japokuwa hao wanaosemwa au kupewa ushauri huo, watajisikia tofauti kwa namna moja ama nyingine.

Inawezekana sisi ni watu wa karibu kabisa katika ufanyaji kazi huo, ila linapokuja suala la ukweli hakuna jinsi. Tuambiane tu kwa nia ya kufika pale tunapohitaji.

Jamani, kwenye ukweli siku uongo hujitenga. Hivyo hakuna haja ya kuogopana. Ni kutokana na hilo, acha niseme kuwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), chini ya Rais wake, Leodgar Tenga, tujiandaye kulia zaidi.

Katu tusijidanganye kupiga hatua kamwe. Wala tusitarajie kupanda viwango vya soka vya juu zaidi au kucheza michuano mikubwa duniani, ikiwamo Kombe la Dunia.

Tunachotakiwa sisi ni kujiandaa kulia zaidi kwa kuporomoka kwenye michezo, maana viongozi wengi wanafanya kazi zao kisiasa zaidi wakiwa na nia ya kulindana hata pale watu hao wanapoharibu na kuwakera watu.

Nikiwa kama mdau wa michezo, nitamlaumu Tenga kwakuwa ndiyo Rais, ila zaidi wa kubeba lawama hizo ni Katibu Mkuu wake, Angetile Osiah.



 Tenga kulia na Sunday Kayuni
Ndio, maana yeye ndio mtendaji mkuu wa yote japo kuwa amekuwa mwepesi mno kujitetea au kumtetea yule anayeonekana tofauti kwenye utendaji kazi wake.

Angalia mwenendo wa timu ya taifa, Taifa Stars. Ni utumbo mtupu. Kila mara kumekuwa na kasumba za hapa na pale. Klabu zinakwenda ndivyo sivyo.

Osiah bila kujua analofanya, anajichanganya zaidi kwa kumuondolea majukumu yake, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni. Eti kuboronga kote huko hakusababishwi na yeye, wakati anajua fika ufundi wote upo chini yake.

Kwa madai yake, wa kulaumiwa ni watu wengine wakiwamo wakuu wa mashindano. Jamani, kabla ya kufika huko kwenye mashindano, lazima ufundi utangulie.

Ni yeye wa kuangalia ratiba zinakwendaje ili mambo yaende vizuri. Kubadilishwa ovyo kwa mechi za ligi kuu au vitu kuingiliana kumesababishwa nay eye.

Wala sina haja ya kutoana kafara hapa, kama walivyomtoa kafara Ofisa Habari wao wa zamani, Florian Kaiajage kwenye tukio la kugoma CD ya wimbo wa Taifa, ila ukweli lazima usemwe maana baadhi ya Watanzania, hawajui wajibu wao.

Hakuna mipango kabisa TFF. Hawasimamii michakato ya kupiga hatua katika sekta ya michezo, ukiwamo mpira wa miguu, zaidi ya kukalia vyeo wasivyoviweza.

Kwa bahati mbaya au nzuri, wanaojitolea kusema ukweli huonekana tofauti katika nyuso zao na kusemwa kupita kiasi, wakijifanya wao ni miungu watu wasioweza kukosea.

Eti, ndio tatizo na watapekelekea wadhamini wawatose kwa namna moja ama nyingine. Jamani, hakuna malaika hapo. Hakuna aliyekamilika. Kukoselewa kuna maana ya kujipanga ili Taifa lipige hatua kutoka hapa lilipo.

TFF wamekosa changamoto na ari kwa wadau na wachezaji wote, kuanzia Taifa Stars na wale wanaocheza ligi. Ndio maana ligi inakosa mvuto kwa ratiba mbovu.

Mara kadhaa timu ya taifa, Taifa Stars, inakosa mechi za kujipima nguvu, kitu kinachoifanya ishindwe kupiga hatua kutokana na maandalizi yao hafifu.

Ni matatizo makubwa. Kwa timu kama hiyo isiyokuwa na jipya, inahitaji maandalizi ya uhakika na wala sio kuzima moto kama wanavyofanya sasa na kufuja fedha za walalahoi.

Ona, hawa wameanza kulinganisha uwepo wa Osiah na ule wa Fredrick Mwakalebela. Mwakalebela ni Katibu Mkuu wa zamani, aliyemaliza muda wake na kuhamia kwenye siasa.

Huko alishindwa kuingia bungeni kwa sababu anazojua mwenyewe na chama chake. Sitaki kuingia huko kwenye siasa, maana ndizo zinazoharibu mfumo wetu wa maendeleo ya michezo.

Wakati wa Mwakalebela, hakujatokea hayo yanayotokea sasa. Na hata kama yaliyotokea, basi si kwa kiwango kikubwa kama inavyokuwa sasa kiasi cha kukosa kusafiri kwa timu ya Taifa, huku klabu ikifanikiwa kwenda Sudan.

wachezaji wa Tanzania wanayecheza soka la kulipwa nje walikuwa wakiwasili kwa wakati tofauti na sasa. Hakuna mawasiliano mazuri wao na Mashirikisho mengine duniani.

Kulikuwa na mawasiliano ya uhakika. Mechi za kujipima nguvu zilikuwa za kutosha. Hali hiyo ilimfanya hata kocha wa wakati huo, Mbrazil, Marcio Maximo, afanye kazi yake vizuri.

Leo hii baadhi ya wadau wameanza kumtupia lawama kocha wa sasa wa Stars, Mdenmark, Jan Borge Poulsen. Hoja wanayo, ila pia wasisahu na ubabaishaji huu wa TFF.

Nadhani wanafanya hivyo kwasababu kocha ndiyo mwenye jukumu hilo, lakini wakati mwingine tunaweza kumuonea na kumtupia mzigo wa bure, wakati anashindwa kusimamiwa na viongozi hao wa TFF wanaojaribu kukwepa majukumu yao.

Hasaidiwi huyu. Hata akisaidiwa, wakubwa hao huangalia namna ya kupambana na wezi wa milangoni na kusahau mengine, maana nia yao ni kuingiza mapato ya kutosha.

Kwanini viongozi wasikubali kushindwa na kuweka mipango mingine? Hatuna ligi nzuri yenye ushindani.

Hatuna msingi imara wa kuendeleza vijana wadogo, bado tunaota ndoto ya kuwa na kiwango imara. TFF wa leo, wakiulizwa vijana wanaopatikana kwenye michuano ya Copa Coca-cola leo wanafanya nini hawatakuwa na jibu hilo.

Uwapi umuhimu wa kuwa na ligi hiyo? Huko wilayani kwenye vijana wengi kuna endelea na nini? Mkurugenzi wa Ufundi, Kayuni kazi zake ni zipi pale TFF?

Ziwekwe wazi ili wadau wazijuwe. Ni hapo ndipo ninapojikuta nikishindwa kuwaelewa TFF.

Najua ni kazi ngumu kusema ukweli, ila kwa hali ilivyo, Watanzania wajiandaye kulia zaidi, maana mafanikio kwetu ni ngumu na tusijidanganyane kwa hilo.

Hatuwezi kufanikiwa wakati tunafanya kazi midomoni. Ni ngumu kupiga hatua wakati sisi tunachojua ni kusawazisha kauli zinazopingwa na wadau, ili waonekane viongozi wazuri kwa jamii wakati ni uongo mtupu.

Osiah ambaye ndio mtendaji mkuu wa TFF, kazi yake imekuwa ngumu mno. Ameshindwa kuwa na ushawishi kwa wadau na upo uwezekano wa kuwapoteza hata wadhamini waliokuwapo sasa kwenye timu zetu.

Najua Osiah ni ndugu yetu ila kumuangalia anavyokwenda ni kumuharibia. Watu wanamuona. Sifa yake inazidi kupotea kwa ubabaishaji wake.

Binafsi napenda kuona anakwenda vizuri na ndio maana nakuwa muwazi kwa ufanyaji wake wa kazi. Hana jipya. Ajaribu kuangalia namna anavyoweza kujiendesha.

Kama ni mpole awe mkali zaidi. Zipo tetesi zinazodai kuwa Osiah licha ya kuwa na cheo hicho, lakini wapo watu wa chini yake wanamuendesha.

Sitaki kuliamini hilo japokuwa najua lisemwalo lipo, maana nia ni kuwekana sawa ili Tanzania ipige hatua katika sekta ya michezo, ukiwamo huo mpira wa miguu.

Kwanini? Hivi kweli sisi tunakuwa watu wa kuchekelea mafanikio ya wenzetu, wakati tuna idadi kubwa ya wanamichezo waliozagaa katika wilaya mbambali.

Fanya uchunguzi utakubaliana na mimi. Huko Handeni mkoani Tanga, Iringa, Mtwara, Tarime, Morogoro na kwengineko kumejaa vipaji vya hali ya juu ila hawaendelezwi wala hawaibuliwi kutokana na mipango yenye tija na Tanzania.

Vijana hao wanakosa walau jezi za kuvaa wakati tuna TFF inayoungwa mkono na wadau wakubwa tu. Sitaki kuamini kama muda umekwisha, maana wanaweza kujirekebisha na kusonga mbele wakiacha kasumba zao.

Kwa sasa TFF hawana jipya. Viongozi wapo wapo tu kwenye viti vyao vya kuzuunguka. Kusua sua huku kukiendelea, lawama hizi ni zenu, maana wadau wanawaunga mkono.

Tatizo lipo wapi?  Siasa? Ubinafsi ama ni kuogopana? Kila mtu lazima afanye kazi yake kama inavyotakiwa. Tenga, lazima awe mkali kwa vijana wake ili mambo yaende.

Osiah lazima akubali kukosolewa na watu wakiwamo wanahabari ambao kifani ni ndugu zake kabisa. Naye ni mwanahabari hivyo uwepo wake TFF ni mafanikio kwa waandishi wote nchini wakiona mwenzao anakwenda vema.

Malalamiko mengi yamekuwa kwa vyama vingine vya michezo miaka nenda rudi maana ufanyaji kazi wao ni wa midomoni.

Faida yao wanaijua, ndio maana kila siku malalamiko yao ni fedha za maandalizi na hakuna anaewasikiliza.

Wakati huo TFF wao walitulia lakini kwa bahati mbaya sasa kibao kinaanza kuwaugeukia wao. Zindukeni nyie? Kumbushaneni wajibu wenu. Punda hawezi kwenda bila mchapo.

Binafsi nipo tayari kwa lawama maana najua siku zote sio mzigo ili mradi ujumbe wangu umewafikia.

Kwa mwendo huu wa TFF, kikweli maendeleo ya soka ni ndoto ya kuku kutamani kunyonyesha watoto wake.

Naomba kutoa hoja waungwana.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...