Pages

Pages

Friday, September 30, 2011

Bongo fleva zindukeni usingizini





Msanii wa Bongo Fleva, Bob Junior akiwa katika pozi. Huyu ni miongoni mwa wasanii wanaofanya vema mno katika ulingo huo wa muziki wa vijana na unaopendwa mno.

 
TANZANIA inaweza kupiga hatua kama wote wanaojihusisha katika sanaa watahamasika na kufanya sanaa ya ndani na si kupapukia zile za tamaduni za wenzao, wakiwamo Wamarekani.

Nawazungumzia wakina Jeniffer Lopez, Rihannah, Mac Anthon, Jay Z na wakali wengine wa huko wanaokula raha nyingi kutokana na kazi zao kukubalika duniani kote.

Wasanii wanaowika nchini kama watajaribu kuingiza muziki wa Tanzania zaidi, hasa ngoma zao za makabila, kama vile Wazigua, Wasambaa, Wamakonde huwenda mambo yakawa mazuri.

Vijana wale wanaoona hawawezi kuishi bila kufanya sanaa, hapana shaka huu ni wakati wao kuingia zaidi kulitumikia Taifa lao kwa kuhakikisha sauti zao zinaitangaza nchi yao .

Nasema hivyo huku nikifahamu kasumba ya Watanzania kwa siku za hivi karibuni kutoipenda zaidi nchi yao . Hata wasanii wetu nao wamo kwenye mkumbo huo.

Wananchi sasa hawana cha kufaidika kutoka kwa wasanii. Kila msanii anaona ni vema kuimba muziki wa Kimarekani, eti anajua hiyo ndio njia yake ya kuwika kimataifa.

Kwa bahati mbaya wanashindwa kutambua kuwa hiyo siyo njia ya kumfanya Ludacriss awatambuwe. Mimi ni miongoni mwa waandishi wachache waliofanikiwa kusikiliza wasanii nyota wa Kimarekani, akiwamo Ludacriss aliyekuja hivi karibuni.

Msanii huyo alisema kuwa Bongo fleva haijui ni kitu gani duniani. Hata hivyo msanii Shaggy naye alisema maneno kama hayo, kuashiria kuwa kazi bado ipo.

Vipi wanaweza kufika huko walipokuwa wenzao? Hayo ni maswali ambayo majibu yake ni mepesi kuliko maswali. Yani kuuliza vipi wasanii wa Tanzania wanaweza kufanikiwa ni ngumu kuliko majibu yake.

Utashangaa, ila utaelewa ninachomaanisha. Angalia, japo kuwa Shaggy hautambui muziki wa Tanzania , hasa huo wa Bongo Fleva, ila aliposhuhudia Wasukuma, Wanyamwezi wanacheza ngoma zao za asili katika Uwanja wa Bujora, aliinuka na kucheza.

Alishangaa kwa mengi kutokana na wakazi hao wa jiji la Mwanza walivyoweza kudumisha ngoma za asili. Ni kutokana na hilo , nathubutu kusema Shaggy, amerudi kwao na wazo la ngoma za kabila ya Wasukuma na Wanyamwezi na sio Bongo fleva.

Hata kama hutaki ila huo ndio ukweli. Huu ni wakati wa wasanii na wadau wote tukazinduka na kufanya kazi zetu kwa minajiri ya kukuza utamaduni wetu maana ndio wenye soko.

Shabiki wa muziki wa Hip Hop ya Kimarekani hawezi kupoteza muda wake kukaa na kumuangalia msanii wa Tanzania . Ana kitu gani kipya? Si bora ananunuwe CD ya wasanii wao wa huko wenye soko hata wale waliotangulia mbele ya haki?

Hakuna kufichana hapa. Ni bora tuambiane ili tujifunze. Sio siri, nilikuwapo jijini Mwanza, wakati Shaggy ametembelea huko hasa kwenye tamasha la Fiesta 2011.

Sijamuona akitikisa hata kichwa chake kuonyesha kwamba amekoshwa na msanii kama vile Prof Jay, Fid Q, Roma, Mataruma, Barnabas na wengineo waliokuwapo uwanjani pale.

Shoo hii ilifanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, Juni 25 na kuhudhuliwa na mashabiki wengi mno.

Wakati pale ameshindwa kuguswa na muziki huo wa ‘mikono juu’, muda mchache uliopita alipagawishwa na ngoma za makabila, hivyo kuonyesha kuwa ngoma za makabila zinaweza kuwaletea mafanikio vijana hao na kukuza utamaduni wan chi.

Kwa bahati mbaya Watanzania siku hizi kama tumerogwa. Ukisema ukweli huna thamani machoni mwao wala midomoni mwao. San asana watakusema kwa mabaya, hata kama lengo lako halikuwa baya.

Hakuna haja ya kulambana kisogo hapa. Kwa wale waliokuwapo kwenye tasniaa ya sanaa, waingize japo ngoma za makabila yao waone utamu wao.

Hata kama sio kwa albamu nzima, ila wanaweza kuimba hata nyimbo moja au mbili, ili wanapofanikiwa kupata shoo za kimataifa, waimbe mbele ya watu walioingia kwa ajili yake.

Waswahili wamesema kila muomba chumvi, huombea chungu chake. Kwa msanii wa Tanzania kuzidi kutumbia katika muziki wa nje ni kujimaliza mwenyewe.

Kila kitu kinawezekana kinachotakiwa hapo ni kutimiza wajibu wetu. Angalia Makhirikiri kutoka Botswana . Hawa wasanii wanaimba muziki na ngoma za kwao. Lakini wanawika na kuvuma mno.

Hivyo hata hawa wanaoimba Tanzania lazima wafuate nyayo za wengine, hasa wale wanaoimba ngoma za asili yao , namzungumzia, Costar Siboka, Wanne Star na wengineo.

Huo ndio ukweli, maana waswahili wamesema ‘kijua ndio hichi, msipounika mtaula wa chuya kwa uvivu wa kuchagua’.

Jumamosi Njema

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment