Pages

Pages

Thursday, November 10, 2016

Madarasa matatu ya Bayport kwa EOTF yamkuna DC wa Kibaha


Mkuu wa Wilaya Kibaha, Mheshimiwa Assumpter Mshama, akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya makabidhiano ya majengo ya madarasa matatu yaliyojengwa na Taasisi ya Bayport Financial Services kwa ajili ya Kituo cha Kibaha Children Village Centre jana, wilayani humo.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa wilaya Kibaha, mkoani Pwani, Mheshimiwa Assumpter Mshama, amekunwa na majengo ya madarasa matatu ya kisasa na ofisi ya walimu yaliyojengwa na Taasisi ya Kifedha ya Bayport Financial Services, kwa ajili ya msaada wa kituo cha kulea watoto yatima cha Kibaha Children Village Centre (KCVC) chenye mpango wa kuanzisha shule.
Mkurugenzi Mkuu wa Bayport Financial Services, John Mbaga  akizungumza katika halfa ya kukabidhi majengo iliyojenga kwa ajili ya kituo cha KCVC.

Majengo hayo yaliyojengwa wilayani Kibaha, yamekabidhiwa jana na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo DC Kibaha, aliyeambatana na watumishi kadhaa wa ofisi yake na wale waliotoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Pwani wanaohusiana na elimu.
Watoto wa Kituo cha Watoto yatima cha KCVC wakiimba.
Akizungumza jana katika makabidhiano hayo yaliyopokewa kwa furaha, DC Mshama, alisema hajatarajia kwamba angekuta majengo bora na yenye kuvutia maalum kwa watoto yatima na wale watakaofanikiwa kusoma katika kituo hicho, hususan wale wanaotoka maeneo ya karibu na kituo hicho.

Alisema kwamba Bayport wamefanya mambo ya kiungwana na yanapaswa kuungwa mkono na taasisi zote ili kuhakikisha watoto yatima na Watanzania kwa ujumla wanaishi vizuri kwa kupata haki zao za msingi.
Mkuu wa wilaya  ya  Kibaha Mh Assumpter Mshama kushoto, akishiriki katika tukio la ukataji utepe kama ishara ya Bayport kukabidhi majengo iliyojenga kwa kituo cha KCVC. Kulia ni Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa.

“Nimeshangazwa na majengo haya kutokana uzuri wake na hakika Bayport nawapongeza kwa kujitoa kwenu katika kujenga jamii bora na hakika huduma zenu za mikopo ziendelee mbele maana mnaonesha dhamira ya kuwakwamua wana jamii wenzenu,” alisema DC Mshama.
Naye Mkurugenzi  Mkuu wa Bayport Financial Services, John Mbaga, alisema kwamba ujenzi wa madarasa hayo ni harakati zao za kusaidia jamii katika mambo mbalimbali ikiwamo elimu.

Alisema ujenzi wao umegharimu zaidi ya Sh Milioni 200 maalum kwa ajili ya kituo hicho cha watoto yatima, ambapo ni mwendelezo wa kuhakikisha Bayport inakuwa na tija kwa Watanzania wote bila kuwabagua kwa namna yoyote, ukizingatia kuwa taasisi yao inahudumia watu wote kwa kupitia mikopo ya fedha kwa watumishi wa umma na kampuni zilizoidhinishwa.

“Bayport tuna furaha kubwa mno kuona leo tunatimiza ahadi yetu kwa kukabidhi majengo haya ya kisasa na yanayoweza kuwasaidia watoto wetu kwa namna moja ama nyingine, hivyo wote tunafarijika kwa kufanikisha ndoto yetu na kila mmoja anajionea jinsi tulivyojenga kwa ubora wa hali ya juu,” alisema Mbaga.

Naye Mlezi wa Kituo hicho, mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa, aliwashukuru Bayport na menejimenti yote kwa kufanyia kazi wazo la kuwasaidia watoto wa kituo chao kuwajengea majengo ya madarasa matatu, ambapo utakaosaidia jamii.

“Unaweza kuwa na kitu kikubwa bila kupenda kujitolea kwa jamii, ila kwa wenzetu wa Bayport wamejitoa kwa hali na mali ili kusaidiana kuboresha makazi ya watoto wa kituo chetu maana endapo wazo la kuanzisha shule litakamilika, litanufaisha wengi,” Alisema Mama Anna Mkapa na kuwataka Bayport waendelee kujitolea kusaidia jamii.


Makabidhiano ya majengo hayo yameenda sambamba na taasisi hiyo kusherehekea miaka 10 ya huduma tangu walipoanzishwa nchini Tanzania kwa ajili ya kutoa huduma za mikopo ya fedha ambapo mpaka sasa wana matawi 82 katika wilaya na mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Mlezi kituo  hicho mama Anna Mkapa akitoa hotuba kwa wageni waalikwa. 
Mkuu wa  wilaya  ya  Kibaha  mh Asumta  Mshama akiongea na  wageni  waalikwa  katika  hafla ya uzinduzi  wa kituo cha KCVC.

No comments:

Post a Comment