Pages

Pages

Saturday, July 09, 2016

Ninachokifahamu kuhusu ubunifu na wabunifu Tanzania

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWEZI January mwaka 2011 nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu, Ahmad Ally ‘Madee’. Madee ni msanii wa muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva, akipatikana katika kundi la Tip Top ‘Connection’. Madee hakunipigia kunipa habari za kisanaa, ila jinsi anavyomjua kijana mwenye kipaji cha ubunifu wa vitu mbalimbali. Kijana huyo anaitwa Ally Bundu. Wakati huo alikuwa amebuni kifaa kinachojulikana kama simu ya kifuu cha nazi.
 Kijana wa Kitanzania mwenye kipaji cha ubunifu, Ally Bundu, akionyesha moja ya vifaa anavyobuni kila siku kama sehemu ya kuonyesha kipaji chake. Bundu pia alibuni simu ya kifuu cha nazi.

Ni kweli ilikuwa simu ya kifuu cha nazi. Ilikuwa imebuniwa barabara, ikiunganishwa na waya zisizokuwa na idadi ndani yake na ikiingia na kutoka pindi inapopigwa simu hiyo. Baada ya mazungumzo yetu mimi na Madee, nikaafiki wazo la kijana huyo aliyebuni simu hiyo ya kifuu cha nazi kuonana na mimi. Nikiwa na hamu ya kujionea simu hiyo. Siku iliyofuata nikakutana na Bundu katika ofisi yetu ya New Habari 2006 Ltd, kampuni inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Rai, Dimba na The African.
Kambi Mbwana kushoto akiangalia simu ya kifuu cha nazi kutoka kwa mbunifu wake, Ally Bundu kulia.

Baada ya kumuona kijana huyo mwenye sura ya kisanaa ya ubunifu haswa, anayeonekana kujawa na vipawa hivyo vya kubuni, nikaiepeleka akili yangu kwenye kumpyuta  kwa ajili ya kuandika kile nilichoshuhudia kutoka kwa Bundu. Baada ya kumaliza kuandika makala yale, ikapata fursa ya kutumika kwenye gazeti la Mtanzania. Naweza kusema ni miongoni mwa makala au maandiko yangu kadha wa kadha yaliyokuwa na mwendelezo ulionisisimua sana. Siku siku chache baadaye, nakumbuka nilikuwa kwenye mgahawa wa Best Bite, Morocco, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, nikipunguza mawazo na kuzungumza na jamaa zangu kadha wa kadha, ghafla nikaona simu yangu inaita. Namba ilikuwa ngeni
na haijanishtua zaidi ya kuiwaza ilikuwa inatokea wapi? Ilikuwa ni namba ya ofisini.
Simu ya kifuu cha nazi iliyobuniwa na Ally Bundu inavyoonekana pichani.
Bila wasiwasi nikaipokea, nikiwa na wazo labda ilikuwa ni simu ya mwaliko kutoka kwenye moja ya maofisi yaliyopo jijini Dar es Salaam. Sikujidanganya. Ni kweli ilikuwa ni simu ya ofisini, ijapokuwa haikuwa na lengo la kunialika kama nilivyodhani wakati ule. Simu ile ilikuwa inatoka kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, wakati huo ipo chini ya RC wake, William Lukuvi, ambaye sasa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Baada ya kupokea na kusalimia kama ilivyokuwa kawaida, yule dada akaniomba nisikate simu, maana alikuwa ananiunganisha na Mkuu wa Mkoa, yani Mheshimiwa Lukuvi.
Kweli nikafanya hivyo, lakini wakati huo nikawa na hofu kidogo. Sikuelewa kwanini Mheshimiwa Lukuvi alikuwa anataka kuzungumza na mimi. Wakati huo sikuwa na mwingiliano wowote wa wanasiasa, ijapokuwa nilikuwa nafuatilia siasa za ndani ya nchi na nje pia.

Baada ya kuunganishwa na mheshimiwa Lukuvi, nakumbuka alichoniambia mheshimiwa yule ni kuniita ofisini kwake, akisema kuna jambo anataka tukalijadili. Nikakubali na kuahidiana siku inayofuata saa nne asubuhi ningekuwa ofisini kwake. Nilipomaliza kuongea na simu na mheshimiwa Lukuvi, nikainuka kuelekea ofisini, yani Sinza Kijiweni Makao Makuu ya kampuni ya New Habari. Kufika tu, nikakutana na mkuu, Manyerere Jackton. Kamanda Manyerere alikuwa ni mmoja wa wahariri kwenye gazeti la Mtanzania.  

Akanieleza kwamba wamepokea simu kutoka kwa RC Lukuvi, akitaka mawasiliano yangu. Nikamjibu ni kweli, amenipigia, nimezungumza naye. Akanipongeza na kunitaka nifike ofisini kwake kusikiliza agenda anayoniitia huko. Nakumbuka kauli ya bosi wangu Manyerere ni kwamba; “Nisiende kama mwanamichezo,”. Nilimuelewa, alimaanisha nisiende na t-shirt na jinsi au fulana kama tulivyozoea katika viwanja mbalimbali vya michezo au kwenye kumbi za starehe. Si unajua tena wanaoandika habari za michezo na burudani.

Siku iliyofuata saa nne asubuhi ilinikuta Ilala, ndani ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam. Safari za ahadi zina raha yake. Sijasubiri mapokezi wala kujieleza sana, isipokuwa nilipotaja jina langu, nilipelekwa moja kwa moja hadi kwa RC Lukuvi. Baada ya salamu, RC Lukuvi alinipongeza sana. Ni juu ya makala ya yule kijana aliyebuni simu ya kifuu cha nazi. “Makala yako uliyoandika inasisimua na umefanya kazi nzuri sana. Badala ya kuandika siasa chafu, wewe umezama kwenye mambo yanayohusu jamii, ni jambo la kusisimua, hongera,” alisema RC Lukuvi na kuwaita baadhi ya wataalamu wake, akiwamo bwana ambaye siwezi kumkumbuka kwa jina, wakati huo ni afisa elimu wa mkoa, tukaketi naye kwenye kikao chetu. RC Lukuvi alitaka kujua kama kijana huyo yupo? Anaishi sehemu gani? Mimi nimemjua vipi? Baada ya mazungumzo mafupi, hatimae RC Lukuvi akanipa gari la ofisi yake na dereva kwa ajili ya kumsaka yule Bundu, aliyebuni simu ya kifuu cha nazi.

Safari yangu ikaanza. Nimefunga mkanda kwenye gari kubwa na zuri la serikali. Naweza kusema wakati ule niliifaidi sana kodi yangu. Safari yangu iligotea Manzese Tip Top, nikimsaka Bundu. Nikamkuta amezungukwa na watu, akiendelea na shughuli zake binafsi. Baada ya kuzungumza naye, alifurahi na kunipongeza pia. Bundu alisema amekuwa akipokea simu nyingi za pongezi. Na nzuri zaidi, amekuwa akiitwa kwenye mahojiano na redio na tv mbalimbali. Nikamwambia Bundu ajiandaye twende kwa mheshimiwa Lukuvi. Kweli tukafika kwa RC Lukuvi. Nikimfikisha yule kijana, ndipo kikao chetu kikaendelea na kupatikana majibu kwamba serikali ilikuwa imeamua kumsaidia Bundu katika majukumu yake. Siku iliyofuata tulifika Chuo cha VETA Chang’ombe tukiwa watu kadhaa. VETA nao walipokea agizo la RC, maana waliombwa watafute namna ya kumuwezesha Bundu. Majibu yalipatikana kwamba VETA wamtengee somo maalum la kumwendeleza yule mbunifu wa simu ya kifuu cha nazi bila kuangalia changamoto ya kiwango chake cha elimu.

Baada ya VETA kukamilisha mchakato wao, ndipo nilipokuja kugundua kwamba agizo la kumsaidia Bundu limetokea ngazi za juu kabisa na likiratibiwa na ofisi ya mke wa rais mstaafu, Mheshimiwa mama Salma Kikwete. Kwamba kusudio pekee lilikuwa kumwendeleza Bundu. Na mwenyewe alikuwa na ndoto za kuendelea na aliona dalili zote. Kwa sababu nilishatimiza wajibu wangu, nikaacha kuongozana na Bundu, wakati huo nilishaingia na kutoka katika ofisi kadhaa, ikiwamo WAMA nk. Lengo lilikuwa ni kuendelea na shughuli zangu. Nasikitika kwamba yule kijana akaanza kutembea nenda rudi, akizunguushwa bila mafanikio. Anazunguushwaje? Mbona kila kitu kilishakamilika? Yule kijana akanifikishia taarifa za kusikitisha, akisema anaona ndoto zake zinatoweshwa. Baada ya kuchunguza, nikagundua ni kweli, watu waliokabidhiwa suala hilo wanamuonea mtima nyongo, hawataki afanikiwe katika maisha ya ubunifu ambao ndio jambo nyeti duniani kote.

Hadithi hii inaweza kuendelea kutwa hata kujaza kitabu, ila ni muhimu kubaini kuwa nchi hii ina vijana wengi wenye vipaji. Vipaji ambavyo kama wangezaliwa katika mataifa mengine, huenda sisi Watanzania tungezibabaikia bidhaa zao. Huu ndio ujinga wa karne. Bundu alikuwa na uwezo wa kuzalisha kwa wingi simu ya kifuu cha nazi. Hata kama tusingeweza kutembea nazo mifukoni, lakini majumbani, maofisini na pengine kwenye mahoteli na maeneo mengine, zingefaa. Kama kweli Bundu alikwamishwa na baadhi ya watu hao nab ado watu hao wapo, nchi yetu haiwezi kupiga hatua. Kila tunachokibabaikia kutoka nje ya nchi, lazima tujue ni ubunifu na ni vipaji vya watu. Sio simu, magari, ndege na nk. Tena ubunifu au ugunduzi una changamoto nyingi. Kinachotakiwa ni kuweka mfumo mzuri ili kuendeleza vijana wetu. Tunavyo vyuo kibao vya ufundi. Tunapoona mwangaza wa kipaji cha kijana yoyote, anapaswa kushikwa na serikali, ili asimamiwe na kumwendeleza katika mambo yake kwa faida ya nchi husika. Wasomeshwe.

Nimeamua kuandika haya baada ya kuona mengi juu ya wabunifu yanasemwa. Kwanza ni mbunifu wa helikopta huko mkoani Mbeya na wengineo wanaosikika kila siku. Binafsi naunga mkono vijana wanaohangaika kubuni vitu vyao. Ni jambo la msingi. Nchi yetu itasonga mbele kama vijana hao wataibuka kwa wingi na pengine kuendelea. Hatuwezi kununua hata vijiti vya kutolea uchafu kwenye meno kutoka China, Kenya na kwingineko. Hata matoi ya kuchezea watoto yanatoka nje, huu ni ujinga na unaosababishwa na sisi wenyewe wana jamii.Utawala huu wa kazi uwe na dhamira chanya kwa wenye vipaji vyao. Na lazima tufahamu kwamba wenye vipaji wengi elimu zao zinakuwa za kawaida au wasiwe na elimu kabisa. Lakini mwenye kipaji mmoja ni sawa na wenye degree 100 waliosomea tu vitu kwa kupitia makaratasi na vyeti. Basi tuwachanganye nao. Tuchukuwe wenye vipaji ama wabunifu wanaotokea pembe zote za nchi na kuwachanganya na wanaoitwa wasomi wetu vyuo vikuu na katika vyuo vingine vya ufundi. Tuache dharau na kejeli.  Ingawa wapo wanaowadhihaki wabunifu hao, lakini wanapaswa kujua ndio mwanzo.

Leo wanabuni teknolojia ambazo si ngeni, ila kuna siku watatoa bidhaa ambazo ni ngeni hivyo taifa litavuna kutoka kwenye vichwa vyao. Na sisi tunaoishi na vijana hao tuwape moyo. Tuwasaidie au kushirikiana nao kwa hali na mali. Ikitokea tunao uwezo wa kuwaendeleza tufanye hivyo. Endapo Bundu angekuwa amesaidiwa kama ilivyotarajiwa hapo mwanzo, huenda leo hii kipaji chake kingekuwa mara dufu. Huo ndio ukweli. Na kwa nchi yetu ilipotokea, huenda serikali ilifanya kama ilivyotaka kwa Bundu, ila msaada huo haujafika kwa mlengwa. Pengine yupo Bundu mwingine anayenufaika na msaada wa mama Kikwete ama serikali ya mzee Jakaya Kikwete mwenyewe, ambao tumeshuhudia mara kadhaa wakijishusha na kutaka kusaidia jamii mbalimbali katika mambo kadhaa.

Natamani kufika VETA nitafute kumbukumbu za kijana huyu Bundu. Lakini pia nifike WAMA au kumuuliza mheshimiwa Lukuvi kama anakumbuka juhudi alizofanya juu ya kijana yule wa Manzese aliyeingiza namba zake kwenye simu hiyo ya kifuu cha nazi na ikaita kama zinavyoita simu nyingine tunazotumia?
Nasikia Bundu anaendelea na ubunifu wake licha ya kuzaliwa kwenye Taifa linalowekeza kwenye ununuaji wa bidhaa za Mataifa ya nje na kuacha bidhaa za Tanzania. Naumia zaidi kuona nilitaabika juu ya kumuibua Bundu na kuishia njiani. Lakini pia wapo akina Bundu kila mahali wakipambana kuibua vipaji vyao na hakuna chochote kinachotokea. Serikali ipo. Diwani na wenyeviti wa mitaa wapo ambao huenda wanawaona kama vikatuni vinavyopoteza muda. Tulivyokuwa wajinga, ukitangaza unatibu ugonjwa ukimwi, vidonda vya tumbo, nguvu za kiume, hata kama sio kweli utaona wanamiminika kwako. Kumbe! Tanzania ni taifa la wagonjwa! Wagonjwa wa mwili na baadhi yao sasa ugonjwa huo umehamia kwenye vichwa vyetu, hatuoni sasa tunadharau na kudhihaki wenye vipaji, wagunduzi na wabunifu.

Bundu asichoke kubuni na akipata muda zaidi ajaribu kubuni vitu vinavyoweza kurahisisha suala la kilimo huku kwetu Handeni, mkoani Tanga atakuwa na soko kubwa, kuliko huko Dar es Salaam kwenye watu wanaowekeza zaidi habari zisizokuwa na tija.
+255 712053949

No comments:

Post a Comment