Pages

Pages

Saturday, December 26, 2015

Ridhiwani Kikwete avunja ukimya

RIDHIWANI KIKWETE AAMUA KUFUNGUKA ..
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Ndugu zangu waandishi wa habari, nimeamua kuwaita ili kuzungumza nanyi kuhusu baadhi ya mambo yaliyokuwa yanasemwa katika vyombo vya habari kuhusu mimi.
Awali ya yote napenda kusema kuwa habari hizo ni UONGO mtupu, ni mambo yanayozushwa na waandishi wa habari hizo kwa nia ya kuchafua jina langu kwa sababu wanazozijua wanaoandika. UKWELI ni kwamba haya ni mambo yenye kufanywa kwa nia na dhamira mbaya dhidi yangu na hata familia yangu.
Hivi karibuni, kwa mfano, lipo gazeti moja liliandika na kutoa picha yangu na mtu mmoja waliyedai ni Mhe. Paul Makonda eti akinifunga kamba za viatu. Katika maelezo yake mwandishi akadai kuwa Mhe. Makonda alipata uteuzi kuwa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni kwa sababu hiyo. Huu ni uongo usiokuwa na hata chembe ya ukweli. Napenda watanzania wajue kuwa hakuna wakati wowote Baba yangu alipokuwa Rais wa nchi yetu alinihusisha kwa namna yeyote ile katika uteuzi wa mtu yeyote katika Serikali. Hivyo basi kujaribu kunihusisha na uteuzi wa Mhe. Paul Makonda kuwa Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni ni jambo lisilokuwa na ukweli wowote.
Pili, Yule mtu anae onekana katika ile picha siyo Mhe. Paulo Makonda bali ni Bwana Deogratius Kessy anayefanya kazi katika kampuni ya ushonaji na mavazi ya Bwana Sheria Ngowi. Nilishona safari suti kwenye kampuni hiyo. Nilipokwenda kuchukua nguo yangu na nilipovaa ili kuona kama imeshonwa vizuri, Bwana Sheria Ngowi alitaka nivae viatu vya ngozi. Bahati mbaya nilikuwa nimevaa sandals hivyo akaamua kunipa viatu vya dukani kwake nivae. Wakati bwana Deogratius Kessy akinisaidia kuvaa viatu ndipo ile picha ikapigwa nampiga picha wa kampuni ya Bwana Sheria Ngowi , inashangaza na kusikitisha kuona picha hiyo inatumiwa kupotosha ukweli kwa kutoa maelezo ya uongo. Ni dhahiri kwamba mwandishi aliamua kufanya hivyo kwa maksudi mazima ya kutoa sifa mbaya kwangu na kwa Mheshimiwa Paul Makonda. Hivi ndivyo uhuru wa habari unavyostahili kutumika ?

Siku za nyuma gazeti lingine liliandika eti kuwa nilihojiwa kuhusu sakata la makontena bandarini. Napenda kuwaambia ndugu waandishi wa habari kuwa sijawahi kuhojiwa na mtu yeyote, chombo chochote au kamati yeyote kuhusu madai hayo. Ni uongo usiokuwa na ukweli wowote. Ni mambo ya kugushi na uzushi kabisa, Ninayasema maneno haya kwa kujiamini na kama mwandishi ana uthibitisho wa madai yake autoe hadharani watu wauone. Aidha, nasema kama yupo mtu aliyenihoji ajitokeze kukanusha ninayoyasema, Namtaka aseme wazi. Nawahakikishia kuwa mtu huyo hayupo na wala hatakuwepo.
Ndugu waandishi na watanzania wenzangu, inaelekea kuna mtu au genge la watu mahali Fulani ambao wameamua na kudhamiria kuchafua jina langu na la familia yangu kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Tangu Serikali ya awamu ya tano ianze jitihada za kuwabana watu wanaokwepa kulipa kodi za Serikali bandarini wapo watu wamekuwa wakifanya jitihada za kunihusisha na watu Fulani wanaotuhumiwa kuhusika na ukwepaji huo. Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakidai eti baadhi ya makontena hayo ni yangu. Na, wapo waliodai eti kuwa nimekuwa nawasaidia baadhi ya wafanyabiashara hao kukwepa kodi kwa kutoa maagizo kwa maofisa wa forodha wasiwatoze kodi inayostahili kulipwa.
Napenda kuwafahamisha kuwa sijawahi kuagiza bidhaa zozote kutoka nje hivyo sijawahi kuwa na kontena lolote ambalo nililowahi kutakiwa kulipia ushuru nikakwepa. Aidha, sijawahi kumuombea msamaha wa kutokulipa au hata kupunguziwa kodi mfanyabiashara yeyote au mtu yeyote aliyeingiza kontena nchini kutoka nchi za nje. Kama mtu ana ushahidi autoe hadharani mimi niuone na dunia iuone. Nawahakikishia ushahidi huo haupo na wala hautokuwepo. Labda uwe wa kugushi na wakifanya hivyo wataumbuka.
Napenda pia kutumia nafasi hii kusema kuwa sina na wala sijawahi kumiliki lori au basi wakati wowote katika maisha yangu. Aidha, sina hisa au ubia na mtu yeyote au kampuni yeyote ya malori au mabasi. Nayasema haya kwa sababu wapo wabaya wangu wanaoeneza maneno ya kunihusisha na kumiliki malori na mabasi. Pia kunihusisha na baadhi ya makampuni yanayomiliki na kuendesha biashara ya malori na mabasi.
Ndugu wanahabari, napenda kusema kwa kurudia na kusisitiza kuwa sina lori wala basi hata moja na sina ubia na wafanyabiashara ama makampuni yoyote yanayofanya shughuli hizo. kama yupo mtu yeyote ana ushahidi wa kuhusika kwangu auweke hadharani watu wauone. Napenda ieleweke kuwa kama ningekuwa na ubia wa namna hiyo nisingekuwa na sababu ya kuficha. Niogope kitu gani ? Ukweli ni kwamba sizuiliwi kufanya biashara kama nikipenda kufanya hivyo , Hata kwa nafasi yangu ya sasa ya uongozi yaani mbunge bado sina kizuizi. Mbona Bungeni wapo wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo. Isingekuwa ajabu kwangu kufanya biashara hivi sasa mimi pamoja na kuwa mbunge ni mwanasheria wa kujitegemea na nimeiweka katika TAMKO langu la mali na madeni la viongozi kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi.
Nimewavumilia sana lakini sasa nimechoka, nimeona leo nivunje ukimya. Nimeona niseme kidogo kwani bila ya kufanya hivyo nitaliacha genge la watu wenye nia mbaya na mimi waonekane wanasema kweli. Wahenga wanasema msema pweke hushinda! Nikiendelea kukaa kimya uongo wao utageuka kuwa ukweli dhidi yangu. Naambiwa hapa nchini siku hizi kila jengo jipya linalojengwa linasemekana ni la Ridhiwani, kituo kipya cha petrol ni cha Ridhiwan. 
Nimeanza kuona athari za uongo huo, Siku moja kuna mtu alikuja kuniomba nimpangishe katika lile jengo la PSPF pale stesheni. Nilipomuuliza nitampangishaje akasema mbona watu wamemwambia ni jengo langu!? Siku nyingine nikakutana na jamaa mmoja mwenye asili ya kiasia akiwa anahema. Akasema ananiomba sana niache kutaka kupora kampuni yake,nikamuuliza kampuni gani hiyo? Na kwanini anasema hivyo? Akanijibu, anasikia wakisema kampuni yake ni ya ridhiwani wakati kampuni hiyo hata yeye kairithi kwa baba yake na yeye alirithi kwa baba yake zaidi ya miaka hamsini iliyopita, Nikamwambia kuwa habari hiyo si kweli, sina mpango huo na wala sina sababu ya kufanya hivyo. Hayo ni maneno yanayoenezwa na wabaya wangu walioamua kunipakazia kwa sababu wazijuazo wao. Tukaachana ,sijui kama ameamini kama sina mpango wa kumpora kampuni yake. Siku moja Mzee wangu mmoja wa kwetu kijijini alinilalamikia kuwa nina roho mbaya kwa vile sitaki kumpa kazi mwanae kwenye kampuni yangu ya malori wakati yeye ni dereva mzuri, Nilipomueleza Yule mzee kuwa sina lori hata moja akashangaa na kusema mbona watu wanasema nina malori mengi. Ndugu zangu mnaiona fitina kubwa inavyotengenezwa katika jamii kuhusu maneno haya, Wapo wanaoniona mimi FISADI, Wapo wanaoniana mimi nina Roho mbaya, Wapo wanao niona mie nataka kupora mali zao. Baada ya Baba kustaafu maneno yamekuwa mengi na yanazidi kupata kasi. kila kukicha wanazua jambo jipya. Nimeoa niyaseme haya ili watu wajue ukweli wa upande wangu.
Naomba nimalize kama nilivyoanza kwamba yanasemwa mengi lakini ni maneno ya uzandiki, uzushi na ni uongo mtupu usiokuwa na chembe ya ukweli. Wale wanaosema, kuandika, na kueneza maneno hayo wanajua kuwa wanasema UONGO, ila wanafanya hivyo kwa vile wana nia mbaya dhidi yangu na familia yangu , Naomba watanzania muyapuuze maneno hayo, naomba watanzania wenzangu muupuuze uongo huo.
siko hivyo, sina mali hizo na wala sifanyi hayo wanayodai nafanya na wala sina mpango wa kuyafanya.
Imetolewa na:-
Ridhiwan J. Kikwete
Mbunge wa Jimbo la Chalinze.

No comments:

Post a Comment