Pages

Pages

Monday, April 13, 2015

SIWEZI KUVUMILIA: Hongera Twiga Stars, wa hapa hapa wajifunze kutoka kwenu

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars wanajua nini wanachokitaka Watanzania. Wanafahamu kuwa Watanzania wamekuwa na kiu kubwa ya kushiriki au kufanya vizuri katika michuano mikubwa ikiwamo ile ya Afrika.
 

Kwa bahati mbaya, timu ya aina hiyo kwenye mpira wa miguu hamna, hususan zile timu za wanaume ambazo mara kwa mara zinaambulia patupu. Licha ya kuambulia patupu, lakini watu wamekuwa na matumaini nao, kiasi cha kuwaunga mkono mara kwa mara.

Wanajitahidi kuingia uwanjani kwa wingi au hata kumwaga udhamini wao mnono huko kwa minajiri ya kuwaunga mkono. Kwa Twiga Stars hapana. Hapa ndipo ninaposhindwa kuvumilia.

Ona sasa, Twiga Stars wamefanikiwa kufuzu michuano mikubwa ya Fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake (AWF 2015) zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Congo-Brazzavile, baada ya kuwafunga She-Polopolo kwa mabao 6-5.
Awali Twiga Stars walishinda bao 4-2 nchini Zambia na juzi Ijumaa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, walifungwa bao 3-2, hivyo Twiga kufuzu kwa kufanikiwa kupata ushindi wa bao 6-5.

Huu ni ushindi wa Watanzania wote, wakiwamo wale wanaoshindwa kuwaunga mkono akina Sophia Mwasikili, Fatuma Rashidi na wengineo wanaoitangaza vyema nchi yetu kwa kupitia soka la wanawake.

Huo ndio ukweli. Twiga Stars wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuonyesha kiu ya mafanikio ya soka, jambo linalohitaji kuigwa na kaka zao, Taifa Stars au hata timu za Tanzania.

Ikumbukwe Twiga wanafanya vizuri kwa jitihada zao. Hawana Ligi nzuri kama ilivyokuwa ile ya Vodacom. Tangu enzi za kocha wao Boniface Mkwassa hadi leo Rogasian Kaijage, wachezaji wanafanywa kuokotezwa tu kisha wanaingia kwenye timu ya Taifa.

Ni wakati huu wadau wa soka kuzidi kushangazwa na matokeo ya mabinti hawa wa Twiga Stars, ikiwezekana wawaunge mkono kwa namna moja ama nyingine ili kuwapa nguvu zaidi.

Wachezaji wa soka la wanawake wawekewe mkazo kuwaibua na kuwaendeleza zaidi na zaidi kwa maendeleo yao. Soka la wanawake liwe na dira, ikiwamo ya kuwaingizia kipato wachezaji kuliko ilivyokuwa sasa.

Kinyume cha hapo tutaishia kuangalia soka la wanaume lisilokuwa na tija kwa mechi za Kimataifa, huku wale wasioangaliwa wakisonga mbele mara kwa mara, hivyo kuwa aibu yao au aibu yetu?

Tuonane wiki ijayo
kambimbwana@yahoo.com
+255 712053949

No comments:

Post a Comment