Pages

Pages

Wednesday, April 08, 2015

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yamlilia Dr Mohamed Mhita

Hayati Dkt. Mohamed Mitha Mekuru Genzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi anasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu (mstaafu) Dkt. Mohamed Mhita kilichotokea siku ya Jumatatu tarehe 06 Aprili 2015 katika hospitali ya Agakhan jijini Dar es Salaam. 

Marehemu Dr Mohamed Mhita enzi za uhai wake, aliyesimama, aliyetarajiwa kuzikwa leo jioni wilayai Handeni, mkoani Tanga

Dkt. Mhita alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa kwa kipindi cha miaka 8 kuanzia 1992 hadi 1999 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kipindi cha miaka 9 kuanzia 1999 hadi 2008. 

Dr. Mhita kwa kushirikiana na uongozi wa iliyokuwa idara Kuu ya Hali ya Hewa alishiriki katika kuishauri Serikali kuhusu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kutoka iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa.

Pamoja na nafasi ya Mkurugenzi Mkuu pia alikuwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani kuanzia mwaka 1992 hadi 2008. Alichaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza Kuu la Shirika la Hali ya Hewa Dunia kuanzia mwaka 1995 hadi 2007.
Alichaguliwa kushika nafasi ya Rais wa Jumuiya ya Hali ya Hewa katika Bara la Afrika (RA 1) kuanzia mwaka 1998 hadi 2007. Dkt Mhita alikuwa Rais wa ‘Tanzania Meteorological Society’ sambamba na nafasi nyingine nyingi mbalimbali alizoshika ndani na nje ya nchi. 

Akielezea baadhi ya mambo makubwa yatakayomfanya Dkt. Mhita aendelee kukumbukwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Dkt. Agnes Kijazi alisema ‘Dkt. 

Mhita atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza sayansi ya hali ya hewa hapa nchini, katika Bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hususani katika ushiriki wake wa kuianzisha Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuandaa dira (vision) na dhamira (mission) ya Mamlaka kwa kipindi cha miaka kumi na tano (15) kuanzia mwaka 2000 hadi 2015’.

Dkt. Mohamed Mhita ni mmoja kati ya wanasayansi waliokuwa zao la chuo kikuu cha Stolkholm, Sweden ambako alitunukiwa shahada ya hali ya hewa (BSc. Met) mwaka 1977. Kuanzia mwaka 1981 hadi 1984 alikuwa mafunzoni katika chuo Kikuu cha Reading, Uingereza ambako alitunikiwa shahada ya uzamivu (PhD). 

Hapa nchini alipata mafunzo ya Sekondari katika shule za Tanga na Kamrimjee zote zikiwa mkoani Tanga. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inajumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki katika kuomboleza msiba huu. Innalilah Wainnailaih Rajiun. 

Imetolewa na Monica Mutoni
Afisa Mahusiano wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania


No comments:

Post a Comment