Pages

Pages

Thursday, April 09, 2015

Jamal Malinzi aitakia kheri Twiga Stars dhidi ya She-polopolo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi, ameitakia kila la kheri timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) katika mchezo wake wa kesho wa marudaino dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (She-Polopolo) utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Azungumza na wachezaji wa Twiga Star na benchi la Ufundi katika chakula cha pamoja cha mchana leo katika hosteli za TFF zilizopo Karume, Rais Malinzi amesema watanzania wote wana matumaini na timu yao kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa marudiano.

Aidha Rais Malinzi amewaambia bechi la ufundi na wachezaji wa Twiga Stars kuwa pesa zote zitakazopatikana katika mchezo wa kesho baada ya makato ya Uwanja na VAT, wagawane kwa pamoja wachezaji na viongozi.

Naye Mgeni mualikwa Ryhs Torrington ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Luninga cha Azam, alisema anaitakia kila la kheri Twiga Stars katika mchezo wao wa kesho, na kusema mechi hiyo itaonyeshwa moja kwa moja na Azamtv, hivyo waitumie vizuri nafasi hiyo kujitangaza kimataifa.

Kocha mkuu wa Twiga Stars Rogasian Kaijage na nahodha wake Sophia Mwasikili, wamewahakikishia ushindi katika mchezo wa kesho,  na kuwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kuwashangilia.

Mechi inatarajiwa kuanza majira ya saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, na tiketi za mchezo zitauzwa kesho saa 2 asubuhi eneo la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku viingilio vya mchezo huo vikiwa ni tsh. 5000 kwa VIP na tsh. 2000 kwa majukwaa yaliyobakia.

Twiga Stars ambayo katika mchezo wa awali iliibuka na ushindi wa mabao 4-2, inahitaji sare ya aina yoyote ili kuweza kufuzu kwa fainali za Michezo ya Afrika zitakazofanyika nchini Congo-Brazzavile mwezi Septemba.

No comments:

Post a Comment