Pages

Pages

Monday, March 02, 2015

SIWEZI KUVUMILIA:Kalale pema Alex Massawe, Simba haijalipa fadhira zako hata kidogo

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KWA walioanza kufuatilia mpira wa miguu Tanzania, hakika watakumbuka kile kikosi cha Mabingwa wa zamani wa Tanzania Bara, Simba SC, katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003. Kikosi imara kilichowatoa timu ngumu ya Zamalek na hatimae Watanzania hao kuingia hatua ya robo fainali na kushangaza wengi.
Marehemu Christopher Alex Massawe enzi za uhai wake.
Kabla ya kuwatoa Zamalek, timu nyingi za Tanzania, ikiwamo Yanga walikuwa wakishindwa kuzitoa  timu za Misri. Kila walipokutana inakuwa mwisho wao. Ilishazoeleka, inapotokea Yanga au Simba wanacheza na Al Ahly, Zamalek na nyinginezo za huko tunauona mwisho wetu.

Kwa mwaka huo ikawa tofauti. Na walioifanya Simba ifuzu hatua hiyo ngumu ni mchezaji Christopher Alex Massawe, ambaye amefariki wiki iliyopita mjini Dodoma, alipokuwa akiishi nyumbani kwa mama yake na kuugua kwa muda mrefu.

Massawe aliugua sana kabla ya kufariki. Na kuugua kote huko hakuna msaada wowote uliomfikia mchezaji huyo kutoka kwa timu yake ya Simba aliyoichezea kwa mapenzi makubwa. Na Massawe alishawahi kulalamikia sana hilo, akiomba viongozi na wadau wa 
Simba wamkumbuke hata kwa macho tu ili wamfariji.

Hakika siwezi kuvumilia ninaposhuhudia nyota wa mpira wa Tanzania wanavyoishi kimasikini na wasivyokumbukwa kwa mazuri yao. Hivi kweli Simba yenye neema ya rasilimali wa watu na fedha pia, wanashindwa kuwakirimu wachezaji wao?

Hii inakuwaje? Kwa wachezaji kama akina Massawe, Emmanuel Gabriel, Juma Kaseja, Selaman Matola na wengineo wote waliokuwa kwenye Simba ile kiboko ya wa Misri ilipaswa waangaliwe kwa jicho pana ili walau kuwalipa fadhira zao.

Kwa bahati mbaya wachezaji wa enzi hizo walicheza kwa mapenzi makubwa na hakukuwa na pesa nyingi. Ni tofauti na wachezaji wa leo wanaoogelea kwenye Mamilioni ya fedha. Enzi hizo wachezaji walijisikia faraja tu kuichezea Simba, Yanga au timu ya Taifa (Taifa Stars).

Kama tunashindwa kuwahudumia wakongwe japo kwa uchache tu tunaweza kuwa na maendeleo kwenye mpira wa miguu Tanzania? Simba imejaza wanachama, wapenzi na mashabiki wanaoweza kulia timu yao inapofungwa. 

Je, anajua kulia kwake kunatokana na jasho na nguvu za wachezaji wanaopambania ushindi uwanjani?

Lakini pia wanajua kuwa mara zote hao waliopambania Simba hasa katika michuano mikubwa, yenye mvuto wameishia kutupwa kama mizoga? Nakumbuka Massawe kilio chake cha mwisho ilikuwa ni kuwaomba Simba wamtembelee na kumfariji.

Aliamini viongozi wake na wadau wakimtembelea walau wanaweza hata kumnunulia dawa ya kutuliza maumivu, lakini sivyo. Hii inatia kichefuchefu. Na huenda machozi ya akina Massawe ni bakora ya kuiadhibu klabu ya Simba.

Andiko hili halina faida kwa Massawe kwasababu amekufa akiwa hajamuona hata huyo Matola, ambaye mwaka  2003 walipoitoa Zamalek alikuwa nahodha wao. Viongozi wa Simba na klabu zote zinapaswa kuweka utaratibu wa kuwatunza wakongwe wao. Ndio ubinadamu. Kinyume cha hapo siwezi kuvumilia, maana jambo hili linakera.
Tuonane wiki ijayo.
+255712053949

No comments:

Post a Comment