Pages

Pages

Monday, December 22, 2014

Kizazi kipya waliteka tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014



Na Mwandishi Wetu, Handeni
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, msimu wa pili wa tamasha la NSSF Handeni Kwetu 2014 lililofanyika katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, mkoani Tanga, Desemba 20, ulimalizika huku wasanii wa muziki wa kizazi wilayani hapa, wakiliteka tamasha hilo lenye mguso wa aina yake.

Wasanii hao wanaofanya vizuri wilayani Handeni na mkoa mzima wa Tanga, wakiongozwa na RSK Kibajaji, Diki Mani na kundi la WC, walionyesha uwezo wa juu kiasi cha kuvipoteza vikundi vya ngoma za asili vilivyokuwapo katika tamasha hilo.

Awali, wasanii hao walipangwa kama sehemu ya kunogesha tu na pia kuwapa nafasi ya kujitangaza ili wafikie malengo yao, lakini uwezo wa kuimba, ubunifu na ujuzi wa kulishambulia jukwaa kuliwafanya wasanii hao washangiliwe muda wote uwanjani hapo.

Akizungumza katika tamasha hilo, Mratibu Mkuu, Kambi Mbwana, alisema kwamba waliamua kuwaalika wasanii wa kizazi kipya ili kuwatangaza, jambo ambalo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa hasa pale vijana hao walipoweka ubunifu wa hali ya juu katika kazi zao.

“Hawa wasanii waliweza kuchanganya lugha katika mashairi yao, kuimba nyimbo zinazoelezea mazingira ya Handeni na mkoa wa Tanga, bila kusahau kuhamasisha mambo ya kimaendeleo sambamba na kuelimisha wahudhuriaji namna ya kusomesha watoto wao.

"Hii iliwafanya mashabiki, wadau na wahudhuriaji washindwe kukaa kwenye viti vyao kutokana na kazi nzuri ya wasanii hao ambao kwa kiasi kikubwa wanaonyesha vipaji na uwezo mkubwa wa kushambulia jukwaa,” alisema.

Naye mgeni rasmi katika tamasha hilo, ambaye ni Katibu Tawala wa wilaya ya Handeni, John Ticky, aliyemuwakilisha Mkuu wa wilaya Muhingo Rweyemamu, alilimwagia sifa tamasha hilo kwa hatua ya kuitangaza Handeni, sanjari na mafanikio yake kwa ujumla.

“Hili ni tamasha zuri mno maana limechanganya burudani ukizingatia kuwa sera zao zinachangia maendeleo kwa kiasi kikubwa mno, hivyo kama sehemu ya serikali naomba juhudi hizi ziendelee kwa maendeleo ya Taifa letu,”  alisema.

Nao Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF ambao ndio wadhamini wakuu wakiwakilishwa na Meneja Mkoa Tanga, Frank Maduga, alisema tamasha la Handeni Kwetu limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mkoa mzima wa Tanga, jambo linalowafanya waliunge mkono na kuwataka pia Watanzania wote wajiunge na mfumo wa hifadhi wa NSSF Tanzania, hususan wakazi wa Handeni na mkoa wa Tanga.

NSSF tunajivunia kwa kiasi kikubwa kuwa wadhamini wa tamasha hili ambalo kwa mwaka huu tumeshuhudia wananchi wakielimishwa umuhimu wa kuwa wanachama ambapo wengine walivutiwa na kujiunga moja kwa moja kwenye mfuko wetu wakati tamasha linaendelea uwanjani hapo,” alisema Maduga.

Naye Candy Masunzu, Meneja wa Taasisi inayojihusisha na mikopo, Bayport Tanzania ambao pia walikuwa wawezeshaji wa tamasha hilo, alisema Handeni Kwetu ni moja ya matukio makubwa yenye kuburudisha na kuelimisha sanjari na kukuza uchumi wa Taifa, huku akiwataka Watanzania kuchangamkia fursa ya mikopo kwenye taasisi yao ili wakuze uchumi wao.

Wadhamini wengine wa tamasha hilo lililoshirikisha vikundi mbalimbali vya ngoma za utamaduni wilayani Handeni, ukiacha NSSF na Bayport Tanzania ni pamoja na Phed Trans, SmartMind & Partners iliyopo chini ya Anesa Co. Ltd kwa kupitia kitabu cha ‘Ni Wakati wako wa kung’aa, Handeni Kwetu Foundation, Wait & Watch Film Company Ltd, Qs Mhonda J Apex Group of Companies Ltd na Skyblue Security and Risk Mgt Ltd na Michuzi Media Group.


No comments:

Post a Comment